Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu maalumu ya kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa hatua ndogo ndogo kwa muda mrefu bila kuacha.
Kanuni kuu ya uwekezaji tunayoifanyia kazi kwenye programu yetu ni WEKEZA NA SAHAU. Kanuni hiyo inatutaka tuwekeze kisha tuendelee na mambo yetu mengine, ili tuuache uwekezaji ukikua na kutuzalishia faida.
Lengo letu ni kuwekeza kwa muda mrefu, kuanzia miaka kumi na kuendelea kwa sababu ndiyo kipindi kizuri cha kuweza kuiona faida ya uwekezaji, yaani ule ukuaji halisi wa uwekezaji ambao umefanyika.

Kwenye somo hili tunakwenda kukumbushana kwa nini kuweka akiba pekee ni kujijengea umasikini.
Kwa miaka mingi, mafunzo ya fedha binafsi yamekuwa yakisisitiza umuhimu wa kuweka akiba kama sehemu ya kujenga utajiri. Kumekuwa na kauli kama akiba haiozi na nyingine ambazo zinahamasisha uwekaji wa akiba.
Lakini kuweka akiba ni moja ya hatua za kujenga utajiri, kuishia hapo huwezi kujenga utajiri ambao unautaka. Ni lazima uende zaidi ya kuweka akiba ndiyo uweze kujenga utajiri unaoutaka.
Ukweli ni kwamba, hakuna mtu ambaye amewahi kujenga utajiri mkubwa kupitia kuweka akiba pekee. Lakini bado kuna watu wanang’ang’ana na kuweka akiba, hasa kwa njia ambazo ni nje ya mifumo ya fedha wakidhani ni salama kufanya hivyo. Matokeo yake ni wanaishia kubaki kwenye umasikini mkubwa.
Kuweka akiba pekee ni kujijengea umasikini kwa sababu zifuatazo;
1. Mfumuko wa bei unapunguza thamani ya fedha unayoweka akiba.
Kila mwaka vitu huwa vinapanda bei, hiyo ina maana kwamba fedha ile ile uliyokuwa nayo mwaka jana, haiwezi kununua kiwango kile kile cha kitu mwaka huu.
Ukichukua mfano wa sukari, kama mwaka jana sukari ilikuwa Tsh 2,500/= ukiwa na elfu 15 ulipata kilo 6 za sukari. Kama mwaka huu sukari imepanda bei na kuwa Tsh 3,000/= ukiwa na elfu 15 unapata kilo 5 za sukari. Hivyo unaweza kuona hapo, fedha ile ile, imekuwa na thamani ndogo zaidi.
Kwa kuweka akiba pekee, fedha inabaki ile ile, wakati thamani yake kiuchumi inapungua. Ndiyo maana kama utaweka akiba pekee, utazidi kubaki kwenye umasikini, kwani kwa muda mrefu thamani inakuwa imeshuka sana. Yaani ni kama unakuwa umeamua kutupa pesa kabisa.
2. Benki inakutoza kukutunzia fedha zako.
Kuna akaunti mbalimbali za benki ambazo huwa zinaonekana kuwa na riba kwa akiba unayoweka. Lakini riba hiyo huwa ni ndogo sana kiasi kwamba benki inakutoza wewe fedha zaidi kwa kukutunzia fedha zako. Kwa kutoa makato ya kila mwezi ya akaunti, tozo za kutoa fedha na makato mengine ya benki, unaishia kuingia gharama kubwa kuweka akiba peke yake.
3. Benki inawapa wengine fedha zako wakazitumie.
Kama kuweka akiba ingekuwa ndiyo utajiri, benki zingefanya kazi ya kutunza fedha za wateja tu. Lakini hiyo siyo biashara kuu ya benki. Biashara kuu ya benki ni kuchukua fedha ambazo watu wanaweka na kuwapa wale wanaoweza kuzitumia kuzalisha na kulipa riba. Benki zinaingiza fedha siyo kwa makato wanayofanya kwenye fedha unazoweka, bali kwa riba wanazokusanya kwenye mikopo wanayotoa.
Hivyo unapoweka akiba pekee ukidhani benki inakutunzia, yenyewe inachukua akiba yako na kuwapa wengine waitumie kuzalisha faida zaidi na kuweza kurudisha fedha hiyo benki pamoja na riba.
4. Ni rahisi kutumia akiba ulizoweka.
Ukiwa umeweka akiba na ukapatwa na shida, hutaumiza sana kichwa chako kwenye kuitatua, badala yake utajikuta unatumia akiba hiyo kutatua shida ulizopata. Wakati mwingine hata kama umeweka ugumu kwenye kutoa akiba hiyo, unapobanwa hasa na shida, unajishawishi na kujikuta umeshatoa akiba na kutumia. Sasa kwa kuwa shida huwa haziishi, akiba nazo huwa hazikai. Na wakati mwingine sida huwa zinaonekana kukuandama pale unapokuwa na akiba. Akiba ikiisha na shida nazo zinaisha! Ni jambo la kushangaza hilo jinsi unavyoweza kujidanganya na kutumia akiba zako mwenyewe.
5. Ni kutegemea nguvu zako mwenyewe kujenga utajiri.
Naandika hili kwa herufi kubwa kwa msisitizo; HAKUNA MTU AMEWAHI KUJENGA UTAJIRI MKUBWA KWA KUTEGEMEA NGUVU ZAKE MWENYEWE. Kwenye kujenga utajiri kuna kitu kinaitwa nyenzo, ambapo unatumia rasilimali za wengine kupata matokeo makubwa.
Unapokuwa unaweka akiba, hapo unatumia fedha zako mwenyewe tu, ni nguvu za mtu mmoja, ambazo haziwezi kuleta madhara makubwa. Kujenga utajiri mkubwa kadiri ya unavyotaka, lazima utumie rasilimali za wengine, utumie nguvu za wengine, muda wa wengine, utaalamu wa wengine na hata fedha za wengine. Hayo yote huwezi kuyafanya kwa kuweka akiba pekee.
Ufanye nini ili kuondoka kwenye mtego wa akiba kukufanya masikini?
Ili kuondoka kwenye huu mtego wa kunasa kwenye umasikini kwa kuamini kwenye kuweka akiba pekee, chukua hatua zifuatazo.
1. Kumbuka akiba ni hatua ya kwanza ya kujenga utajiri.
Akiba ni mwanzo wa safari na safari yenyewe, siyo mwisho wa safari. Kila unapoweka akiba, jikumbushe hiyo ni mbegu tu, manufaa ya mbegu ni pale inapopandwa. Hakuna mkulima anayekaa na mbegu kama amemaliza. Bali anapanda mbegu ili kupata mavuno makubwa. Akiba yako ni mbegu, unapaswa kuitumia kuzalisha zaidi.
2. Kutumia akiba kuongeza kipato ni muhimu.
Hatua muhimu ya kutumia akiba yako ni kwenye kuongeza kipato chako zaidi ya unavyoingiza sasa. Haijalishi kipato unachoingiza sasa, unaweza kuongeza zaidi kipato hicho. Na hilo litawezekana kwa kuanza kuweka akiba kisha sehemu ya akiba hiyo kuiweka kwenye mzunguko ambao unaongeza zaidi kipato chako. Mara zote hakikisha kuna uzalishaji unaofanya ili kuongeza kipato chako zaidi ya kile unachoingiza sasa.
3. Unapaswa kutumia rasilimali za wengine (nyenzo).
Kila mara jikumbushe unahitaji kutumia rasilimali za wengine kwenye kujenga utajiri mkubwa kwako. Muda wako pekee haukutoshi, unapaswa kutumia muda wa wengine pia. Ujuzi wako pekee haukutoshi, tumia na wa wengine. Na hata fedha zako pekee hazikutoshi, tumia fedha za wengine pia. Akiba ni hatua ya kwanza kukuwezesha wewe kutumia rasilimali za wengine kuzalisha zaidi.
4. Uwekezaji ni hatua muhimu zaidi kwenye kujenga utajiri kwa muda mrefu.
Hatua ya juu kabisa ya kutumia akiba yako kukujengea utajiri, ambayo inaondoa changamoto ya thamani ya fedha kushuka ni uwekezaji. unapowekeza fedha, inakuwa inaongezeka thamani kadiri muda unavyokwenda, hivyo hupotezi kama ambavyo ingetokea kwa kuweka akiba pekee. Weka akiba ili kuwekeza na unapowekeza kwa muda mrefu unapata faida kubwa pia.
5. Kuwa na akiba ya dharura pekee.
Kitu kimoja unachoweza kukiona kwenye hili eneo la akiba ni kwamba fedha ikitulia mahali pamoja, inashuka thamani. Fedha inaongezeka thamani pale inapokuwa kwenye mzunguko. Hivyo una wajibu mkubwa wa kuhakikisha fedha yako karibu yote inakuwa kwenye mzunguko. Kuanzia mzunguko wa shughuli zako za kuongeza kipato na mzunguko wa uwekezaji.
Akiba pekee unayopaswa kubaki nayo inapaswa kuwa ya dharura. Ile akiba unayoweka kwa ajili ya kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza. Na tena uandike kabisa ni dharura gani zinastahili wewe kutumia fedha hizo. Unapoingiza kipato, kwanza weka pembeni kiasi kinachokidhi bajeti yako na hiyo akiba ya dharura, kisha kiasi kingine rudisha kwenye mzunguko wa uzalishaji na uwekezaji. Kwa njia hiyo utaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako kama utajipa muda wa kutosha.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili kushirikisha yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Elezea kwa nini kuweka akiba pekee ni kujijengea umasikini na jinsi gani ya kuvuka hilo.
2. Ni njia zipi unazotumia kuweka fedha zako kwenye mzunguko ili kukuza thamani na kujenga utajiri?
3. Ni rasilimali gani za wengine unazotumia kutengeneza utajiri mkubwa kwako?
4. Karibu uulize swali lolote kuhusu somo hili au programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama ushahidi wa kusoma na kulielewa somo hili ili kwenda kulifanyia kazi na kuwa mwekezaji bora huku ukidumu kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.