Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye programu yetu ya mafunzo ya mauzo inayoitwa CHUO CHA MAUZO, kauli mbiu yetu ni KILA MTU NI MUUZAJI. Hivyo wewe hapo rafiki, kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, unauza. Unauza kwa sababu kuna namna unataka kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe.
Watu wanaofanikiwa kwenye maisha ni wale wanaopata kile wanachotaka na wanaopata kile wanachotaka ni wale wenye ushawishi mkubwa. Hivyo basi rafiki, unajionea mwenyewe hapo kwa nini mafanikio kwenye maisha yako yanategemea sana wewe kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea.

Hata bila ya kujifunza zaidi kuhusu mauzo, tayari kuna vitu unajua, ambavyo vimekuwa vinakusaidia kuwashawishi watu wakubaliane na wewe. Kama upo kwenye biashara, kuna namna unajua ya kuendana na wateja wako ambayo inawafanya wakubali kununua kwako. Kadhalika kama umeajiriwa au kujiajiri, kuna namna umekuwa unafanya kazi zako na kuwa na ushawishi kwa wengine.
Ninachomaanisha hapa ni kuna mambo ambayo umekuwa unayafanya vizuri, hongeza sana kwa mambo hayo. Swali ambalo nataka ujitafakari nalo, ni kwa nini hayo unayoyafanya vizuri huyafanyi kwa ukubwa zaidi? Kwa nini umeridhika na matokeo unayopata sasa na usiyaendee matokeo ambayo ni makubwa zaidi? Je umewahi kujiuliza maswali hayo na kujipa majibu ya kina?
Utakubaliana na mimi kwamba kama umeweza kufanya hivyo unavyofanya sasa, basi pia unaweza kufanya zaidi ya unavyofanya sasa. Ndiyo maana ni muhimu kwako kutafakari nini kinakuzuia usifanye zaidi ya unavyofanya sasa.
Na hapa ndipo ninapotaka nikuonyeshe kitu kimoja ambacho umekuwa unakipenda sana na hicho ndiyo kimekuwa kikwazo kwako kufanya zaidi ya unavyofanya sasa na kuweza kupata matokeo makubwa.
SOMA; Ukifanya Kitu Hiki Kimoja, Utakuza Zaidi Mauzo Yako.
Kama unaweza kuwauzia wateja 10, nini kinakuzuia usiwauzie wateja 100? Uvivu inaweza kuwa sababu moja, kwa sababu hutaki kuweka kazi zaidi ili kuwafikia wengi. Lakini nikuulize swali jingine, kama wateja 100 watakuja wenyewe, utaacha kuwauzia? Utawaambia ondokeni mimi naweza kuwauzia wateja 10 pekee? Jibu ni hapana, utawauzia kwa furaha kabisa.
Kumbe basi unaweza kuwauzia wateja wengi kuliko unaowauzia sasa, sasa mbona huwauzii hao wengi? Ni kwa sababu mchakato wa kuwapata hao wengi unazuiwa na hicho ambacho umekuwa unakipenda.
Iko hivi rafiki yangu, ili uweze kuwauzia wateja wengi, ni lazima uwafikie wengi sana na uwafikie mara kwa mara hata kama wanakataa kununua. Kwa maneno mengine ya wazi ni kwamba unatakiwa KUPIGA KELELE na KUWA MSUMBUFU. Unapiga kelele kwa kuwafikia wengi zaidi, kuhakikisha kila wakati watu wapya wanajua kuhusu uwepo wako. Na unakuwa msumbufu kwa kung’ang’ana na wale ambao umeshawafikia mpaka wakubali kununua, hata kama wanasema hapana.
Hayo ndiyo mahitaji makubwa mawili ya kuuza zaidi, KELELE na USUMBUFU. Nikirudi tena kukuuliza swali, na leo utanisamehe kwa maswali mengi ninayokuuliza ujiulize, nini kinakuzuia kupiga kelele na kuwa msumbufu? Wewe si kuna wakati au maeneo ambayo huwa unaonekana una kelele na usumbufu? Kwa nini hupeleki hayo kwenye mauzo ili uweze kuuza zaidi?
Rafiki kitu kimoja ambacho umekuwa unakipenda sana, kimekuwa kinakukwamisha usipige kelele na kuleta usumbufu. Kitu hicho ni kutaka kuonekana wewe ni MSTAARABU. Ustaarabu ni dhana ambayo imekuwa inachukuliwa tofauti na matokeo yake kuwa kikwazo kwa mtu kupiga hatua kubwa kwenye maisha. Ustaarabu umekuwa gereza ambalo watu wanajifungia na kujikwamisha kufanya makubwa.
Leo nataka tukubaliane kitu kimoja, ili usiendelee kutumia ustaarabu kujikwamisha kufanya makubwa. Ninachotaka ufanye ni kubadili maana ya ustaarabu kwako. Kuanzia sasa, maana ya ustaarabu kwako ni hii; KUPATA KILE UNACHOTAKA BILA YA KUVUNJA SHERIA. Ni hivyo tu, na hakuna cha ziada.
Kwa maana hiyo basi, kama hujapata unachotaka, wewe siyo mstaarabu. Hivyo fanya kila kinachopaswa kufanyika ili uweze kupata kile unachotaka. Usijizuie na ustaarabu uchwara wa kutaka kuonekana na wengine kwa namna fulani, wakati ndani yako unajua hujafika unakotaka kufika.
Kama hujapata kile unachotaka, tumia kila njia ambayo haivunji sheria za msingi zilizopo kuhakikisha unakipata. Usijali sana wengine wanakufikiria au kukusemaje, hiyo ni biashara yao, wewe kazana na biashara yako kuu ambayo ni kupata kile unachotaka.
Rafiki, ukiweza kuachana na ustaarabu uchwara ambao umekuwa unajipachika, utaweza kufanya makuba sana kwenye biashara, kazi na maisha kwa ujumla. Kuwa na njaa kali na endesha mapambano yasiyo na mapumziko yatakayokupa kile unachotaka.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha kwa kina zaidi jinsi ya kuondokana na ustaarabu uchwara ili uweze kupata kila unachotaka kwenye maisha yako. Karibu ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.