Rafiki yangu mpendwa,

Lengo kubwa la kila mmoja wetu kwenye maisha ni kuwa huru. Hatua nyingi tunazochukua kwenye maisha, lengo lake ni kupata uhuru zaidi. Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa hawana uelewa sahihi kwenye uhuru wanaoutafuta.

Hilo limekuwa linasababisha changamoto mbili kubwa. Ya kwanza ni watu kujiwekea vikwazo vinavyowazuia wasipate uhuru wanaokuwa wanaupambania. Na ya pili ni kupata uhuru waliokuwa wanaupambania, ila wakashindwa kuufurahia. Kwa changamoto hizi mbili, sehemu kubwa ya watu wamekuwa hawapati uhuru kwenye maisha yao, licha ya kuweka juhudi kubwa kwenye hilo.

Kwa changamoto ya kwanza, watu wamekuwa wanajiwekea vikwazo vinavyowazuia kupata uhuru, kwa sababu wanakuwa hawajui maana halisi ya uhuru wanaoutaka. Watu wengi wamekuwa wanadhani kwamba uhuru ni kuwa na kipato kikubwa kuliko wanavyohitaji. Hivyo wanaweka juhudi kubwa kwenye kazi na biashara zao, na kweli wanaongeza sana kipato chao. Lakini kwa bahati mbaya sana, kadiri kipato kinavyokuwa kikubwa, ndivyo pia kazi na biashara hizo zinavyokuwa zinahitaji muda wao mwingi. Hiyo inawapelekea watu kuwa na kipato kikubwa sana, lakini hawana muda hata wa kukifurahia kipato hicho.

Uhuru kamili wa maisha unahusisha mtu kuweza kuamua yeye mwenyewe bila ya kulazimishwa na mtu yeyote mambo haya manne;

Moja ni nini ambacho anafanya. Hapa mtu anakuwa huru kuchagua ni nini afanye, halazimiki kufanya ambacho hataki kufanya. Ukiwa na kipato kikubwa ambacho kinategemea wewe ufanye kazi au biashara, unakuwa unakosa uhuru huu. Hivyo lazima uhakikishe kipato kikubwa unachoingiza hakitegemei wewe kufanya moja kwa moja.

Mbili ni wakati wa kufanya. Kuchagua tu cha kufanya bado haitoshi kukuweka huru, lazima pia uweze kupangilia muda wako kwa namna unavyotaka wewe. Hivyo hulazimiki kutumia muda kwa namna ambayo wewe hutaki. Hapa ndipo unaamka muda unaotaka na kulala muda unaotaka. Kama kipato chako kikibwa bado kinakutaka uwe mahali fulani kwenye muda fulani la sivyo kipato kinaathirika, hicho kinakunyima uhuru. Pata uhuru wa kupangilia muda wako kwa namna inavyokufaa wewe.

Tatu ni wapi unafanyia. Wengi wenye kipato kikubwa kinachotokana na kazi au biashara, lazima wawepo kwenye kazi au biashara zako kila siku kwenye muda wote wa kazi. Hawawezi hata kusafiri kwa muda mrefu bila ya kipato chao kuathiriwa na hilo. Unapaswa kujenga uhuru ambao unakuwezesha kusafiri kwenda popote na hilo lisiathiri kabisa kipato chako.

Nne ni nani unafanya naye. Kuna watu ambao huwezi kuendana nao kwenye maisha, iwe ni kwenye kushirikiana nao kwenye kazi au kuwa wateja wako. Kama huna uhuru wa kuachana na wale ambao huwezi kuendana nao, kama inabidi uwavumilie tu kwa sababu huna namna ya kuwaacha, hujawa huru. Unapaswa kuwa na uhuru wa kuchagua nani utaendelea nao na nani utaachana nao ili uweze kuyafurahia maisha yako.

Kwa mara zote kuzingatia maeneo hayo manne na kuangalia nini ufanye ili kuwa huru kwenye kila eneo, ndiyo unaweza kujenga uhuru mkubwa wa maisha yako.

SOMA; Wakishakulipa, Wanakupangia Cha Kufanya, Na Hapo Ndipo Unapoteza Uhuru Wako.

Eneo la pili ni kushindwa kufurahia uhuru baada ya kuupata.

Kwa baadhi ya watu, mapambano wanayoweka yanawapelekea kupata uhuru. Wanakuwa wamefikia ngazi ambayo hawahitajiki kufanya chochote. Na hapo ndipo shida huwa zinaanzia, kwa sababu hawajazoea kukaa bila kufanya chochote.

Mwanzoni wanafurahia uhuru wanaoupata na kufanya yale yote waliyokuwa na ndoto za kuyafanya. Lakini baada ya muda mfupi wa kufurahia uhuru, wanaanza kupata hofu na wasiwasi juu ya maisha yao, kwa sababu hawajazoea kukaa bila kitu cha kufanya. Ni hali hiyo ya hofu na wasiwasi ndiyo inawafanya wasiyafurahie maisha. Wengine huenda mbali zaidi na kuanza kufanya chochote kinachokuja mbele yao na kupelekea hata kuharibu biashara na uwekezaji ambao walikuwa tayari wameshajenga.

Kuondokana na hiyo hali ya kutokuweza kutulia na uhuru ambao umeujenga, unapaswa kuwa na mambo ambayo yataendelea kukutinga hata baada ya kuwa huru. Yanaweza yasiwe yanayohusu kazi au biashara moja kwa moja, bali yanapaswa kuwa mambo ambayo yanakupa changamoto ya kukutaka uweke juhudi zaidi.

Baadhi ya mambo ambayo mtu unaweza kuyafanya ni kuboresha mahusiano yako na watu wengine, kujifunza endelevu na kuifanya dunia kuwa bora zaidi ya ilivyo sasa. Hapa unahitaji kuwa na maono makubwa ambayo yanaendelea kukuamsha kila siku ukiwa na shauku ya kwenda kupambana zaidi. Hivyo ndivyo utakavyoweza kufurahia uhuru wako na maisha yako yakaendelea kuwa na maana kubwa kwako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumejadili kwa kina eneo hili la kujenga uhuru kamili wa maisha kutoka kwenye kitabu cha 4 HOUR WORKWEEK kilichoandikwa na Tim Ferriss. Karibu ufungue kipindi hicho na ujifunze ili kuweka juhudi sahihi za kukujengea uhuru unaoutaka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.