Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio makubwa kwenye maisha, huwa yanakuja na gharama kubwa pia.

Lakini kwa bahati mbaya sana, huwa hatuoni gharama ambazo waliofanikiwa wamelipa. Na hivyo kudhani safari ya maisha ya wale waliofanikiwa ilikuwa rahisi kuliko ya wengine wanaoshindwa.

Kwa asili, wanaofanikiwa sana ndiyo pia wamekuwa ambao walipitia magumu sana. Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni uwezo wa kuyavuka magumu yao na kupambania ndoto zao.

Joanne K. Rowling ni mwandishi wa nchini Uingereza ambaye ndiye mtu wa kwanza kuwa bilionea kutokana na uandishi. Yaani shughuli yake kuu iliyompa ubilionea ni vitabu alivyoandika. Huyu ni mwandishi wa vitabu maarufu vya hadithi vinavyoitwa HARRY POTTER.

Maisha ya Joanne hayakuwa rahisi kama inavyoonekana baada ya kufanikiwa. Alikulia kwenye familia ambayo haikuwa na maelewano mazuri, ambapo mama yake alikuwa na ugonjwa sugu na kufariki akiwa bado ni binti.

Alihama kutoka nchi yake ya Uingereza na kwenda nchi ya Ureno ambapo alifanya kazi kama mwalimu wa Kiingereza. Chuoni alisomea fasihi ya Kifaransa na ya kale.

Tangu akiwa mtoto alipenda kuandika, lakini hakuwa ameweka umakini mkubwa kwenye kuendeleza uandishi wake.

Akiwa nchini Ureno alikutana na mwanaume ambaye alimwoa, wakapata mtoto mmoja. Lakini ndoa ilikuwa ya migogoro na kutokuelewana, kitu kilichopelekea ndoa hiyo kuvunjika.

Joanne alilazimika kurudi nchini Uingereza, ambapo hakuwa na kazi ya kufanya, huku pia akiwa na mtoto ambaye alimlea peke yake. Alilazimika kuishi kwa kutegemea misaada ya serikali.

Katika wakati huu ndiyo aliamua kuweka umakini mkubwa kwenye uandishi wake na kukamilisha kitabu cha kwanza cha HARRY POTTER. Kitabu hicho alikuwa ameanza kukiandika muda mrefu, na wazo la kukiandika alilipata akiwa kwenye treni.

SOMA; Jifunze Ung’ang’anizi Wa Rambo Ili Uweze Kupata Mafanikio Makubwa.

Msukumo wa kuandika kitabu hicho pamoja na visa vingi alivitoa kwenye maisha yake moja kwa moja. Yale aliyoyapitia kwenye maisha pamoja na watu aliohusika nao waliweza kuchangia kwenye matukio ya hadithi yake.

Alipokamilisha kuandika kitabu, japo kwa taabu kwa sababu ya malezi ya mtoto, alituma kwa wachapaji wengi. Wachapaji wote walipitia kitabu chake walikataa kukichapa, wakimweleza kwamba hakiwezi kuuza. Aliendelea kutuma kitabu kwa wachapaji kwa zaidi ya mwaka mmoja bila ya mafanikio.

Baadaye mchapaji mmoja alikubali kukichapa, kwa kiwango kidogo, akimsisitiza kwamba atafute kazi ya maana ya kufanya kwa sababu uandishi wa vitabu vya hadithi hauwezi kumpa kipato cha kuendesha maisha.

Mambo yalikuwa tofauti pale kitabu kilipochapwa, kwani kulipokelewa kwa ukubwa sana na wasomaji wa kila rika. Hapo alipata ruzuku ya kuendelea kuandika mwendelezo wa vitabu vingine mpaka kufikia vitabu 7 kwenye mfululizo wa HARRY POTTER.

Vitabu hivyo vimeshikilia rekodi ya kuwa vitabu vilivyouzwa sana na kwa muda mrefu kwenye orodha maarufu ya NEW YORK TIMES BESTSELLER LIST. Vitabu hivyo pamoja na bidhaa nyingine zilizotokana navyo, kama filamu na vitu vingine vimeweza kumfikisha kwenye ubilionea.

Kuna mengi sana ya kujifunza kwenye safari hii ya maisha ya J.K. Rowling. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumeyajadili kwa pamoja na washiriki wa kipindi hicho. Fungua hapo chini uweze kujifunza hayo ambayo washiriki wa kipindi waliweza kuondoka nayo kutokana na safari ya Joanne.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.