Kwenye maisha pamoja na mambo mengi tunayofanya, huwa tunahitaji kusikia maneno ya faraja au maneno ya kututia hamasa. Bila kujali aina ya huduma tunayopata.

Kiasili sisi binadamu kwa asimilia kubwa ni viumbe wa hisia, tu wepesi wa kusahau mambo mengi tuliyotendewa. Kitu kimoja ambacho hatuwezi kusahau ni namna mtu anavyofanya tujisikie vizuri.

Mahali popote tunapokuwa bila kujali gharama, tupo tayari kuingia mfukoni na kutoa pesa kupata huduma ya mtu huyo. Hii ni kwa sababu tumechoka kuumizwa sehemu nyingi na kukosa uponyaji. Moja ya vitu vinavyofanya tujisikie vizuri ni pale tunapoambiwa maneno mazuri wakati tunahudumiwa.

Je, ni maneno yapi hayo, mtu akitwambia tunajisikia vizuri? Usiwe na wasiwasi makala hii, imeandaliwa kwa ajili yako. Karibu tujifunze maneno haya na kuyatumia kwa wateja wetu mara zote;

Moja;  Habari
Hili ni neno linalofungua mazungumzo. Badala ya kumwambia, mwana! Oi oi! Nikupe nini? Unaanza na neno, habari Mr/miss Elizabeth. Mimi ni Robert, natokea Amka Consultants. Hapo mteja ni rahisi kukupa nafasi ya kukusikiliza. Kisha unaendelea na mazungumzo kadiri ya mahitaji yake.

Mbili; Karibu.
Inasikitisha sana, unaingia katika biashara au sehemu mhusika anakutazama tu kama picha bila kukukaribisha. Kisha anasema, unataka nini au nikuhudumie nini? Hayo ni mazoea na siyo jambo zuri kufanya mbele ya mteja. Mwambie, karibu nikuhudumie.
Au unayaunganisha, habari Anna, karibu tukuhudumie. Mteja anaona unamthamini.

Tatu; Tafadhali.
Badala ya kumwambia, “Oya, Wewe, au sema”. Unatumia neno, tafadhali, ningependa tu kujua….
Tafadhali, naomba urudie hapa. Inaonyesha heshima na unamjali mteja unayeongea naye.

Nne;  Àsante.
Ni neno dogo sana, lakini manufaa yake ni makubwa . Unamfanya mtu aone thamani ya kutumia huduma yako. Unaweza kulitumia mwanzoni, katikati au mwishoni mwa mazungumzo na mteja. Kwa lugha rahisi, unapotumia neno àsante, maana yake unaomba mtu arudi tena.

Tano; Samahani.
Hii unaitumia kuomba msamaha au pale unapotaka kumpendekezea kitu kwa mteja. Hii itumike ikiwa umesahau neno hili; “sina uhakika kama itakufaa, lakini”. Japo hatushauri neno samahani litumike mara nyingi. Kwenye biashara, muuzaji unapaswa kuthibiti mazungumzo. Neno samahani linapunguza uthibiti. Litumike kidogo sana, ikiwezekana mara moja tu.

Sita; Naomba.
Hii inaonyesha utulivu, ukaribisho kidogo tofauti na  neno nipe kitu au nionyeshe hii. Mara zote unapotaka kitu kutoka kwa mteja, Omba. Maandishi ya mengi yameweka wazi, kwamba aombaye hupewa. Pale unapotaka namba ya simu au mteja wa rufaa, tumia neno hili.

Wakati wa kutamka maneno haya, ukiongezea na tabasamu ndo unamtamanisha mteja sana na kumshawishika kununua bidhaa au huduma yako.

Haya maneno yatumie mara zote ukiwa unaongea naye. Mfanye atamani kuona simu yako, afike katika eneo lako au ufike katika biashara yake.

Muhimu; Siyo lazima yatumike kwa mpangilio au yote moja kwa moja. Unayatumia kadiri na nafasi. Usijifungie katika neno moja.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.