Habari Njema Wauzaji Bora Kuwahi Kutokea.
Mafanikio ambayo tunayapata kwenye kila eneo la maisha yetu, yanategemea sana aina ya watu ambao wanatuzunguka. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio yako kwenye mauzo, yanategemea sana aina ya watu wanaokuzunguka. Ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, lazima uchague kuzungukwa na watu sahihi.
KAA KWENYE CHUPA.
Ukichukua mdudu aina ya kaa na ukamweka kwenye chupa, kama hutafunika chupa hiyo atatoka kwenye hiyo chupa na kuwa huru. Lakini ukiweka kaa zaidi ya mmoja kwenye chupa, huna haja ya kuifunga hiyo chupa, kwani pale kaa mmoja atakapokazana kutoka kwenye hiyo chupa, kaa mwingine anamvuta na kumrudisha ndani ya chupa.
Hivyo pia ndivyo binadamu tulivyo, watu waliokuzunguka hawatakuachia uwe zaidi ya vile ulivyo sasa. Wanataka ubaki vile ulivyo, ambavyo pia ndivyo walivyo. Kila unapojaribu kufanikiwa ukiwa umezungukwa na watu ambao hawajafanikiwa, unaishia kuanguka na kubaki pale ulipo.
Pamoja na changamoto nyingine zinazokuangusha, wanaokuzunguka ni sababu namba moja ya kushindwa kufanikiwa. Kwa sababu hao hawawezi kukubali upande juu na kuwaacha wao chini. Wanataka mbaki pamoja, muendelee kulalamika pamoja na kufarijiana pamoja.

WASTANI WA WATU WATANO.
Jim Rhon alikuwa na kauli yake maarufu kwamba mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano wanaokuzunguka, ambao unatumia nao muda wako mwingi.
Kauli hiyo inaendelea kusisitiza athari ya watu wanaokuzunguka, hakuna namna unaweza kufanikiwa kuliko mafanikio ambayo watu hao wanayo. Kama unataka kupata mafanikio makubwa, halafu umezungukwa na watu ambao hawajafanikiwa, unakuwa umeshashindwa kabla hata ya kuanza.
Hata ukazane kiasi gani, matokeo utakayoyapata yataishia kufanana na wale wanaokuzunguka. Hakuna namna utaweza kupata matokeo makubwa kuliko hao unaotumia nao muda wako mwingi.
Hivyo kama unataka kujenga mafanikio makubwa, anza kwa kubadili watu ambao unatumia nao muda wako mwingi. Chagua kwa usahihi kama ambavyo utaendelea kujifunza kwenye somo hili.
USICHEZE NA WALE.
Tangu ukiwa mtoto, wazazi wako walikuwa wakikuasa ni watoto wa aina gani usicheze nao. Watoto waliokuwa na tabia mbaya, wasiosikia na wasiofanya vizuri shuleni, uliambiwa usicheze nao. Huenda walikuwa ndiyo marafiki zako na hukuwa unawaelewa wazazi wako kwa nini wanakuambia usicheze nao.
Ulikuwa pia unajitetea kwamba unaweza kukaa na watoto hao ambao wana tabia mbaya lakini usiige tabia zao. Lakini ulikuwa ni utoto tu, hukujua athari ya wale wanaokuzunguka kwenye maisha yako, jinsi walivyo na ushawishi mkubwa kwako.
Pamoja na kwamba umeshakuwa mtu mzima sasa, lakini bado hujaelewa madhara ya wale wanaokuzunguka. Unatumia muda mwingi na watu ambao hawajafanikiwa halafu unataka upate mafanikio makubwa, hicho ni kitu ambacho hakiwezekani.
Huu ni wakati mzuri kwako kurejea kwenye hekima za wazazi wako ambao walikuambia usicheze na watoto wa aina fulani. Kwa sasa ni usicheze na mtu yeyote ambaye hana kiu ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
SOMA; Hapa Ndio Unapoweza Kuwapata Watu Watano Wanaokuzunguka Watakaokuwezesha Kufikia Mafanikio Makubwa.
WATU SAHIHI WA KUZUNGUKWA NAO.
Kwa lengo lako la kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea ili uweze kufanya mauzo makubwa, unapaswa kuzungukwa na watu sahihi ambao wana sifa zifuatazo;
1. Wana malengo ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao na wanapambana kila siku kupata mafanikio hayo.
2. Wanafikiri chanya na uwezekano, kamwe hawaongei mambo hasi wala kusema haiwezekani.
3. Wanakutia moyo kwenye ndoto kubwa ulizonazo na wanaenda hatua ya ziada kukupambania ili ufikie ndoto hizo.
4. Wanapenda kujifunza kupitia kusoma vitabu na kupata mafunzo mbalimbali yanayowafanya kuwa bora zaidi.
5. Wanaendelea kuweka juhudi kubwa na kwa matumaini licha ya kupitia magumu na changamoto mbalimbali.
6. Hawakuonei wivu pale unapopiga hatua kubwa kuliko wao, badala yake wanafurahia na kukazana kupiga hatua kama zako.
7. Hawana tabia za majungu na kusengenya wengine, wanatumia muda wao kwenye kupambania malengo yao badala ya kufuatilia maisha ya watu wengine.
Kwa sifa hizi na nyingine zinazoendana nazo, utakuwa umewapata watu sahihi ambao ukizungukwa nao lazima utapiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
MTU WA MFANO KWAKO.
Kwenye maisha unapaswa kuchagua mtu wa mfano kwako (role model), mtu ambaye unataka kufikia mafanikio ambayo yeye amefikia. Mtu huyo anaweza kuwa hai au alishakufa, wa karibu au wa mbali. Muhimu ni awe ni mtu ambaye anakupa msukumo mkubwa wewe kupambana ili ufanikiwe.
Ukishamchagua mtu huyo, jifunze kila kitu kuhusu yeye. Soma historia ya maisha yake, jua mengi sana ambayo alipitia kwenye maisha yake mpaka kuweza kufanikiwa. Kama ni mtu aliye hai na karibu, tafuta nafasi ya kukutana naye ili kujifunza kutoka kwake moja kwa moja. Kama ni mtu ambaye alishafariki au yuko mbali hivyo huwezi kumfikia, jifunze kupitia taarifa zake zinazopatikana.
Kwa kila unachofanya kwenye maisha yako, jiulize kama angekuwa mtu wa mfano kwako angefanyaje? Kwa kujiuliza swali hilo utafanya mambo mengi kwa usahihi badala ya kufanya tu kwa mazoea. Kwa kila changamoto unazopitia, angalia mtu wako wa mfano alivukaje changamoto za aina hiyo na utapata mwongozo mzuri.
YA KUJIFUNZA KWA WALIOSHINDWA.
Kama huna watu sahihi wa kukuzunguka au huna waliofanikiwa ambao unaweza kujifunza kwao, bado una mengi ya kujifunza kwa wale ambao wameshindwa.
Hapa unaangalia yale ambayo wale walioshindwa wamekuwa wanayafanya kwenye maisha yako kisha usiyafanye kabisa. Yaani kile ambacho kinafanywa na watu walioshindwa, wewe usikifanye.
Hapa angalia watu ambao unawajua kwenye maisha yako na hutaki maisha yako yaishie kuwa kama yao. Kisha angalia ni mambo gani waliyafanya mpaka kuwa na maisha kama hayo. Ukishayajua mambo hayo, kataa kabisa kuyafanya.
Kwa kwenda kinyume na wale walioshindwa, unaishia kupata ushindi. Una mengi ya kujifunza kwa walioshindwa, wajibu wako ni kujua makosa waliyofanya kwenye maisha yao na kuepuka kuyarudia.
ZUNGUKWA NA VITABU.
Kitu kimoja ambacho unapaswa kukipa muda wako mwingi kwenye maisha ili uweze kufanikiwa ni vitabu. Soma sana vitabu, tumia muda wako wa ziada kwenye kujifunza. Igawe siku yako kwenye mambo makubwa mawili tu; kufanya kazi na kujifunza.
Chagua kila wakati kuwa kwenye hali moja kati ya hizo mbili, kufanya kazi au kujifunza. Kama hujifunzi basi unafanya kazi na kama hufanyi kazi basi unajifunza. Kwa kuweka muda wako ambao hufanyi kazi kwenye kujifunza, unaondoa hatari ya kuzungukwa na watu ambao siyo sahihi.
Ukianza kuweka kipaumbele kwenye kujifunza, wale ambao siyo sahihi wataanza kukukimbia wao wenyewe na hivyo kukupa muda mwingi zaidi wa kujifunza. Na unapofanyia kazi yale unayojifunza, unaweza kupiga hatua kubwa sana.
Tayari unazo zana za kujifunza, una kitabu chako cha CHUO CHA MAUZO na una mtandao wa AMKA MTANZANIA. Ukitumia muda wako kujifunza kwenye vyanzo hivyo viwili na kuweka kwenye matendo, utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, jifanyie ukaguzi wa kupitia watu wote ambao unatumia muda wako mwingi kuwa nao. Jiulize kwa kuambatana na watu hao utafika wapi. Kisha chukua hatua sahihi kama ulivyojifunza kwenye somo hili ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
Ni maajabu kabisa yale mabadiliko chanya yanayo kuja kwa kubadili wanaokuzunguka,
Nitafanyia kazi zaidi mgawanyo wa siku, kujifunza na kufanya kazi
LikeLike
Vizuri.
LikeLike