3368; Thamani halisi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Thamani halisi ya kitu huwa inaamuliwa na upatikanaji wa kitu hicho.
Mara nyingi vitu vinavyopatikana kwa wingi na urahisi, thamani yake huwa ni ndogo.
Wakati vitu vinavyopatikana kwa uchache na ugumu, thamani yake ni kubwa.
Kuielewa dhana hii na kuifanyia kazi kwa vitendo, utaweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Kuna maeneo makubwa mawili ambayo unapaswa kuyatengenezea thamani kubwa kwa njia hiyo.

Eneo la kwanza ni muda.
Thamani halisi ya muda wako inategemea urahisi wa upatikanaji wake.
Kama muda wako unapatikana kirahisi, thamani yake inakuwa ni ndogo na hivyo watu kuuchezea hovyo.
Hata kama kwa nadharia utaupa muda wako thamani kubwa, uhalisia ndiyo unaoamua thamani yake halisi.

Unachopaswa kufanya ni kuupangilia muda wako wote wa siku nzima, kisha kufuata mpango huo.
Usiruhusu chochote nje ta mpango ulioweka kuingilia na kuvuruga mpango huo. Usiwape watu nafasi ya kutumia muda wako kwa mambo yasiyokuwa na tija.
Kwa kifupi ni muda wako usipatikane kirahisi kwa kila mtu.
Kufanya hivyo ndiyo kunaufanya muda wako kuwa na thamani kubwa.

Eneo la pili ni vitu unavyouza.
Thamani ya chochote unachouza haitaamuliwa na bei unayoweka, bali upatikanaji wake sokoni.
Kama unachouza kinapatikana kwa wingi na kwa urahisi, thamani yake inakuwa ni ndogo.
Hiyo ni kwa sababu kama mtu atakosa au kushindwa kwako, anaweza kupata kwa urahisi mahali pengine.

Kujenga thamani kubwa kwenye vitu unavyouza, hakikisha kuna upekee mkubwa ambao haupatikani mahali pengine isipokuwa kwako tu.
Hilo linawafanya watu walazimike kununua kwako kwa sababu kuna kitu wanachopata ambacho hawezi kukipata pengine.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti kabisa tunayoijenga, muda ni kitu ambacho tunakipa thamani kubwa sana.
Kwa sababu muda ni adimu na wenye ukomo, tunaupa thamani kubwa, kisha tunadhihirisha hilo kupitia upatikanaji wake na yale tunayofanya.

Tumekokotoa thamani ya muda wetu na kiasi tulichopata ndiyo inakuwa mchujo wa nini tunafanya na nini hatufanyi.
Ukishapata thamani ya muda wako, hupaswi kukubali kitu chochote ambacho ni chini ya thamani hiyo.

Kwenye mauzo, kila mwanajamii wa KISIMA CHA MAARIFA anatoa kitu ambacho watu hawawezi kukipata mahali pengine isipokuwa kwako tu.
Hivyo ndivyo unavyotoa thamani kubwa na kulipwa vizuri zaidi.

Kamwe usifanye kitu chochote kwa mazoea yaliyopo. Kufanya hivyo ni kujishusha thamani na kukubali kupata matokeo duni.

Tengeneza thamani halisi kwa ukubwa  kwenye mambo yote unayojihusisha nayo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwa kadiri unavyotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe