Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Utajiri Ukiwa Umelala.
Rafiki yangu mpendwa,
Bilionea Mwekezaji Warren Buffet amewahi kunukuliwa akisema kama huwezi kuingiza fedha ukiwa umelala, basi utafanya kazi kwa maisha yako yote.
Hakuna ubaya kufanya kazi maisha yako yote kama ndiyo kitu unachopenda kufanya na siyo kulazimika kufanya. Lakini kama unafanya kazi kwa maisha yako yote kwa sababu ndiyo namna pekee utaweza kuyaendesha maisha, basi umejiweka kwenye mtego mbaya sana.

Rafiki, ipo njia rahisi sana ya wewe kuweza kuingiza kipato bila ya kuhitajika kufanya kazi moja kwa moja. Njia hiyo ni kufanya uwekezaji, ambapo unawekeza mtaji wako na huo kuzalishwa na wewe kupata faida.
Kitu kizuri zaidi kuhusu uwekezaji ni kwamba kile kinachozalishwa kama faida, ambacho hata hukukifanyia kazi, kama hutakitumia na ukakiacha kwenye uwekezaji, basi na chenyewe kinakuzalishia faida.
Nikupe mfano ambao kama umekula chumvi kidogo na kukaa kijijini kwenye ufugaji utakuwa unaelewa. Chukua mfano wewe unakuwa na ng’ombe kadhaa, anakuja mtu na kukuomba umpe ng’ombe jike mmoja akamtunze na anapozaa ndama mnakuwa mnagawana. Unampa ng’ombe na yeye anaenda kumtunza, anapozaa, ndama wa kwanza anakuwa wa kwako, anayefuata wa kwake, mnaenda mkibadilishana hivyo.
Hapo unakuwa umepata ndama kwenye ng’ombe wako, bila ya wewe kumtunza ng’ombe huyo moja kwa moja. Sasa basi, unaamua hutamchukua huyo ndama, badala yake yule uliyempa aendelee kumtunza mpaka afikie kuzaa na kisha mnagawana tena hao ndama.
Ona picha linavyokuwa zuri hapo, wewe ulitoa ng’ombe, ambaye alienda kutunzwa na mtu mwingine na ukapata ndama. Hujafanya kazi yoyote kumpata ndama huyo, zaidi tu ya kuwa ng’ombe alikuwa wako. Ndama aliyepatikana, ambaye hujamfanyia kazi kabisa, naye anatunzwa na kuzaa, kisha unapata ndama kutoka kwake. Hapo unakuwa umepata ndama ambaye hakuna chochote umehusika katika kumpata.
Hivyo ndivyo imekua inafanyika miaka na miaka, kwenye jamii za wakulima na wafugaje. Wale wenye mitaji wamekuwa wananufaika kwa kujenga utajiri bila kulazimika kufanya kazi kabisa.
SOMA; Dhana Ya Riba Mkusanyiko Na Nguvu Yake Kwenye Uwekezaji.
Rafiki, dhana hiyo kwenye uwekezaji inaitwa RIBA MKUSANYIKO (COMPOUND INTEREST) na mwanasayansi Albert Einstein aliita dhana hiyo kama ajabu la nane la dunia. Ni maajabu kwa jinsi dhana hiyo ilivyo na nguvu ya kumwezesha mtu yeyote kujenga utajiri mkubwa bila ya kuhitajika kufanya kazi moja kwa moja. Kitu pekee kinachohitajika ili dhana hii ifanye miujiza kwako ni kuipa muda na kuwa na utulivu.
Rafiki, kama huijui dhana hii na hujaielewa kwa kina, basi unajisababisha kubaki kwenye umasikini kwa maisha yako. Acha kila unachofanya sasa na angalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ambapo nimeifafanua kwa kina dhana hiyo ya RIBA MKUSANYIKO na jinsi ya kunufaika nayo.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.