Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako. Na tulijifunza kanuni ya kwanza ambayo ni njia pekee ya kushinda mabishano ni kuyaepuka.
Na hapa tuliondoka na kitu kimoja ambacho ni njia pekee ya kushinda mabishano ya aina yoyote ile ni kuyaepuka, usikubali kabisa kuingia kwenye mabishano. Unapaswa kuepuka mabishano kama vile nyoka au ajali.
Soma hapa; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Kwanza
Habari njema ni kwamba, leo tunakwenda kujifunza sehemu nyingine ambayo ni jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako sehemu ya pili.
Dale anatuambia njia ya uhakika ya kutengeneza maadui kwenye maisha yako ni kuwaambia watu wamekosea au hawako sahihi, hata kama ni kweli.
Watu wanathamini sana kile wanachosimamia, hivyo unapowakabili kwa kuwaeleza kwamba wanakosea na hawako sahihi, unaumiza nafsi zao na hivyo watakuchukia kwa hilo.
Hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kuwa sahihi mara zote, Theodore Roosevelt aliyekuwa raisi wa Marekani, akiwa raisi aliwahi kunukuliwa akisema, kama angeweza kuwa sahihi kwa asilimia 75 tu, angefanya makubwa sana. Na hata kwa mtu wa kawaida, ukiweza kuwa sahihi kwa asilimia 55 tu ya maamuzi yako, utaweza kufanya makubwa.
Lakini, hakuna anayeweza kuvuka asilimia 50 kwenye usahihi, unapata wapi ujasiri wa kuwaambia wengine hawapo sahihi?

Unapowaambia watu wamekosea au hawapo sahihi, ni kama umewakutana, umewaambia ni wajinga na hakuna wanachojua. Umewadhalilisha utu wao na kile wanachosimamia, hawatapokea hilo kwa urahisi, watahakikisha wanapambana kulinda heshima zao. Haijalishi utawapa hoja gani kwamba wakekosea , hawatakubali.
Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea na kwa sababu kila mtu ni muuzaji, unapokutana na mtu ambaye anakuambia kile ambacho unajua siyo sahihi au kweli, usimjibu kwa kumwambia hauko sahihi au kumwonesha ni kwa namna gani anakosea, badala yake elewa kwa nini anaamini anachoamini, kisha tafuta njia ya kumfanya yeye mwenyewe auone ukweli, siyo wewe kumwonesha ukweli.
Watu wote wenye hekima walijua hili na walilitumia vizuri.
Papa Alexander aliwahi kunukuliwa akisema, wafundishe watu bila ya kuonekana unafundisha na kama mtu hajui kitu, mwoneshe amesahau, siyo hajui.
Galileo naye akasema, huwezi kumfundisha mtu kitu chochote, bali unaweza kumsaidia mtu kujifunza anachotaka kujua.
Lord Chesterfield alimuusia mtoto wake; kuwa mwenye hekima kuliko wengine, lakini usiwaambie.
Na mwanafalsa Socrates aliwahi kusema, najua kitu kimoja pekee, kwamba hakuna ninachojua.
Kama mtu anaongea kitu ambacho unajua siyo sahihi, au kweli usianze kwa kumwambia siyo sahihi au siyo kweli.
Badala yake msikilize amalize kuongea, kisha mwambie; “Mimi nilikuwa nafikiri tofauti, lakini naweza kuwa ninakosea, maana mara nyingi huwa ninakosea. Kama nimekosea ningependa kurekebishwa, hebu tuangalie ukweli kwenye hili.”
Kwa kutumia kauli ya aina hii, hakuna anayeweza kubishana na wewe kwa kukiri unaweza kuwa unakosea na kuwa tayari kujifunza kama hauko sahihi, inamfanya mtu awe tayari kukupa ushirikiano na kisha kwa pamoja mnaweza kuona ukweli uko wapi.
Hata kama una uhakika wa asilimia 100 kwamba uko sahihi, haitakusaidia kama utamwambia mtu wazi kwamba amekosea.
Lakini kwa kuanza kukiri kwamba unaweza kuwa umekosea, utampa mtu nafasi ya kuuona ukweli mwenyewe na kisha kuchukua hatua ya kubadilika atakapoujua ukweli.
Kwa wewe kuanza kukubali kwamba unaweza kuwa umekosea, unamfanya mwingine naye awe tayari kubadilika atakapoujua ukweli.
Kuwaambia watu wazi kwamba wamekosea, hata kama ni kweli, ni kama vile kummwagia pombe mlevi, hata kuelewa kwa kweli, lazima atakuzingua kwa namna yoyote ile kukuonesha kwamba yeye yuko sahihi.
Kuwaambia watu wazi kwamba wamekosea huwa haisaidii kwa sababu sisi binadamu huwa hatufanyi maamuzi yetu kwa fikra, bali tunafanya kwa hisia kisha tunakuja kuhalalisha kwa fikra.
Huwa tunakimbilia kuhukumu kabla ya kuchunguza.
Wengi tunasukumwa na hisia za wivu, hofu, chuki na ufahari na huwa hatupo tayari kubadili misimamo yetu kwenye ya dini, siasa, michezo na mengine tunayoshikilia.
Mwanasaikolojia Carl Rogers amewahi kuandika, ni muhimu sana mtu ujifunze kuwaelewa wengine, kabla hujafanya maamuzi. Kwa sababu mara nyingi huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia kabla hatujajipa nafasi ya kumwelewa mtu.
Pale mtu mwingine anapoongea, huwa hatutafakari na kuelewa bali huwa tunahukumu, “ni kweli, ni ujinga, hajui, haipendezi, hamna kitu na kadhalika.
Mtu anapotambua amekosea, anaweza kukubali na kuchukua hatua za kubadilika. Lakini anapoambiwa amekosea hilo huwa linaumiza na kutafuta jinsi ya kujitetea kwenye kile anachoambiwa amekosea.
Wasaidie watu kuuona ukweli, usiwaambie wamekosea au hawako sahihi.
Kitu kimoja zaidi, kadiri unavyokuwa na hekima, ndiyo unavyokuwa mgumu kujifunza. Kwa sababu unajua vitu vingi ni rahisi kuona wengine wanakosea na unatamani kuwaonesha kwamba wanakosea.
Hilo litawafanya watu waepuke kufanya maongezi na wewe kwa sababu wanajua utawakosoa.
Hivyo basi, kuwa makini kadiri unavyojua zaidi, ndivyo unavyopaswa kujifanya mjinga zaidi.
Epuka kuwaambia watu wamekosea hata kama una uhakika na hilo, badala yake tengeneza mazingira ya kumsaidia mtu kuuona ukweli yeye mwenyewe.
Kwa njia hiyo, watu watafurahia kuongea na wewe kwa sababu wanajua unawasaidia kuona ukweli.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz