Rafiki yangu mpendwa,
Chochote unachotaka kwenye maisha yako, tayari wanacho watu wengine. Ili uweze kupata kila unachotaka kutoka kwa wale ambao wanacho, kuna njia mbili unazoweza kutumia.
Njia ya kwanza ni kuchukua kwa nguvu au hila bila ya ridhaa yao. Hapa unatumia njia za mabavu au wizi kuchukua kile ambacho wengine wanacho. Njia hii huwa siyo nzuri, kwani mwisho wake huwa ni mbaya.
Njia ya pili ni kuwashawishi watu wakupe kwa ridhaa yao wenyewe kile walichonacho. Siyo tu wanakupa, bali pia wanafurahia kukupa kile unachotaka. Njia hii ni ya uhakika na salama ya kupata unachotaka kwa namna unavyotaka.
Njia ya pili ambayo ndiyo sahihi, ni njia inayotaka mtu kutumia misingi sahihi ya ushawishi. Kwa bahati mbaya sana, sisi binadamu huwa tunashawishika kirahisi sana, pale maeneo fulani yanapoguswa.

Mwanasaikolojia na mwandishi Robert Cialdini kwenye kitabu chake cha INFLUENCE; THE PSYCHOLOGY OF PERSUASION ametushirikisha misingi ya uhakika ya ushawishi, ambayo tukiweza kuitumia tutaweza kuwashawishi watu watupe chochote tunachotaka.
Kwenye kitabu hicho ameshirikisha nyenzo saba za ushawishi ambazo tunapaswa kuzijua jinsi zinavyofanya kazi kwa malengo mawili. Lengo la kwanza ni kuzitumia kuwashawishi wengine watupe tunachotaka. Na lengo la pili ni kuwazuia wale wanaozitumia kwa hila wasiweze kujinufaisha kupitia sisi.
Hivyo hata kama unajiambia huhitaji kuongeza ushawishi, bado unapaswa kujifunza hapa kwa sababu bila ya kujua umekuwa unashawishiwa vibaya na watu kujinufaisha kupitia wewe huku ukiumia.
Zifuatazo ni nyenzo saba za ushawishi zinazofundishwa kwenye kitabu cha INFLUENCE.
Nyenzo ya kwanza ni FADHILA.
Binadamu huwa hatupendi kuwa na deni, hivyo pale watu wanapotupa vitu, tunalazimika kuwapa vitu pia kama kulipa fadhila. Hii ni njia ambayo imekuwa inatumika kuwashawishi watu, kwa kuanza kuwapa vitu ili nao wawe tayari kutoa vitu.
Ili kuwashawishi watu, anza kwa kuwapa kitu fulani na hapo watajiona wakiwa na deni la kukupa kile unachotaka wewe.
Nyenzo ya pili ni KUPENDA.
Watu huwa wanashawishika na kuwaamini wale wanaowapenda na kuwakubali. Kwa kuona mtu yuko kama wao, watu wanakuwa na imani zaidi na kukubaliana naye.
Ili kuwashawishi watu, tengeneza hali ya kupendwa na kukubalika nao kupitia kuwa na mwonekano mzuri, kuonyesha mambo mnayofanana na hata kujihusisha na vitu vinavyopendwa.
Nyenzo ya tatu ni MKUMBO.
Pale ambapo watu hawajui nini cha kufanya au hawana uhakika wa nini wafanye, huwa wanaangalia watu wengi wanafanya nini na kisha kuiga hicho. Sisi binadamu huwa tunaamini wengi wako sahihi na hata kama ni kukosea, bora kukosea na wengi kuliko kuwa sahihi peke yako.
Kuwashawishi watu, waonyeshe kwamba kile unachotaka wakubaliane nacho ndiyo kinachokubalika na watu wengi zaidi. Kwa kufuata mkumbo watu hao nao watashawishika.
SOMA; Jifunze Kuwa Na Ushawishi Mkubwa Kutoka Kitabu HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE.
Nyenzo ya nne ni MAMLAKA.
Tumefundishwa kuwatii wale wenye mamlaka, kwa sababu tunaona wanajua kuliko sisi kwenye maeneo yao. Mtu anapokuwa na mamlaka kwenye eneo fulani, tunamsikiliza na kushawishika naye, bila hata ya kuhoji.
Kuwashawishi watu, onyesha mamlaka uliyonayo juu ya kile unachotaka wafanye, hapo utakuwa na ushawishi mkubwa.
Nyenzo ya tano ni UHABA.
Binadamu huwa tunathamini zaidi vitu ambavyo havipatikani kwa urahisi. Hivyo kitu kinapokuwa na uhaba, huwa tunashawishika nacho zaidi. Kitu kikiwa kinapatikana kwa wingi, tunajua kipo tu muda wote na hivyo hatusumbuki sana. Lakini pale tunapoona kuna nafasi ya kupoteza kitu, tunachukua hatua haraka.
Kuwashawishi watu, waonyeshe kile unachotaka wakubaliane nacho kina uhaba, hapo watachukua hatua mara moja ili wasipoteze.
Nyenzo ya sita ni MSIMAMO.
Watu hawapendi kuonekana ni wababaishaji, hivyo huonyesha msimamo kwenye maamuzi ambayo wameshayafanya. Watu wakishafanya maamuzi wanaendelea kuyasimamia ili kuonyesha nguvu yao ya kuamua.
Kuwashawishi watu, waweke kwenye hali ambayo watataka kuonyesha msimamo wao kwenye kitu fulani. Hapo wataendelea nacho bila hata ya wewe kuwalazimisha.
Nyenzo ya saba ni UMOJA.
Kilichowezesha jamii ya binadamu kuvuka magumu na kufanikiwa ni ile hali ya umoja. Uwezo wa kushirikiana pamoja, umepelekea kufanya makubwa kama jamii nzima. Hivyo watu huwa wanashawishika zaidi na mambo ambayo yanaleta umoja.
Kuwashawishi watu, waonyeshe kile unachotaka wakubaliane nacho kinaleta umoja kwako na watu wengine. Hilo litawafanya wachukue hatua kwa kuona ndiyo sahihi.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri sana juu ya nyenzo hizi za ushawishi. Karibu ujifunze kwenye kipindi hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.