Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Moja ya masomo tunayopata kwenye mauzo ni ya MAENDELEO BINAFSI ambayo yanatujenga sisi kuwa bora na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yetu kufanya mauzo makubwa.
Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.
Kwenye somo hili unakwenda kujifunza kuhusu kuwa mbunifu ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Ubunifu ni eneo muhimu lakini ambalo wengi wamekuwa hawalifanyii kazi na hivyo kujizuia kufanikiwa kwenye maisha.

KILA MTU NI MBUNIFU.
Watu wengi wamekuwa wanashindwa kuwa wabunifu kwenye maisha yao kwa kudhani ubunifu ni kitu cha watu wachache. Huwa wanachukulia kuna watu wachache ambao wamezaliwa na ubunifu na wengine hawana ubunifu.
Ukweli ni kwamba kila mtu ni mbunifu. Na kila mtu amekuwa anatumia ubunifu wake pale inapohitajika kufanya hivyo. Angalia kwenye uvaaji wa mavazi, kila mtu anajua jinsi ya kupangilia mavazi yake ili kuwa na mwonekano mzuri, huo ni ubunifu. Kadhalika mtu ukiwa unataka kuwahi mahali, utatafuta njia za mkato za kukufikisha pale haraka, huo ni ubunifu.
Kila mmoja wetu amewahi kutoka nje ya mazoea fulani ili kupata kile anachotaka, huo ndiyo ubunifu wenyewe. Na hicho ni kitu ambacho umekuwa unakifanya mara kwa mara, japo umekuwa huoni kama ni ubunifu.
Hapa anza kwa kujiambia wewe ni mbunifu, ili sasa uweze kutumia ubunifu wako kufanya makubwa.
UBUNIFU UNAANZA NA ULICHONACHO.
Kitu kingine ambacho kimekuwa kinawakwamisha watu kuwa wabunifu ni kudhani kuna wakati fulani au mahali fulani pa kuwa na ubunifu. Wengi hudhani ubunifu ni mpaka ukae mahali na kuanza kutafuta mawazo ya kibunifu. Ujifungie mahali na kufikiri kwa kina kisha kuandika mawazo ya tofauti ambayo unayapata. Mtazamo huo kuhusu ubunifu umekuwa kikwazo kwa wengi kutumia ubunifu ambao tayari upo ndani yao.
Ubunifu huwa unaanza na kile kinachokuwa mbele yako, kwa wakati ambao umekutana nacho. Yaani ubunifu siyo kitu ambacho unakipangia muda wa kufanya, bali ni kitu ambacho unakifanya kulingana na hali unayokuwa umekutana nayo.
Kama kuna mahali unataka kwenda, ukisema ukae chini kwanza na kuja na ubunifu wa kufika unakotaka, litakuwa zoezi gumu sana. Lakini kaa utaianza safari, kisha mbele ukakutana na kikwazo, hapo ndiyo unapaswa kufikiria njia gani ya tofauti utumie ili kufika unakotaka. Kukabiliana na kile kilicho mbele yako ndipo ubunifu unapohitajika.
Acha kufikiria ubunifu kama kitu cha kutenga muda wa kukifanya, bali kwenye kila jambo au hali unayokutana nayo, jiulize unawezaje kupata matokeo unayoyataka kwa uhakika zaidi. Huo ndiyo ubunifu, kutumia kile unachokabiliana nacho kupata matokeo unayokutana nayo.
Kwa maneno mengine, ubunifu ni kugeuza kikwazo kwenye njia kuwa ndiyo njia yenyewe. Yaani kile ambacho kinakuzuia usipate unachotaka, unakigeuza kuwa ndiyo njia ya kukipata. Ukiweza hilo, hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata chochote unachotaka.
SOMA; Jinsi Ya Kukuza Mauzo Mara Mbili Kwenye Biashara Yako.
GAZIJUTO KWENYE UBUNIFU.
Kwenye hisabati huwa kuna kifupisho cha GAZIJUTO, ambapo ni GA (gawanya), ZI (zidisha), JU, (jumlisha) na TO (toa). Sehemu kubwa ya hesabu unazohitaji kuyaendesha maisha yako inakamilishwa na hilo.
Hivyo pia ndivyo ubunifu ulivyo, kama tulivyoona hapo juu, ubunifu unaanzia na kile ambacho umekutana nacho. Na jinsi ya kutumia unachokutana nacho kuwa na ubunifu ni kutumia hiyo kanuni ya GAZIJUTO.
Kwa kila unachokutana nacho, jiulize maswali haya na kujipa majibu;
GA; Nini unachoweza kugawanya kwenye kitu hicho ili kupata matokeo unayotaka?
ZI; Nini ambacho ukikizidisha kitakuletea matokeo ambayo unataka?
JU; Nini ambacho ukiongeza kwenye kitu hicho utaweza kupata matokeo unayoyataka?
TO; Nini ambacho ukiondoa au kupunguza kwenye kitu hicho utapata matokeo unayotaka?
Kwa kujiuliza maswali hayo na kujipa majibu, utaweza kuona njia tofauti za kukuwezesha kupata kile unachotaka.
KUGEUZA NA UBUNIFU.
Kanuni nyingine muhimu kwenye ubunifu ni kugeuza. Mara nyingi tunapokuwa tunataka kupata kitu, huwa tunajiuliza tunawezaje kukipata, hapo tunapata majibu ya nini tunapaswa kufanya.
Unaweza kugeuza swali na ukapata majibu ambayo yatakupa hatua za kibunifu za kuchukua ili kupata matokeo unayotaka. Badala ya kujiuliza unawezaje kupata unachotaka, unajiuliza UNAWEZAJE KUKOSA UNACHOTAKA.
Kwa kujiuliza jinsi ya kukosa kila unachotaka, utapata majibu ya vitu vya kuepuka ili usikose unachotaka. Na ukiyaepuka hayo, moja kwa moja unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kukipata.
Charlie Munger alikuwa na usemi wake maarufu kwamba; ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa ili nisiende hapo. Hiyo ni njia ya kugeuza ili kupata unachotaka kwa kuepuka kukipoteza.
USHINDANI NI KUKOSA UBUNIFU.
Watu wengi wamekuwa wanalalamikia ushindani kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yao. Ushindani umekuwa unaonekana kama kikwazo kwa watu kufanikiwa. Lakini tukiangalia kwa undani, ushindani ni ukosefu wa ubunifu. Unapata ushindani kwa sababu umewaiga wengine kile wanachofanya au wengine wamekuiga wewe.
Njia ya uhakika ya kuushinda ushindani ni kuwa mbunifu. Kwa kila mara kujiuliza maswali ya kibunifu uliyojifunza hapa, utaweza kuona njia za kufanya vitu kwa namna ya tofauti ili uwe tofauti na wengine wanaofanya.
Ukiweza kutumia ubunifu ambao tayari upo ndani yako, watu wataishia tu kushangaa kwa nini licha ya kufanya kama wewe, bado hawapati matokeo ambayo wewe unayapata. Hiyo ni kwa sababu unakuwa mbele yao mara zote, kile unachofanya leo, wakati wao wanaiiga kesho, wewe hiyo kesho unafanya kingine tofauti.
UBUNIFU KWENYE MCHAKATO WA MAUZO.
Kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO tuna mchakato ambao tunaufanyia kazi kwa msimamo bila kuacha. Kwa sababu mchakato ni wa kujirudia rudia, unaweza kuona hauhitaji ubunifu. Lakini siyo kweli, huko kwenye kurudia rudia mchakato wa mauzo, kunahitaji ubunifu mkubwa kama unataka kupata matokeo makubwa na ya tofauti.
Mchakato wetu wa mauzo una vipengele vikuu ambavyo ni USAKAJI, UKAMILISHAJI, UHUDUMIAJI na UFUATILIAJI. Na pia kuna vipengele vingine vidogo vidogo. Kwenye hivi vipengele vikuu, jiulize maswali ya kuboresha kila unavyofanya.
Kwa mfano kama unamfuatilia mteja lakini mara zote hapokei simu yako au akipokea anakata, unahitaji kuwa na ubunifu zaidi ili kuhakikisha unampata. Unaweza kulazimika kumtembelea kule alipo, kutuma ujumbe, kumpa zawadi, kumfuatilia kwenye mitandao ya kijamii anayotumia na kujua mambo anayopendelea na kisha kutumia hayo kumfikia. Huo ni mfano mmoja tu ambao unaona jinsi kufikiri kwa utofauti kunakupa njia nyingi za kukamilisha kile unachofanya.
Kwa kila unachofanya, jiulize maswali ya namna gani unaweza kufanya kwa ubora zaidi ili kupata matokeo bora. Kwa mfano kwenye uhudumiaji, lengo ni kutoa huduma bora kwa wateja ili ubaki nao kwa muda mrefu. Ukiangalia upande wa nini cha kufanya, kuna vitu unaweza usivione na ukapoteza wateja, licha ya kukazana kuwapa huduma nzuri. Ukitumia njia ya ubunifu ya kugeuza, unaweza kujiuliza ni vitu gani ukifanya utawapoteza wateja, kisha kuepuka kufanya vitu hivyo na kuweza kubaki na wateja kwenye biashara yako kwa muda mrefu.
SOMA; Jikubali Wewe Mwenyewe Ili Uweze Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
ACHILIA BREKI ZINAZOKUZUIA KUWA MBUNIFU.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, nataka nitabiri kitu hapa. Umejifunza na kukubali kwamba wewe ni mbunifu. Na umejifunza njia za kufanya ubunifu kwenye mchakato wako wa mauzo. Lakini bado utatoka hapa na kuendelea na mazoea yako, bado hautakuwa mbunifu. Naweza kuweka dau na nikashinda.
Kwa nini natabiri hivyo? Kwa sababu najua kuna breki zinazokuzuia wewe usiwe mbunifu. Unajua kabisa kwamba unatakiwa kuwa mbunifu, unaziona kabisa fursa za kuwa mbunifu, lakini bado unafanya kwa mazoea.
Breki kuu inayokuzuia usiwe mbunifu ni HOFU. Kila unapofikiria kufanya kitu cha tofauti, unaingiwa na hofu kwa sababu unakuwa huna uhakika wa matokeo utakayoyapata. Hivyo unajikuta ukiendelea kufanya yale uliyozoea kufanya kwa sababu yanakupa matokeo ambayo unayategemea.
Ili uweze kuwa mbunifu, itumie hofu kama kichocheo cha ubunifu. Pale unapopanga kufanya kitu cha tofauti, halafu ukaingiwa hofu inayokuzuia kukifanya, jiambie hicho ndiyo unapaswa kufanya na hakikisha unakifanya.
Unapofanya kile unachohofia, kwanza kabisa unaiua hofu na pili unapata matokeo ambayo hujawahi kupata. Na hata kama matokeo utakayoyapata siyo kama ulivyotarajia, una nafasi ya kuendelea kutumia ubunifu na kuyaboresha mpaka kupata matokeo mazuri.
Ondoka hapa ukiwa umechochea ubunifu mkubwa ambao tayari unao na kuutumia kwenye mauzo ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.