Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye somo la leo nataka twende kwa namba ili tuweze kuelewana vizuri na ukachukue hatua sahihi.
Pata picha unaendesha biashara, ambayo kwa mwezi unafanya mauzo ya milioni 100 na kwa wateja 100. Unawapitia wateja hao mmoja mmoja na kugundua wateja 20 wamesababisha mauzo ya milioni 80, wakati wateja 80 waliobaki wamechangia mauzo ya milioni 20 tu.

Je kama unataka kukuza mauzo yako zaidi, bila ya kuongeza kazi unayofanya sasa, nini unapaswa kufanya? Jibu utakuwa nalo, kuongeza nguvu kwa wateja wachache (20) ambao wameleta mauzo makubwa (milioni 80).
Rafiki, hiyo uliyojifunza hapo ni kanuni ya msingi sana kwenye kuongeza matokeo bila ya kuongeza juhudi, ambayo inaitwa kanuni ya Pareto. Kanuni hii inasema sehemu kubwa ya matokeo inachangiwa na sehemu ndogo ya juhudi. Hivyo kama utaweka umakini zaidi kwenye sehemu ndogo ya juhudi, utaweza kuongeza zaidi matokeo yako.
Rafiki, inapokuja kwenye biashara, wateja hawalingani. Kuna wateja wachache ambao wanafanya manunuzi makubwa na wanaithamini biashara. Hawa unakuwa unafurahia sana kufanya nao biashara. Halafu kuna wateja wengi ambao wanaleta mauzo kidogo na pia hawaithamini biashara. Mara zote huwa ni wateja wa kulalamika na kutaka zaidi hivyo gharama za kuwahudumia zinakuwa kubwa kuliko faida wanayochangia.
Kila biashara inayo fursa ya kukuza zaidi mauzo yake bila ya kuhitajika kuongeza rasilimali zozote zile. Inapaswa kuanza kwa kuangalia yale ambayo tayari yanafanyika, kisha kuweka nguvu kwenye machache ambayo yanaleta matokeo makubwa.
SOMA; 3176; Kuza mauzo kwa macho na masikio.
Fanya zoezi hili kwenye biashara yako, pitia wateja wote ambao huwa wananunua mara kwa mara kisha pima mchango wao kwenye manunuzi. Chagua wale ambao wanachangia mauzo makubwa zaidi. Hao wawekee juhudi kubwa zaidi kuhakikisha unawapa thamani kubwa ili waendelee kununua.
Wale wengine ambao hawaleti mauzo makubwa siyo kwamba unawafukuza, bali tu huwakazanii sana kama wale wachache uliowachagua. Kama watakuja kununua wanauziwa, lakini wakileta malalamiko yao ambayo lengo lake ni wao kujinufaisha zaidi, wanapaswa kuelezwa wazi kwamba hawataweza kuendelea kuhudumiwa kama wataendelea na huo utaratibu wao.
Rafiki, kabla hujaondoka hapa ukifurahia kwamba unaenda kupunguza kazi na kuongeza kipato chako naomba nikutahadharishe, ukishawaondoa wateja wengi ambao hawachangii mauzo makubwa, unakuwa umeanza kazi kubwa ya kutengeneza wateja wapya ambao wana sifa za wale wanaochangia mauzo makubwa.
Kamwe usije ukabweteka na wateja wachache wanaofanya manunuzi makubwa na mazuri. Hupaswi kuruhusu mteja mmoja kuwa sehemu kubwa ya mauzo yako, hivyo unawajibika kutengeneza wateja wengi zaidi wazuri ili yeyote akiondoka kusiwe na pengo kubwa. Ni rahisi kubweteka na mauzo makubwa yanayoletwa na wateja wachache, lakini mambo huwa yanabadilika, yanapokuja kubadilika wakati wewe una utegemezi mkubwa kwa hao wachache, utaumia sana.
Jenga biashara yako kwa kuweka nguvu zako kwa wateja wanaoleta mauzo makubwa, lakini hakikisha unao wateja wa aina hiyo wengi. Na hata baada ya kuwa nao wengi, endelea kutafuta wateja wapya kila wakati, wenye sifa zinazoendana na hao wanaofanya vizuri.
Usikubali mteja mmoja kuwa anachangia zaidi ya asilimia 10 ya mauzo kwenye biashara yako. Haimaanishi ukiwa na mteja wa aina hiyo umfukuze, badala yake unapaswa kujenga wengi wa aina hiyo ili mauzo yawe makubwa kutoka kwa wateja wazuri wengi.
Kwa kujenga biashara yako kwenye misingi hiyo utaweza kukuza mauzo na kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumejadili kwa kina kuhusu kuchuja wateja wa biashara yako. Fungua kipindi na uweze kujifunza kutokana na mjadala huu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.