3375; Raha sahihi kwako.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mambo yote ambayo tunayafanya, msukumo mkubwa kwetu huwa ni kupata raha.
Tunafanya mambo kwa sababu yanatupa raha kufanya au tunategemea matokeo tunayoyapata yatupe raha.
Hata kwa mambo yanayoonekana ni ya kijinga kabisa ambayo watu wanayafanya, bado msukumo ni huo huo.
Tatizo kubwa la raha huwa ina uraibu,
Raha yoyote tunayoipata, huwa inadumu kwa muda mfupi sana na baadaye kuisha.
Hivyo ili mtu apate tena raha, inamlazimika arudie tena kufanya kile alichofanya kikampa raha.
Hivyo ndivyo uraibu unavyotengenezwa, kwa watu kurudia rudia kufanya yanayowapa raha.
Kwenye maisha, raha rahisi na inayopendwa na walio wengi ni kulaumu na kulalamika.
Kwa yoyote ambayo mtu anakuwa anapitia, huwa analaumu watu na kulalamika kuhusu wengine.
Mtu anapofanya hivyo, anapata raha ya muda mfupi kwamba siyo yeye amesababisha kuwa pale alipo.
Lakini kama ambavyo tumeshaona, raha hudumu kwa muda mfupi.
Hivyo ndivyo mtu anavyoishia kuwa unarudia rudia kulalamika, hata kwa mambo rahisi, na hivyo kujikwamisha kufanya makubwa.
Na hata uraibu na ulevi mwingine, unajenywa hivyo hivyo, kwa mtu kurudia rudia kufanya ili kupata raha.
Kwa kuwa bado binadamu tunaendelea na kusukumwa kufanya mambo kwa kutafuta raha, tunaweza kutumia hilo vizuri.
Tunachopaswa kufanya ni kuweka maana ya raha kwenye mambo ambayo ni sahihi na yaliyo ndani ya uwezo wetu kuyatekeleza.
Yaani raha tusiiweke tena kwenye matokeo tunayopata, bali kwenye juhudi tunazoweka.
Na juhudi hizo ziwe ambazo haziwezi kukwamishwa na kitu chochote cha nje.
Badala ya kuweka raha yako kwenye kulalamika na kulaumu au kwenye starehe za muda mfupi, unapaswa kuweka raha hizo kwenye vitu sahihi.
Na moja ya vitu sahihi kuvifanya kuwa chanzo cha raha sahihi kwako ni kazi.
Pata raha kwenye juhudi za kazi unazoweka bila ya kujali ni matokeo gani unayopata.
Kwa sababu raha yako ipo kwenye juhudi unazoweka, utaendelea kurudia kuweka juhudi hizo ili kupata raha zaidi.
Kwenye kurudia rudia kuweka juhudi hizo za kazi, unaishia kuzalisha matokeo makubwa na mazuri.
Unapogeuza juhudi za kazi kuwa ndiyo chanzo cha raha, maisha yako yanabadilika sana.
Siyo tu kufanya kunakupa raha, bali pia unakuwa umejisogeza karibu zaidi na matokeo unayoyataka.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, rafiki yetu namba moja ni kazi. Kazi ndiyo kipaumbele cha kwanza kwetu ambacho haturuhusu kingine kukiingilia.
Tunapenda na kufurahia kuweka juhudi kubwa kwenye mambo yote tunayofanya.
Tunahangaika na upande wa juhudi kwa sababu huo ndiyo tuna udhibiti nao.
Upande wa matokeo hautusumbui kwa sababu hatuna udhibiti nao. Lakini tunajua kwa kuendelea kuweka juhudi, tunasogea karibu zaidi na matokeo tunayoyataka.
Wakati watu wengine wanahangaika na kutafuta raha kwenye starehe mbalimbali, sisi starehe yetu ya kwanza ni kazi.
Hivyo hatusiti wala kuchoka kuweka juhudi kwa muda mrefu zaidi ya wengine.
Kazi inakuwa ndiyo kitu ambacho mara zote tunakuwa tayari kuendelea kukifanya, badala ya kukimbilia kwenye mapumziko na starehe nyingine.
Kazi inakuwa ndiyo starehe pekee kwetu na tunasukumwa kufanya muda wote, tena kwa kuboresha zaidi.
Kwa kazi kuwa ndiyo chanzo chetu cha raha, mafanikio yanakuwa uhakika kwetu. Hata kama yataonekana kuchelewa, tunajua ni swala la muda tu.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Kwa kazi kuwa ndiyo chanzo chetu cha raha mafanikio yanakuwa UHAKIKA kwetu.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike