Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye mauzo, kama una bidhaa au huduma ambayo mteja ana uhitaji nayo na unauza kwa bei ambayo anaweza kumudu kulipia, kama mteja hatanunua, sababu ni wewe.
Wewe mwenyewe ndiye unayekuwa umemzuia mteja kununua kutokana na mambo unayokuwa umefanya au kushindwa kufanya wakati wa mchakato mzima wa mauzo.
Moja ya vitu ambavyo vinawazuia wateja kununua licha ya kuwa na uhitaji na kumudu ni kukosa imani na muuzaji. Hakuna mtu anakuwa tayari kutoa fedha zake kama hana uhakika wa kupata kile anachotaka.

Hivyo unakuwa wajibu wako kama muuzaji kuhakikisha unajenga imani kwa kila mteja unayejihusisha naye, hata kama ni kwa mara ya kwanza unakutana naye. Usiseme mteja ndiyo mmejuana tu kwa mara ya kwanza hivyo hawezi kukuamini. Kwa jinsi unavyofanya naye mazungumzo, una fursa nyingi za kujenga imani kwa mteja. Baadhi ya njia unazoweza kutumia ni kujua na kutumia jina lake, kuijua biashara yako kwa kina na kuwa na majibu kwa mapingamizi anayokuwa nayo. Kutumia ushuhuda wa wale walionufaika na kutoa uhakika kwenye kile anachonunua ni njia zenye nguvu pia.
Kitu kingine kikubwa kinachokwamisha wateja kununua ni kukosekana kwa msisitizo wa kutosha wakati wa kukamilisha mauzo. Wateja wengi huwa hawana maamuzi, hivyo wanakuwa wanamtegemea muuzaji ndiyo awafanyie maamuzi. Lakini hawatamwambia muuzaji wanataka kufanyiwa maamuzi. Badala yake watajaribu kuchelewesha maamuzi yao ya kununua, kwa kutumia kauli kama nitakutafuta nikiwa tayari. Kama muuzaji atakubaliana na mteja kwenye hilo, anakuwa ndiyo amempoteza. Mara nyingi kwenye hali kama hizo mteja anakuwa anataka kupewa msisitizo wa kufanya maamuzi badala ya kuendelea kusubiri. Na hapo njia za kuonyesha ukomo na uhaba huwa zina nguvu ya kuwasukuma wateja kuchukua hatua.
SOMA; Mauzo Ya Ziada Na Namma Yanavyokuza Biashara Yako
Huwa kuna fursa kubwa sana ya kuendelea kumuuzia mteja baada ya kuwa amefanya manunuzi, yaani kufanya mauzo ya ziada. Pale mtu anapokuwa amenunua kitu kimoja, inakuwa rahisi zaidi kumshawishi anunue kitu kingine. Kisaikolojia, mtu anapofanya manunuzi, akishawishiwa kununua kitu kingine hapo hapo anakubali ili kujiambia kwamba manunuzi aliyofanya awali yalikuwa sahihi. Wauzaji wengi wamekuwa wanakosa mauzo haya ya ziada kwa sababu hawachukui hata hatua ya kuwaambia wateja wafanye manunuzi ya ziada. Kwa kila mteja unayemuuzia, unapaswa kuchagua kitu cha ziada ambacho utamshawishi akinunue pia. Siyo wote watakaokubali kununua, lakini ukiwaambia watu 10, hata akikubali mmoja ni mauzo ya ziada ambayo hukuwa nayo.
Kama ambavyo umeona hapa, kuna fursa nyingi za kuuza zaidi ambazo wauzaji tunakuwa tunashindwa kuzitumia kwa sababu ya kutokujua. Baada ya kujua hapa, usirudie tena makosa ambayo umekuwa unafanya huko nyuma na yamekugharimu sana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimejadili kwa kina kuhusu kuacha fedha nyingi wakati wa mauzo. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho na kuchukua hatua ili uweze kukuza mauzo yako kwa kiasi kikubwa, bila hata ya kuhangaika na wateja wengi. Kwa wateja hao hao ulionao sasa, bado unaweza kuongeza zaidi mauzo yako. Fungua kipindi hapo chini ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.