Rafiki yangu mpendwa,

Huwa ni hitaji letu kama binadamu kutaka kukubalika na watu wengi zaidi. Hivyo kwa chochote tunachokuwa tunafanya, tunakazana kuhakikisha kila mtu anakubaliana na sisi. Pale inapotokea baadhi ya watu hawakubali au kuridhika, tunaona kama tumeshindwa kabisa.

Rafiki, hivyo sivyo mafanikio yalivyo. Kwenye mafanikio, njia ya uhakika ya kushindwa ni kujaribu kumridhisha kila mtu. Hiyo ni kwa sababu kadiri unavyokazana kuwaridhisha wengi, ndivyo unavyoishia kutokumridhisha yeyote.

Mahitaji ya watu huwa hayafanani, kile ambacho watu fulani wanakikubali, watu wengine wanaweza kukikataa kabisa. Kile ambacho kinapendwa na watu wa aina fulani, kinakuwa kinachukiwa na aina nyingine ya watu. Hivyo kama unafikiria kuja na kitu ambacho kitapendwa na watu wote kwa usawa, unajikwamisha wewe mwenyewe.

Kwa chochote ambacho umechagua kufanya na kukitumia kama njia yako ya kujenga mafanikio makubwa, chagua aina ya watu ambao ndiyo utakuwa unawalenga. Hao ndiyo utawawekea juhudi zako zote kuwapa thamani kubwa, kwa kuwa wanakuwa na uhitaji wa kile unachotoa.

Pale unapochagua kuwalenga watu wa aina fulani, watakuja watu wa aina nyingine na kukuambia kama ungefanya tofauti kidogo basi na wao ungewapata. Kwa kutaka kuwaridhisha wengi zaidi, unaweza kushawishika kufanya hivyo. Watakuja tena wengine, na wengine na wengine, unapokuja kushtuka unakuta una kitu ambacho hata wewe hukielewi, hakuna kinayemlenga wala kumridhisha.

Njia ya kuepuka hilo ni kuchagua wale ambao utawahudumia vizuri, kisha kuwakataa wengine wote. Pale wanapokuja wale ambao hujawalenga na kuanza kukueleza nini ufanye ili nao wanufaike, unawajibu moja kwa moja kwamba kile unachofanya wewe siyo kwa ajili yako.

SOMA; BIASHARA LEO; Fukuza Wateja Hawa…

Kwa kuwakataa watu kwa namna hiyo unaweza kuonekana kama unajinyima fursa ya kupata mafanikio makubwa, lakini ukweli ni matokeo utakayoyapata ni makubwa zaidi kwa kutoa thamani kubwa kwa aina fulani ya watu kuliko kutoa thamani ndogo kwa aina zote za watu.

Hili halimaanishi kwamba utawahudumia watu wachache pekee, bali utawahudumia watu wengi, ambao wana zile sifa ambazo umezichagua. Walio nje ya sifa hizo utawaambia kwamba ulichonacho siyo kwa ajili yao.

Unaweza hata kuchukiwa na baadhi ya watu ambao waliona wangeweza kunufaika na unachotoa ila unawanyima, lakini unachotaka wewe ni kupendwa na wale ambao umechagua kuwahudumia. Kwenye maisha, ili upendwe na aina fulani ya watu, lazima pia ukubali kuchukiwa na aina nyingine ya watu. Kwa kiwango kile kile unachopendwa na wale uliojitoa kwa ajili yako, ndivyo pia utakavyochukiwa na wale ambao unawakataa. Hivyo hilo lisikuumize wala kukukwamisha.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeeleza kwa kina jinsi ya kuwakataa wale ambao hujawalenga ili uweze kuwapa thamani kubwa zaidi wale uliowachagua. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho ili uweze kutoa thamani kubwa na kujijengea mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.