Rafiki yangu mpendwa,
Umekuwa unafuatilia mafunzo mengi ninayoyatoa na unaijua falsafa yangu kuu ya kazi. Kwamba kazi ndiye rafiki wa kweli, rafiki yako namba moja ambaye hawezi kukusaliti. Kazi ndiye rafiki ambaye ukifanikiwa anazidi kukupenda badala ya kukuonea wivu kama ilivyo kwa marafiki wengine.
Vipi kama leo nikikufundisha kwamba unaweza kuongeza sana matokeo unayoyapata, huku ukipunguza zaidi juhudi unazoweka? Yaani unaongeza kile unachopata, huku ukipunguza kile unachoweka. Inaweza kuonekana kama ni miujiza, lakini ni kitu kinachowezekana kwenye uhalisia.
Rafiki, usiwe na hofu, haya yote bado yapo chini ya misingi ya ufanyaji kazi ambayo tumekuwa tunashirikishana. Haimaanishi utapata mafanikio ukiwa umelala, bado utahitaji kuweka juhudi, lakini kwa sasa juhudi zako zitazalisha matokeo makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko awali.
Kwa maana hiyo basi, kama utaamua kuongeza juhudi unazoweka, maana yake matokeo yatakuwa makubwa kuliko unavyoweza kudhania.

Zipo kanuni mbili ambazo ukizijua na kuzifanyia kazi, utaweza kuongeza sana matokeo yako ukilinganisha na juhudi unazoweka. Hapa unakwenda kujifunza kanuni hizo na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi matokeo unayozalisha.
Kanuni ya kwanza ni ya Pareto au 80/20.
Kanuni ya Pareto inasema asilimia 80 ya matokeo inatokana na asilimia 20 ya juhudi zilizowekwa. Kwa maana nyingine ni kuna juhudi kidogo ambazo zinazalisha matokeo makubwa, wakati juhudi kubwa zinazalisha matokeo kidogo.
Hatua ya kuchukua hapa ili kuongeza matokeo huku ukipunguza juhudi ni kuorodhesha juhudi ulizoweka na matokeo uliyopata. Kisha ainisha juhudi chache zilizochangia majukumu makubwa. Hizo tu ndiyo utakazoendelea nazo. Zile juhudi nyingi ambazo zimezalisha matokeo madogo unaachana nazo. Kwa kuacha kuweka juhudi kwenye mengi na kupeleka kwenye machache, utaweza kuongeza matokeo huku ukipunguza juhudi.
SOMA; Njia Bora Ya Kuongeza Ufanisi Wa Wale Unaowaajiri Kwenye Biashara Yako.
Kanuni ya pili ni ya Parkinson.
Kanuni ya Parkinson inasema jukumu huwa linachukua muda ambao limetengewa. Hiyo ina maana kwamba kama una jukumu la kufanya na una masaa 10 ya kulifanya, basi jukumu hilo litachukua masaa 10. Na kama jukumu hilo hilo utapanga kulifanya ndani ya masaa matano, litakamilika kwenye muda huo.
Hatua ya kuchukua hapa ni kupanga kutekeleza majukumu ndani ya muda mfupi ili uweze kuweka umakini wako wote kwenye kuyatekeleza ndani ya muda huo. Kwa ule muda ambao umezoea kufanya jukumu, panga kufanya kwa nusu ya muda huo. Utashangaa jinsi ambavyo utaweza kukamilisha vizuri jukumu hilo ndani ya muda mfupi na kwa matokeo mazuri.
Rafiki, ukitaka matokeo yawe makubwa zaidi, unatumia kanuni zote mbili kwa pamoja. Na hapo unachofanya ni unayapitia majukumu yote na kuchagua machache ambao yanaleta matokeo makubwa. Baada ya kuchagua hayo machache, unapanga kuyakamilisha kwenye nusu ya muda ambao ndiyo huwa unayafanya. Kwa kufanya hayo mawili kwa pamoja, ndiyo unaongeza sana matokeo yako huku ukipunguza juhudi.
Tukienda kwa mfano wa namba ili tuelewane vizuri, kama una majukumu 10 ambayo unayatekeleza kwa masaa 10, unayapitia yote na kupata mawili ambayo yana matokeo makubwa kuliko mengine. Kama hayo mawili kwa kawaida unayafanya kwa masaa mawili, unapanga kuyafanya kwa saa moja. Hapo unakuwa umetoka kwenye majukumu 10 ya kufanya mpaka mawili, na masaa 10 ya kuyafanya mpaka saa 1, huku matokeo yakiwa ni makubwa sana.
Rafiki, huu muujiza unawezekana kabisa kwenye maisha yako, hebu anza kuufanyia kazi mara moja na utaona matokeo makubwa na mazuri utakayoyapata.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeeleza kwa kina zaidi kanuni hizo mbili ili uweze kuzielewa kwa kina na kuzifanyia kazi. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.