Rafiki yangu mpendwa,
Wajapani wanayo dhana inayoitwa OTAKU. Dhana hiyo inamaanisha kitu ambacho watu wanakuwa wanakipendelea kiasi cha kuwa tayari kuchukua hatua za ziada ili kukipata.
Ili uweze kufanya mauzo makubwa kwenye biashara yako, unapaswa kuielewa vizuri dhana hii na kuweza kuijenga kwenye pande mbili za biashara yako kama unavyokwenda kujifunza hapa.

Upande wa kwanza ni kwa wateja.
Unapaswa kujenga biashara ambayo wateja kuna kitu wanakipenda sana kwako na hawawezi kukipata kwa wafanyabiashara wengine. Hilo litawafanya wateja kuwa tayari kuingia gharama ya fedha na muda ili kununua kwako. Wanakuwa tayari kusafiri kutoka mbali ili kuja kununua na hata kunapokuwa na watu wengi, hawachoki kusubiri kupata huduma.
Umewahi kuona biashara mbili zipo eneo moja, kwenye biashara moja wateja wamepanga foleni kusubiri huduma, wakati kwenye biashara nyingine hakuna wateja kabisa, licha ya kuwa wanauza kitu kimoja.
Kwa wasioelewa huwa wanasema anayejaza wateja anatumia dawa na mambo mengine ya kishirikina. Wasichoelewa ni kwamba wenye wateja wengi kuna kitu ambacho wateja wanakipata kwake na hawajaweza kukipata kwa wengine.
Sasa turudi kwenye biashara yako, je una wateja ambao wanatoka mbali kuja kununua kwako? Una wateja ambao wapo tayari kusubiri kwenye foleni kupata huduma? Una wateja ambao wapo tayari kununua kwako kwa gharama kubwa hata kama hicho unachouza kinapatikana kwa gharama ndogo pengine?
Kama majibu ya maswali hayo ni ndiyo, unafanya kazi kubwa na nzuri. Kama majibu ni hapana, una kazi kubwa ya kufanya. Anza kwa kuchagua ni kitu gani ambacho biashara yako inaweza kuwapa wateja ambacho hawataweza kukipata mahali pengine popote. Hilo linawezekana kabisa kama utakuwa tayari kuwapa wateja thamani zaidi bila kuangalia unapata nini kwanza.
Anza kwa kuwaangalia wateja wako na jiulize ni thamani gani unayoweza kuongeza kwenye maisha yao na hawawezi kuipata mahali pengine. Anza kuwapa thamani hiyo na utakuwa umejenga Otaku kwenye biashara yako.
SOMA; Ngazi Ya Sita; Mteja Shabiki
Upande wa pili ni kwa wafanyakazi wa biashara.
Wateja wa kwanza kabisa kwenye biashara yako ni wafanyakazi unaowaajiri kwenye biashara hiyo. Kama wao wenyewe hawaamini na kukubali sana kile kinachouzwa, hawataweza kuwashawishi wateja waamini na kukubali kununua.
Hivyo una wajibu mkubwa wa kujenga timu ya biashara yenye wafanyakazi ambao wanaelewa vizuri kila kinachouwa, wanakipenda na kukikubali. Wao wanapaswa kuwa wateja wa kwanza wa kutumia kile mnachouza na kama siyo kitu wanachoweza kutumia basi wawe wa kwanza kupendekeza kwa watu wao wa karibu kutumia.
Unataka timu ya wafanyakazi wa biashara ambao wana shauku kubwa kwao wenyewe na kwa biashara, ambao wanajiona wakiwa na wajibu wa kuwahudumia vizuri na kuwapa thamani kubwa.
Hupaswi kuwa na timu ya watu ambao hawawezi kutekeleza majukumu yao mpaka uwasukume. Ambao hawajisumbui kuhakikisha wateja wamepata huduma bora. Hao wataikwamisha biashara yako kuuza zaidi.
Weka viwango vya juu vya aina ya watu utakaowaajiri kwenye biashara yako na kuwapa nafasi ya kukua zaidi. Lazima wawe wanaopenda kweli kile wanachofanya na wana msukumo mkubwa wa kufanya. Ambao wapo wapo tu na hawajielewi wanataka nini kwenye maisha, hupaswi kuwaruhusu wasogee karibu na wateja wa biashara yako, maana watawafukuza.
Na hili siyo tu kwa watu wa mauzo, bali kwa watu wote waliopo kwenye biashara yako. Kwa sababu kile ambacho kila mtu anafanya kwenye biashara, kinamgusa mteja kwa namna moja au nyingine. Hata anayefanya usafi, kama hana mapenzi na kazi yake, atawaona wateja kama kisirani kwake, wanaochafua eneo analosafisha.
Fanyia kazi maeneo hayo mawili na utaweza kujenga biashara yenye mauzo makubwa na itakayofanikiwa sana pia.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumejadili kwa kina dhana hii ya Otaku na kukuza mauzo. Fungua uweze kujifunza na kwenda kuchukua hatua ili kukuza mauzo yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.