Rafiki yangu mpendwa,

Mwandishi Stephen Covey kwenye kitabu chake kinachoitwa The 7 Habits Of Highly Effective People ametufundisha misingi sahihi tunayopaswa kuijenga ili kuweza kuwa na mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yetu.

Kwenye tabia saba ambazo anatutaka tuzijenge, tabia tatu za kwanza anaziita ni tabia za USHINDI BINAFSI (PRIVATE VICTORY). Huu ni ushindi ambao unapaswa kutangulia kabla ya ushindi mwingine wowote. Wale wanaoanza na ushindi binafsi ndiyo wanakuwa na msingi imara wa kujenga mafanikio makubwa.

Katika kupata ushindi binafsi, kuna tabia tatu za msingi ambazo tunapaswa kujijengea. Hapa tunakwenda kujifunza tabia mbili kati ya hizo tatu na jinsi ya kujijengea ili tupate ushindi binafsi na kuweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

TABIA YA KWANZA: UWAJIBIKAJI (KUCHUKUA HATUA); MSINGI WA MAONO BINAFSI.

Tabia ya kwanza tunayopaswa kujijengea ili kupata ushindi binafsi na kujenga mafanikio makubwa ni kuwajibika na maisha yetu wenyewe. Tabia hii inahusu kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yako kuwa vile unavyotaka wewe.

Tofauti yetu sisi binadamu na wanyama wengine ambao wana viungo kama vyetu ni utashi tulionao. Utashi wetu unatuwezesha kufikiri na kufanya maamuzi. Wakati wanyama wengine wanaendeshwa kwa mihemko, sisi binadamu tunaweza kujiendesha kwa fikra.

Fikra zetu zina nguvu ya kuumba kitu chochote tunachokitaka. Fikra zetu ndiyo zinatupa uhuru wa kuchagua nini tunachotaka na jinsi ya kukipata. Kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa wanakubali kuendesha maisha yao kwa mazoea na kuiga wengine, badala ya kutumia uwezo wao wa kifikra kujenga maisha wanayoyataka.

Tabia hii ya kwanza ni ya msingi wa maono binafsi, ikimaanisha mtu kujenga maono ya maisha yako, ambayo yanaendana na vile ulivyo wewe na siyo kuiga wengine au kwenda na mazoea ambayo umeshajijengea.

Uko hapo ulipo sasa kwa sababu ya vichocheo mbalimbali ambavyo umekutana navyo kwa kipindi chote cha maisha yako. Vichocheo hivyo vilianzia kwenye urithi, malezi na mazingira. Lakini pamoja na yote hayo, bado unayo nguvu kubwa ndani yako ya kubadilika na kuwa vile unavyotaka wewe.

Sisi binadamu tunao uwezo mkubwa wa kubadili maisha yetu kwa vile tunavyotaka kwa sababu tuna nguvu nne zilizo ndani yetu. Nguvu hizo ni kama ifuatavyo;

Moja ni kujitambua (self awareness), tuna uwezo wa kujiangalia sisi wenyewe kama tunavyowaangalia wengine na hivyo kuweza kuona namna gani tunaweza kuwa bora zaidi.

Mbili ni kujenga taswira (imagination), tuna uwezo wa kujenga taswira ya kitu chochote kwenye fikra zetu na kukileta kwenye uhalisia.

Tatu ni dhamira (conscience), tunajua mazuri na mabaya na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi.

Nne ni utashi huru (independent will), tuna uwezo wa kuamua sisi wenyewe nini tunataka na nini hatutaki, hata kama tumetawaliwa na wengine, bado utashi huru unakua chini yetu.

Ili kuyabadili maisha yako, kupata ushindi binafsi na kujenga mafanikio, unapaswa kutumia nguvu hizo nne kwenye aina ya maisha unayoyataka. Katika mambo mengi yanayokuzunguka, kuna ambayo unaweza kuyaathiri na ambayo huwezi kuyaathiri. Wajibu wako ni kupeleka umakini wako wote kwenye yale unayoweza kuyaathiri na hivyo ndivyo utajenga mafanikio makubwa.

SOMA; Jinsi Ya Kujenga Maisha Yenye Manufaa Kwako Na Wengine Kutoka Kitabu The 7 Habits Of Highly Effective People.

TABIA YA PILI: ANZA KUFIKIRIA MWISHO; MSINGI WA UONGOZI BINAFSI.

Kwenye tabia hii ya pili, mwandishi Stephen Covey anaanza kwa kutupa mfano ambao una nguvu ya kutufikirisha sana. Anasema; pata picha umehudhuria kwenye msiba ambao watu wote unaowajua wamehudhuria. Unatoka kwenda kumwaga marehemu kwa kumwangalia kwa mara ya mwisho. Unapofika kwenye jeneza, unakuta marehemu ni wewe mwenyewe. Unaporudi kuketi, wanasimama watu wanne kutoa wasifu wa marehemu; 1. Kutoka kwenye familia. 2. Kutoka kwenye marafiki. 3. Kutoka kwenye kazi na biashara. 4. Kutoka kwenye jamii yako. Je ungependa kila mmoja kwenye hayo makundi ayaelezeeje maisha yako yalivyokuwa hapa duniani?

Huo ndiyo mwisho unaopaswa kuanza kuufikiria sasa. Mwandishi anatuambia tunapaswa kuanza kwa kuandika historia ya marehemu ambayo tunataka isomwe siku ya mazishi yetu kwa kuangalia maeneo hayo manne muhimu kwenye maisha yetu. Baada ya kuandika historia hiyo, maisha yetu yote tunapaswa kuyaishi kwa kufuata hiyo historia tuliyoandika.

Hii ni tabia muhimu sana kujijengea kwa sababu ndiyo imebeba maana nzima ya maisha na mafanikio kwako. Kwenye haya maisha, unaweza kupotea kwenye safari yako ya mafanikio, ukaishia kukimbizana na mambo ambayo mwisho hutayafurahia. Wengi wamehangaika na mafanikio ambayo hata baada ya kuyapata hawakuyafurahia. Au wanapata mafanikio lakini wanaharibu afya zao au mahusiano yao.

Kwa kuanza na historia yako ya marehemu, na kuitumia kama mwongozo kwenye maisha yako inakuzuia usipotelee kwenye safari ya mafanikio yenye changamoto nyingi. Historia yako ya marehemu ndiyo itakuongoza vitu gani ufanye na vipi usifanye ili kujenga mafanikio yenye maana kwako.

Tabia hii ya pili inaitwa msingi wa uongozi binafsi, kwa sababu ndiyo inayokuongoza nini unapaswa kufanya na nini usifanye. Kuchukua hatua siyo tatizo kwa watu wengi, tatizo lipo kwenye kuchukua hatua kwenye eneo sahihi. Bila ya uongozi sahihi, juhudi nyingi huwa zinapotea. Ni sawa na kwenda mbio wakati haupo kwenye njia sahihi, kinachotokea ni kuzidi kupotea.

Mafanikio ya kweli kwenye maisha yanaanzia kwenye kujiongoza wewe mwenyewe, kubobea kwako binafsi na kuweza kujitawala na kujidhibiti.

Uongozi binafsi unakutaka kuwa na falsafa binafsi, ambayo ndiyo inakuongoza kwenye mambo yote unayoyafanya. Falsafa yako binafsi inaeleza maono ya maisha yako na misingi ambayo unaisimamia kwenye maisha yako. Kwa kukaa kwenye maono na misingi hiyo unakuwa na uhakika wa kujenga mafanikio makubwa kwako.

Maisha yako yanajengwa na vitu vinne ambavyo vinategemeana sana kwenye kuwa na maisha ya mafanikio. Vitu hivyo ni kama ifuatavyo;

Moja ni usalama, hapa unahakikisha kwamba maisha yako hayawi kwenye hatari.

Mbili ni hekima, hapa unajua kilicho sahihi kufanya na kukifanya.

Tatu ni mwongozo, hapa unapata mwelekezo wa kule unakotaka kufika.

Nne ni nguvu, hizi ndiyo zinakuwezesha kupata kile unachotaka.

Maisha ya mafanikio ni yale ambayo yana usalama, hekima, mwongozo na nguvu.

Hatua muhimu ya kuchukua kwenye tabia hii ya pili ni kujenga taswira ya kifikra ya aina ya maisha unayoyataka na kuiweka kwenye fikra zako kwa muda mrefu. Pia unapaswa kuwa na kauli chanya (affirmations) ambazo unajiambia mara kwa mara. Zoezi hili la kuwa na taswira na kauli chanya, zinaelekeza fikra zako kwenye fursa sahihi kwako kupata mafanikio unayoyataka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mpana zaidi wa dhana hii ya USHINDI BINAFSI kwenye kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu. Karibu usikilize kipindi hapo chini ili uendelee kujifunza na kuchukua hatua za kuyabadili maisha yako na kukupa mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.