Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.

Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.

Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Kila wakati kwenye biashara ni wa kusaka wateja wapya na hivyo kila muuzaji anapaswa kutumia njia mbalimbali kukamilisha hilo.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafikia wateja wengi kwa kutumia maudhui ya mitandao ya kijamii.

ZAMA ZA TAARIFA.

Dunia imepitia zama mbalimbali ambapo kwenye kila zama huwa kuna nyenzo kuu ya uchumi. Kwenye zama za mawe, mawe ndiyo yaliyozalisha zana zote muhimu. Kwenye zama za chuma, chuma ikatawala. Kwenye mapinduzi ya viwanda, waliomiliki viwanda ndiyo waliomiliki uchumi.

Na sasa tupo kwenye zama za taarifa, ambapo taarifa ndiyo nyenzo kuu. Katika matajiri wakubwa duniani, wengi wamefika kwenye utajiri huo kwa kutumia nyenzo ya taarifa. Ukiangalia wamiliki wa mitandao ya kijamii kama Mark Zuckerberg wa Facebook na wamiliki wa masoko makubwa ya mtandaoni kama Jeff Bezos wa Amazon, hawa wote nyenzo yao kuu ni taarifa.

Hivyo kwenye hizi zama, nyenzo kuu ni taarifa. Na tunayo bahati nzuri sana kwa sababu kila mmoja anaweza kuingia kwenye matumizi ya nyenzo hiyo kuu, kupitia mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii imekuwa inatumiwa na watu wengi na kwa jinsi ilivyotengenezwa, imekuwa na uraibu mkubwa kwa wengi. Watu wengi wamekuwa wanajikuta wanaitumia kwa kupitiliza, kiasi cha kushindwa kujizuia.

Wakati wengine wanalalamikia mitandao hiyo kama changamoto kwao, wewe muuzaji unapaswa kufurahia hilo, kwa sababu inakupa fursa ya kuweza kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja. Kwa kuwa watu wameganda kwenye mitandao hiyo kwa muda mrefu, inakupa wewe fursa ya kuwafikia kwa uhakika na kuwashawishi wanunue kile unachouza.

NGAZI YA KUINGIA KWENYE TAARIFA.

Kwenye zama hizi za taarifa, kuna ngazi mbalimbali za kuingia na kunufaika kunategemea ngazi gani unaingia.

Ngazi ya kwanza na ambayo ni ya chini ni kuwa mlaji wa taarifa zilizopo. Hii ni ngazi ya watumiaji wa chini kabisa ambao ndiyo huishia kupata uraibu wa taarifa nyingi wanazokutana nazo.

Ngazi ya pili ni ya uzalishaji wa taarifa. Hii ni ngazi ya kati ambapo watu wanazalisha taarifa na hivyo kuwa na ushawishi kwa wale wanaozipokea. Hii ndiyo ngazi ya wasanii na wengine wanaotumia taarifa kuwafikia wengi.

Ngazi ya tatu na ambayo ni ya juu kabisa ni kudhibiti usambazaji wa taarifa. Hapa ndipo ilipo mitandao ya kijamii na vyombo vikubwa vya habari. Hawa ndiyo wanaoamua taarifa imfikie nani na hivyo kuwa na nguvu zaidi kwenye hizo ngazi.

Wewe kama muuzaji, epuka ngazi ya chini ya ulaji wa taarifa na anzia kwenye ngazi ya kuzalisha taarifa na kwenda ngazi ya juu ya kudhibiti usambazaji wa taarifa. Kadiri unavyokuwa na udhibiti mkubwa zaidi, kwenye kuzalisha na kusambaza taarifa, ndivyo pia unavyokuwa na ushawishi mkubwa zaidi.

SOMA; USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kufundisha Kitu Ambacho Hujasomea.

AINA ZA MAUDHUI.

Nafasi yako kama muuzaji kwenye kuzalisha taarifa ni kuwa mtu wa kuzalisha maudhui. Maudhui ni taarifa na maarifa ambayo yanakuwa na manufaa fulani kwa wale wanaoyapokea. Maudhui ndiyo nguzo kuu ya zama hizi za taarifa na wale wanaozalisha na kusambaza maudhui wanakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.

Katika kuzalisha kwako maudhui kama mtu wa mauzo, unapaswa kujua aina tatu za maudhui na uweze kuzalisha kwenye aina zote ili uwafikie wengi na kuwa na ushawishi.

Aina ya kwanza ni maudhui ya kuelimisha.

Maudhui ya kuelimisha ni yale ambayo yanawafundisha watu kitu ambacho hawakuwa wanakijua au kukielewa vizuri. Wewe kuna mambo mengi unayoyajua kuhusu biashara unayofanya na ambayo wateja hawayajui au kuyaelewa vizuri kama wewe.

Kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wateja unaowalenga kuhusu vitu unavyouza, kwa njia hiyo utaongeza zaidi thamani kwao, utaaminika zaidi na kuweza kuwashawishi wanunue kwako. Kwa kukuamini kupitia kujifunza, inakuwa rahisi kwao kukuamini na kununua.

Aina ya pili ni maudhui ya kufurahisha.

Maudhui ya kufurahisha ni yale yanayowafanya watu wacheke na kufurahi. Maudhui haya yanahusu vichekesho mbalimbali vinavyoendana na biashara unayofanya. Kuwa na vichekesho vya aina hiyo na kuwashirikisha wateja unaowalenga. Huwa kuna kauli kwamba wakicheka wananunua, hivyo kadiri unavyoweza kuwachekesha wateja wako zaidi, ndivyo unavyoweza kuwauzia zaidi.

Tahadhari kwenye vichekesho ni kuhakikisha huwadhihaki au kuwanyanyapaa wengine kwa vichekesho unavyotoa. Pia usisambaze vichekesho ambavyo vimeshazoeleka sana. Kuwa mbunifu kwa kuja na vichekesho vyako mwenyewe na vinavyoendana na aina ya biashara unayofanya.

Aina ya tatu ni maudhui ya kuhamasisha.

Watu wanapenda kuhamasika, hasa kwa kupitia hadithi mbalimbali. Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanajiweka kama sehemu ya hadithi za mafanikio na kupitia hadithi hizo wanaona nao wanaweza. Kuwa na hadithi mbalimbali za mafanikio, kuanzia kwako binafsi na kwa wateja wako jinsi ambavyo wameweza kunufaika na kile unachouza na hilo litawahamasisha wengine na kuwavutia kununua.

Kuwa mtu wa hamasa kwa kushirikisha hadithi na taarifa zinazowahamasisha wengine na kuwafanya waone wanaweza kufanya makubwa zaidi. Watu wanapenda matumaini ya aina hiyo na unapokuwa chanzo cha matumaini hayo, wanavutiwa kuja kwako. Muhimu ni uepuke kutumia hadithi za jumla za hamasa ambazo haziendani na biashara unayofanya.

Kwa kila maudhui unayoyatoa, yanapaswa kuendana na aina ya biashara unayofanya na kuwafanya wateja wakuamini zaidi na kuamini kile unachouza. Usikusanye tu maudhui kutoka kwa wengine na kuyasambaza. Yachakate yaendane na biashara yako na yawafae wateja unaowalenga ili yaweze kuwa na ushawishi.

NJIA ZA KUSAMBAZA MAUDHUI.

Njia zote ambazo tumejifunza za kuwafikia wateja, zinaweza kutumika kusambaza maudhui ili yawafikie wengi zaidi.

Ana kwa ana inaweza kutumika, kwa mtu mmoja mmoja au watu wengi kwa pamoja kama pale unapopata nafasi ya kunena mbele ya wengine.

Mazungumzo ya simu na jumbe fupi za simu zinaweza kutumika kwenye kusambaza maudhui kwa wengi zaidi.

Na njia yenye nguvu zaidi ni mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Hii ina nguvu ya kuwafikia watu wengi kwa pamoja, lakini pia inakuwa rahisi kwa watu kusambaziana maudhui ambayo wamependezwa nayo. Hilo linakupa nguvu ya kuweza kuwafikia wengi zaidi.

Andaa maudhui yako ya yasambaze kwa kila njia unayoweza kuitumia, kwa sababu lengo lako ni kuwafikia watu wengi zaidi ili kuwashawishi na kuweza kuuza zaidi.

WANAONA HATA KAMA HAWAJIBU.

Changamoto kubwa ya kutumia maudhui kuwafikia wengi ni uvumilivu mkubwa sana unahitajika. Matokeo ya maudhui huwa siyo ya hapo kwa hapo, kwamba umeshirikisha maudhui na watu wakaanza kununua ka wingi. Unahitaji kutoa maudhui kwa muda mrefu ili kujenga kuaminika na hatimaye kuweza kuuza zaidi.

Hivyo unaweza kujikuta unatoa na kusambaza maudhui, lakini hakuna mrejesho wowote unaokuwa unaupata. Ni rahisi kuona maudhui yako hayakubaliki na ukaacha. Lakini usifanye hivyo, hata kama hawajibu au kukupa mrejesho wowote, wewe endelea kutoa maudhui, usiache. Kitu kimoja unachoweza kuwa na uhakika nacho ni kwamba watu wanayaona maudhui yako. Na ukitaka kujua ukweli wa hilo, toa maudhui kwa muda halafu acha ghafla, kuna baadhi ya watu watakuambia; siku hizi zioni tena jumbe zako.

Jiwekee ratiba yako nzuri ya kuzalisha na kusambaza maudhui ili uendelee kuwafikia wengi na kuwashawishi. Usiumize kichwa sana unawezaje kupata maudhui, kwenye hiyo hiyo biashara unayofanya, kuna maudhui mengi sana ya kuelimisha, kufurahisha na kuhamasisha. Kuwa mdadisi na mbunifu ili uweze kuibua maudhui na kuyasambaza kwa wengi zaidi.

Jifunze pia njia nzuri ya uwasilishaji wa maudhui yako kwa maandishi, sauti na video ili kuwa na ushawishi kwa wengi na kuwafanya wawe tayari kusambaza maudhui yako yawafikie wengi zaidi. Kwa zana tulizonazo sasa, kama simu janja (smartphone), unaweza kuzalisha aina yoyote ya maudhui unayoyataka kwa mfumo wowote na ukawafikia watu wengi. Kwa wanaopenda kusoma utawaandalia maandishi, wanaopenda kusikiliza unawaandalia sauti na wanaopenda kuangalia unawaandalia picha na video.

Kwa zama tunazoishi sasa, kila mtu ni mzalishaji wa maudhui na kila mtu ni chombo cha habari. Wale wanaolielewa hilo mapema na kulifanyia kazi ndiyo wanaopata manufaa makubwa. Weka juhudi kubwa kwenye kuzalisha na kusambaza maudhui, utaweza kuwafikia wengi zaidi, utaaminika zaidi na kuweza kuwashawishi watu wakubali kununua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.