3373; Njia ya haraka ya kuleta mapinduzi.


Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kutoka hapo ulipo sasa na kufika kwenye mafanikio makubwa, kazi kubwa sana inapaswa kufanyika.
Licha ya kwamba inawezekana, kwa sehemu kubwa ya watu itawashinda.
Hiyo ni kwa sababu walio wengi hawajajitoa kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili kupata wanachotaka.

Njia ya haraka inayohitajika ili kuleta mapinduzi makubwa ni kuboresha uwezo wa watendaji.
Wale wanaotekeleza majukumu mbalimbali kwenye kile unachofanya, wanapaswa kuwa na uwezo wa kufanya makubwa kwenye eneo hilo.
Wanapaswa kuwa watu wenye uwezo mkubwa na ambao wanajisukuma hasa kutumia uwezo huo ili kufanya makubwa.

Matokeo ambayo watu wanayapata, huwa yanaanzia kwenye uwezo wa watendaji wanaozalisha matokeo hayo.
Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha mara zote timu ya watendaji ipo kwenye hali nzuri, kwa sababu inahitajika sana kwenye kupiga hatua.

Kuboresha timu yako ya watendaji, mamho matatu yanapaswa kuwa yanafanyika kwa mwendelezo mara zote.
Moja ni kuajiri watu wenye uwezo mkubwa.  Zoezi la kuajiri linapaswa kuwa endelevu ili unapokutana na mtu mzuri, unamshawishi kuungana na wewe.

Mbili ni kutoa mafunzo endelevu ya kuwajengea ubora kwenye kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo ni muhimu sana na yanapaswa kuwa endelevu na yanayowaacha watu wakiwa bora kuliko walivyokuwa awali.

Tatu ni kuwaondoa wale ambao kasi yao haiendani na kasi iliyopo. Kuwachuja na kupata walio bora na kuwapa mafunzo endelevu, bado haimaanishi wote watazalisha matokeo yanayotegemewa.
Kuna ambao bado watashindwa kwenye hilo.
Na hapo ndipo hatua za kuwaondoa zinapopaswa kuchukuliwa ili wasiendelee kurudisha nyuma juhudi kubwa zinazowekwa na wengine.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kujenga timu imara ni hitaji la msingi kwenye kujenga biashara inayojiendesha yenyewe kwa mafanikio.
Mara zote tupo kwenye mchakato wa kupata walio bora, kuwapa mafunzo na kuwaondoa wasio sahihi.

Ili zoezi hilo liwe na mafanikio, lazima wewe mmiliki wa biashara uwe umejijengea uwezo mkubwa sana.
Kwa sababu mtu anaishia kuwavuta kwake watu wanaoendana na yeye.
Kama wewe mwenyewe hufanyi makubwa, unaowapata pia hawataweza kufanya makubwa na utaishia kuwavumilia kwa sababu ndivyo na wewe ulivyo.

Ni lazima uanze kujiwekea viwango vikubwa na kupambana kuvifikia ili uweze kujenga timu yenye viwango vikubwa pia.
Na timu hiyo yenye viwango vikubwa ndiyo itakayoleta mapinduzi makubwa kwenye kile kinachofanyika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe