Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya pili.
Na kwenye kanuni ya pili tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni epuka kuwaambia watu wamekosea hata kama una uhakika na hilo badala yake tengeneza mazingira ya kumsaidia mtu kuuona ukweli yeye mwenyewe. Kwa njia hiyo, watafurahia kuongea na wewe kwa sababu wanajua unawasaidia kuona ukweli.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Pili
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya tatu ambayo ni kubali haraka na kwa dhati.
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea, sisi binadamu huwa tunakosea mara nyingi kuliko tunavyopatia, lakini pia huwa hatupendi kuambiwa tumekosea hata kama ni kweli.
Kwa kuwa sisi ni wauzaji na tunajifunza masomo ya ushawishi, ipo njia nyingine ambayo inaweza kutusaidia sana kuwashawishi wengine kukubaliana na sisi, na njia hiyo ni kukubali haraka na kwa dhati pale unapokuwa umekosea.
Unatakiwa kufanya hivyo haraka kabla mtu mwingine hajakuambia umekosea, kiri kosa ulilofanya na onesha kujutia kosa hilo.
Kwa kuchukua hatua hiyo, mtu mwingine anakosa hoja ya kukushambulia nayo na inabidi achukue nafasi yako.
Atakuonea huruma na kuwa tayari kukusaidia katika kosa hilo.
Kwa mfano, mtoto akikosa na akaenda kumuomba mzazi msamaha, kukiri kosa yeye mwenyewe kwa haraka kabla hajaambiwa na mzazi wake, mzazi anakuwa rahisi kumwonea huruma na kumsamehe bila kumwadhibu.
Ila yule mtu anayekuwa mgumu na kubisha, anakuwa kama anakuongezea hasira zaidi.

Chukulia hata barabarani, kama umefanya kosa la kuvunja sheria za barabarani kama dereva na pale unaposimamishwa na askari, ukikiri kosa yaani kutambua kosa lako na kuomba msamaha, yule askari anakusamehe haraka sana kuliko yule mtu ambaye anakuwa kiburi na mjuaji.
Mwandishi Dale Carnegie anatushirikisha kisa ambacho yeye mwenyewe amewahi kukutana nacho, siku moja akiwa matembezini kwenye eneo la hifadhi alikuwa akimwachia mbwa wake bila kumfunga.
Kisheria inapaswa mtu atembee na mbwa akiwa amefungwa ili asidhuru wanyama wadogo wadogo.
Siku Dale Carnegie alikutana na askari anayelinda hifadhi, ambaye alimkamata kwa kosa la kutembea na mbwa bila kumfunga, kosa ambalo alipaswa kulipa faini.
Sasa alichofanya Dale, ni kukiri kosa haraka kabla hata askari hajamwambia kosa lake, na kueleza ni jinsi gani amekuwa mzembe kwa kumwachia mbwa kiasi cha kuhatarisha maisha ya wanyama wadogo wadogo.
Cha kushangaza sasa, askari yule usijali, ni makosa madogo madogo hayo, endelea na mbwa wako ila hakikisha hadhuru wanyama.
Hapa tunajifunza kitu kimoja kizuri zaidi ambacho ni, kwa kukiri kwake kosa kulimfanya askari akose cha kumhukumu na hivyo kuwa upande wake.
Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, unapaswa kuwa na tabia hii ya kukiri kosa kwa mteja wako au kwa mtu yeyote ambaye umemkosea kabla hata yeye hajachukua hatua. Unapojua tu umekosea, kiri kosa haraka ili umfanye mkosewa kuwa upande wako na kukusaidia.
Kitendo cha kukiri makosa yetu kama wakosa pale tunapokosea, kinawafanya wale tunaowakosea kushindwa kutuhukumu na hivyo kuwa upande wetu. Kwa namna hiyo, unakuwa umeshajenga ushawishi hivyo kukubaliana na wewe kwenye jambo lako.
Unapokiri kosa, unawafanya watu wajisikie vizuri na kuona nao wanathaminiwa na hivyo kuona nao hawana budi kukusamehe ili maisha yaendelee.
Kitendo cha kukiri kosa, unakuwa unamteka yule uliyemkosea na kuyeyusha hasira ambazo alikuwa nazo. Unapokosea na kuongea ubishi na ujuaji, kuna mfanya mtu azidi kukuhukumu na kupunguza nguvu ya ushawishi.
Kama unajua umekosea, unajua wazi kwamba wengine watakusema na kukukosoa kwa kile ulichofanya. Sasa kwa nini usianze kufanya hivyo wewe mwenyewe. Kwa kukiri makosa yako kabla ya wengine hawajafanya hivyo, utawaondoa kwenye hali ya kukushambulia na kuwaweka kwenye hali ya kutaka kukusaidia.
Mpumbavu yeyote anaweza kuficha na kutetea makosa yake, na wapumbavu wengi hufanya hivyo.
Usiwe mpumbavu, unapokosea kiri makosa yako haraka na hilo litawafanya watu wakuheshimu zaidi, maana siyo wengi ambao wako tayari kukiri makosa yao.
Mwisho, unapokuwa sahihi na wengine wamekosea, tumia njia ya makubaliano kuwasaidia wengine kuona kilicho sahihi. Unapokuwa umekosea, na wengine wako sahihi, kiri haraka makosa yako na kwa dhati.
Kwa kufanya haya mawili kila wakati, siyo tu utaondoa migogoro kwenye maisha yako, bali pia utawafanya wengine wakubaliane na wewe maana hakuna cha kukupinga.
Kaongeze ushawishi kwa wateja wako na wale ambao mnahusiana kwa kuwa mtu wa kukiri kosa pale unapokuwa umekosea kabla mhusika hajaanza kukushambulia kwa namna yoyote ile.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz