3381; Kipimo sahihi kilipo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Maisha ni darasa ambalo lina mitihani na masomo mbalimbali.
Mafanikio yanatokana na uwezo wa mtu kukabiliana kwa usahihi na mitihani anayokutana nayo.
Watu wengi hudhani mitihani ya maisha, ipo kwenye kupata mafanikio ambayo wanayataka. Yaani ile kuhitajika kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo ya tofauti.
Lakini kipimo sahihi hakipo kwenye huo mchakato wa kupata mafanikio, bali kipimo halisi kipo kwenye kukabiliana na hisia ambazo mtu unakuwa nazo wakati wa mchakato.
Kama tunavyojua, sisi binadamu ni viumbe wa kihisia ambapo tunasukumwa kufanya maamuzi kwa hisia na kuyahalalisha kwa fikra.
Hivyo kuweza kudhibiti nini unafanya au hufanyi, kunaanzia kwenye kudhibiti hisia zako.
Kuna aina nyingi za hisia za kudhibiti ili kuweza kubaki kwenye mchakato sahihi bila kuyumba.
Hisia za hofu pale unapokuwa bado hujapata unachotana ni za kuvuka ili uendelee na safari.
Hisia za wasiwasi wakati wa mchakato ni za kudhibiti ili kupata utulivu kwenye safari.
Hisia za tamaa pale unapokuwa umeshapata matokeo mazuri ni za kudhibiti ili kuacha kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwako.
Hisia za kukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu ni za kudhibiti ili uweze kuendelea na mchakato bila ya kujali ni matokeo gani unapata.
Uwezo wako wa kukabiliana na hisia ndipo mtihani mkubwa ulipo. Jijenge kuwa imara na kuweza kudhibiti hisia zako ili uweze kufanya makubwa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunaongozwa na kanuni na mchakato na siyo hisia.
Tunajua hisia ni sehemu yetu na tunazitumia kufanya maamuzi mbalimbali. Lakini ushindi wetu tunajua upo kwenye kuzidhibiti hisia zetu na kuuguata mchakato kwa usahihi.
Tunahakikisha tunatekeleza mchakato wetu bila ya kuathiriwa na hisia mbalimbali tunazokuwa nazo.
Huo ni mtihani ambao tukifanikiwa kuuvuka, mafanikio makubwa yanakuwa yetu kwa uhakika kabisa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe