Rafiki yangu mpendwa,

Katika viumbe wote ambao wapo hapa duniani, sisi binadamu ndiyo viumbe ambao tumepewa uwezo mkubwa kuliko wengine wote.

Uwezo tulionao ni wa akili ya kipekee kabisa ambayo inaweza kufikiri na kufanya maamuzi kwenye mambo mbalimbali. Lakini zaidi akili hiyo huwa ina uwezo wa kujenga taswira ya kitu ambacho hakipo kabisa na tukaweza kuamini na hata kukileta kwenye uhalisia.

Tulitegemea kwa uwezo huo mkubwa, hasa wa kutengeneza taswira, basi tungeutumia kutengeneza taswira chanya za yale ambayo tunayataka na kuweza kuyafikia. Lakini sivyo ilivyo kwenye uhalisia, kwani tumekuwa tunatumia uwezo huo mkubwa wa kujenga taswira kutengeneza mambo ambayo yanatukwamisha.

Badala ya kutengeneza taswira ya mambo mazuri tunayoyataka, tunatengeneza taswira ya mambo mabaya ambayo hatuyataki. Matokeo yake ni taswira hizo zinatupa hofu na kuishia kushindwa kupiga hatua ambazo tungeweza kupiga.

Hali hii ya kujenga taswira hasi imekuwa inatupa maumivu mara mbili, kwanza tunaumia kwa taswira tunayokuwa nayo na pili tunaumia kwenye uhalisia. Hili ndiyo limekuwa kikwazo kwa watu wengi kuwa na maisha ya mafanikio.

Rafiki, unaweza kusema kuwa na taswira hasi kwenye fikra zako kunakuandaa na hali hiyo pale inapojitokea. Sawa, lakini pale unapofikiria hayo mabaya yanayotokea kabla hata hayajatokea, inakunufaisha nini?

Rafiki, kama mabaya au magumu yatatokea, utayakabili pale yatakapotokea. Kuhofia sasa wakati bado hayajatokea, haitakusaidia kwa vyovyote vile. Badala yake itakuzuia kuchukua hatua unazopaswa kuchukua sasa ili kupata yale matokeo unayopaswa kupata.

SOMA; 2254; Wakati Sahihi Wa Kuvuka Daraja…

Na hapa ndipo kauli ya UTAVUKA DARAJA PALE UTAKAPOLIFIKIA inapohitajika sana kwako ili uweze kuwa na utulivu. Unachopaswa kujua ni kwamba haijalishi utahofia kiasi gani kuhusu mambo yanayoweza kutokea kesho, huna namna ya kuyaathiri.

Wajibu wako ni kuishi vizuri leo, kwa kutekeleza yale unayopaswa kuyatekeleza. Kisha kuwa na maandalizi sahihi ya kuweza kukabiliana na chochote kinachoweza kutokea kesho. Usipoteze muda wako kufikiria kesho itakuwaje, kuwa na maandalizi mazuri leo na kesho utaikabili kama ulivyoikabili leo.

Kama unataka kutoka nyumbani kwako kwa kuendesha gari ili kufika eneo unalotaka, ukisubiri mpaka taa zote ziwe kijani ndiyo utoke, kamwe hutatoka. Badala yake unatoka, ukikutana na yaa nyekundu unasubiri, ukikutana na kijani unakwenda. Hatua kwa hatua mpaka unafika kule unakotaka kufika.

Changamoto zozote unazoona utakutana nazo kwenye safari yako ya mafanikio, zisikusumbue kwa sasa. Badala yake jiandae uweze kukabiliana nazo pale zitakapotokea. Kwani hata ukihangaika nazo kiasi gani kwa sasa, huna namna ya kuziathiri.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina zaidi dhana hii ya kuvuka daraja pale unapolifikia. Karibu uangalie kipindi hicho hapo chini ili uweze kukaa kwenye safari yako ya mafanikio bila ya kuyumbishwa na chochote.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.