Rafiki yangu mpendwa,

Kama utakutana na mtu ambaye anakazana kukata mti kwa kutumia msumeno, ambapo licha ya kuweka juhudi kubwa hakamilishi, unaweza kumuuliza kama amenoa msumeno wake. Iwapo utamuuliza hivyo na akakuambia hajanoa kwa sababu hana muda wa kupoteza, utamshangaa sana. Hiyo ni kwa sababu unajua kama angetenga muda na kunoa msumeno wake, angerahisisha zaidi kazi yake.

Rafiki, jambo la kushangaza ni kwamba hivyo ndivyo wewe pia umekuwa unafanya kwenye maisha yako. Kuna msumeno ambao unapaswa kuunoa ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio makubwa. Lakini kwa kuwa unahangaika na mambo mengi, unaona huna muda wa kunoa msumeno huo. Matokeo yake ni unaweka juhudi kubwa, miaka nenda, miaka rudi lakini hakuna mafanikio makubwa unayopata.

xr:d:DAF_0orONc8:188,j:6994514058668288571,t:24040418

Mwandishi Stephen Covey, kwenye kitabu chake kinachoitwa The Seven Habits of Highly Effective, ametushirikisha tabia saba za msingi za mtu kujijengea ili kuwa na maisha ya mafanikio. Katika tabia hizo, tabia ya saba anaiita NOA MSUMENO (SHARPEN THE SAW).

MAANA YA KUNOA MSUMENO.

Mwandishi anaelezea kunoa msumeno kama kitendo cha kujiboresha wewe mwenyewe ili uweze kufanya makubwa kadiri ya unavyotaka. Ni kufanya uwekezaji ndani yako mwenyewe, ambao ndiyo uwekezaji bora kuliko wote unaoweza kufanya.

Kuna aina nyingi za uwekezaji unazoweza kufanya, lakini ni uwekezaji wa ndani yako mwenyewe ambao huwezi kuupoteza kamwe. Unaweza kupoteza uwekezaji mwingine wote unaofanya, lakini uwekezaji unaofanya ndani yako, huwezi kuupoteza. Hakuna anayeweza kukuibia au kukunyang’anya uwekezaji uliofanya ndani yako.

Hivyo kama kuna eneo moja ambalo unapaswa kulipa kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako basi ni kuwekeza ndani yako mwenyewe. Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni unawekezaje ndani yako mwenyewe? Majibu unakwenda kuyapata hapa.

MAENEO MAKUU MANNE YA MAISHA YAKO.

Maisha yetu binadamu yamegawanyika kwenye maeneo makuu manne. Hayo ndiyo maeneo ambayo unapaswa kuyaendeleza ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Hapa unakwenda kujifunza maeneo hayo na hatua za kuchukua ili kuyaboresha.

Eneo La Kwanza; Mwili.

Mwili wako ndiyo hekalu lako, hiyo ndiyo nyumba ambayo utaishi kwa kipindi chote cha uhai wako. Mwili wako utakuwezesha kujenga mafanikio makubwa kama utakuwa na afya imara. Hivyo uwekezaji unaopaswa kuufanya kwenye mwili ni wa kujenga afya imara.

Afya imara inajengwa kwa vitu vitatu;

i. Kula kwa usahihi, hapa unapaswa kula vyakula ambavyo ni vizuri kwa afya yako. Epuka sukari, punguza wanga na kula protini, mafuta, mbogamboga na matunda kwa wingi.

ii. Kufanya mazoezi, hapa unapaswa kuwa na mazoezi ya mwili unayofanya ambayo yanaufanya kuwa imara kwa kuongeza kinga.

iii. Kupumzika, hapa unapaswa kutenga muda wa kupumzika ili kuupa mwili nafasi ya kujiponya kwa yale ambayo umepitia.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu BULLETPROOF DIET (Mfumo Bora Wa Ulaji Utakaokuwezesha Kupunguza Uzito, Kuwa Na Nguvu Na Umakini Mkubwa Na Kuwa Na Afya Bora)

Eneo La Pili; Akili.

Akili ndiyo mwongozo wa maisha yako, ndiyo kitu kinachokuongoza nini ufanye au usifanye. Afya ya akili yako ni eneo muhimu la kufanyia kazi ili kuweza kufanikiwa. Akili yako inaboreshwa kwa kufanya mambo manne;

i. Kusoma, usomaji ndiyo unailisha akili yako, na hapa ni usomaji wa vitabu ambavyo vinakupa maarifa na siyo habari za udaku.

ii. Kuandika, uandishi ni kupakua mawazo yaliyo kwenye akili yako, ukiweza kuandika unaweza kupangilia mawazo yako. Jiwekee utaratibu wa kuandika mawazo yako, inatuliza mawazo yako, kupunguza msongo na kutunza kumbukumbu.

iii. Kupanga, hapa unaweka mipango mbalimbali ya mambo unayofanya.

iv. Taswira, hapa unatengeneza picha ya kifikra ya yale unayotaka, picha hiyo ndiyo inakupa msukumo wa kupata mafanikio unayotaka.

Eneo La Tatu; Imani/Roho.

Imani au roho ndiyo sehemu kuu ya maisha yetu, ndiyo kiini chetu. Kile tunachojiita sisi, ni roho zetu. Kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa kiroho ambao tupo kwenye mwili. Unaposema mkono wangu, maana yake wewe ni ile roho iliyo ndani ya mwili. Na ndiyo maana mtu akifa, mwili wake unaitwa maiti au mwili wa marehemu, maana yake hayupo tena pale. Roho inakuwa imeacha mwili. Kujiimarisha kiroho, fanya mambo haya;

i. Sali, sala ni njia yenye nguvu ya kujijenga kiroho kulingana na imani yako.

ii. Tahajudi (meditation), hii ni njia ya kutuliza fikra zako ambapo kunakupa utulivu mkubwa wa kiroho.

iii. Kujifunza kwa kina kulingana na imani yako. Kila imani ina misingi na maadili yake, kadiri unavyojifunza, kuelewa na kuishi misingi hivyo, ndivyo unavyokuwa na maisha imara.

Eneo La Nne; Hisia/Jamii.

Hisia na jamii ni mahusiano na ushirikiano ambao tunao na watu wengine. Hisia zetu zinahusika zaidi na watu wengine, na jinsi tunavyozidhibiti pamoja na kushirikiana vyema na wengine ina athari kwenye mafanikio yetu. Katika kujijenga kihisia na kijamii, fanya yafuatayo;

i. Toa huduma kwa wengine, kwa chochote unachofanya, yafanye maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

ii. Kujali, kwa kuweka mbele maslahi ya wengine na siyo ya kwako tu.

iii. Ushirikiano mzuri na wengine, kwa sababu huwezi kufanikiwa peke yako, unawahitaji sana wengine.

iv. Usalama wa ndani, huu ni muhimu kwako ili uweze kujiamini na kuaminika na wengine. Bila ya usalama wa ndani, huwezi kushirikiana vizuri na watu wengine.

USHINDI WA KILA SIKU.

Haya tuliyojifunza kuhusu uwekezaji binafsi, yanaweza kuonekana ni mengi na magumu kufanya. Lakini siyo, matatu ya kwanza, yaani MWILI, AKILI na IMANI/ROHO unaweza kuyafanya wewe mwenyewe, kwa kuanzia popoye ulipo bila ya kuhitaji kuingia gharama yoyote.

Ili yawe na manufaa kwako na uweze kujenga mafanikio makubwa, hayo matatu unapaswa uyafanye kila siku. Kwa kuweza kuyakamilisha kila siku unakuwa umejijengea ushindi wa uhakika kwenye kila siku yako.

Unachopaswa kufanya ni kutenga saa moja kila siku kwa ajili ya ushindi huo wa kila siku. Kwenye saa yako moja unayotenga, igawe kwa namna hii;

i. Dakika 20 kwa ajili ya ROHO/IMANI, tumia muda huo kusali, kutahajudi na kujifunza imani.

ii. Dakika 20 kwa ajili ya AKILI, tumia kusoma angalau kurasa 10 za kitabu, andika, panga na weka taswira kwenye akili yako.

iii. Dakika 20 kwa ajili ya MWILI, tumia hizi kufanya mazoezi ya mwili wako.

Kwa kuwekeza saa moja kila siku kwenye USHINDI WA KILA SIKU kutakuwezesha kujenga maisha yenye mafanikio makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu kunoa msumeno wako ili kuweza kujenga mafanikio ya uhakika. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini ili uendelee kujifunza na kufanya uwekezaji sahihi kwako na kunufaika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.