Rafiki yangu mpendwa,
Vipi kama ningekuambia kwenye biashara yako kuna mfanyakazi mmoja ambaye ndiye anaikwamisha isiweze kupata ukuaji mkubwa?
Vipi kama nikikuonyesha namna biashara yako itapata ukuaji mkubwa sana kwa wewe kuchukua hatua ya kumfukuza mfanyakazi huyo?
Je utakuwa tayari kuchukua hatua ya kumfukuza mfanyakazi mmoja ambaye amekuwa kikwazo kwenye ukuaji wako ili uweze kukuza sana biashara yako?

Wacha tuone.
Na kabla hatujaendelea, hata kama kwenye biashara uko peke yako, yaani huna mfanyakazi uliyemwajiri, bado unahitaji kumfukuza mtu kazi. Na tena wewe ndiye wa kuchukua hatua haraka sana, maana unajikwamisha sana.
Rafiki, ni nani kwenye biashara yako anayefanya kila kitu?
Nani ambaye kila maamuzi ya biashara ni mpaka kwanza yapite kwake?
Nani ambaye asipokuwepo biashara haiwezi kwenda?
Kama una bahati, mtu huyo ni wewe mwenyewe. Na kama huna bahati, unajikuta ni wewe na kuna wengine pia.
Rafiki, ninachotaka kukuambia ni kwamba wewe mwenyewe ndiye kikwazo namba moja kwenye ukuaji wa biashara yako. Na sababu kubwa ya wewe kuwa kikwazo kwenye ukuaji wa biashara yako ni majukumu yote ya biashara yako kukutegemea wewe.
Sasa wewe kama binadamu, huwezi kufanya mambo yote kwa ufanisi, huna muda wa kutosha na mambo yanakutinga. Hivyo baadhi ya mambo yanakwama.
Lakini mbaya zaidi ni pale unapokwama na kushindwa kuwa kwenye biashara kama ulivyo utaratibu wako. Biashara yako inashindwa kabisa kujiendesha yenyewe.
Hilo la biashara kushindwa kujiendesha zenyewe pale ambapo mmiliki hayupo limekuwa chanzo cha biashara nyingi kufa. Ili kuzuia biashara yako isife, unatakiwa kuanza kujifukuza kazi wewe mwenyewe.
Dhana ya kujifukuza kazi kwenye biashara yako siyo ufunge biashara na kuondoka. Bali ni upunguze majukumu ambayo unayafanya wewe kwa kuajiri watu wengine wayafanye. Hapo unawawekea utaratibu mzuri wa kuyatekeleza na kuleta matokeo mazuri.
Unapaswa kufanyia kazi dhana hiyo hatua kwa hatua. Kila wakati unajifukuza kazi kwenye eneo moja na kumpa mtu mwingine afanye.
Kwa mfano kama umeanza biashara na kila kitu unafanya mwenyewe, unazalisha bidhaa, unatafuta wateja, unawauzia, unakusanya hela n.k. Kadiri unavyokwenda unaanza kujifukuza kazi moja moja. Unaweza kuanza kujifukuza kutafuta wateja, ukamlipa mtu atakayetafuta wateja. Kisha ukajifukuza kazi ya mauzo kwa kuajiri mtu anayeuza. Tena ukajifukuza kazi ya kuandaa bidhaa kwa kuajiri mwandaaji.
Ukienda hivyo, hatua kwa hatua unakuwa unanunua uhuru wako kutoka kwenye biashara yako na kuiwezesha kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea.
Tahadhari muhimu za kuzingatia kwenye hili ni;
1. Ukishajifukuza kazi usirudishe tena pua yako kwenye jukumu hilo. Andaa vizuri miongozo ya ufanyaji kisha wafundishe vizuri watu jinsi ya kufanya. Ukijifukuza kazi halafu ukaanza tena kuingilia hayo majukumu, yatarudi kwako.
2. Unapokuwa huru, yaani biashara haikuhitaji sana, peleka muda wako kwenye kufanya vitu vingine vyenye tija. Ukiwa na muda mwingi na huna cha kufanya, huwa unaishia kufanya uharibifu. Unaweza kujikuta umerudi kwenye biashara yako na kuiharibu.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina kuhusu kujifukuza kazi wewe mwenyewe kutoka kwenye biashara yako. Karibu ujifunze ili ukaweze kurudisha uhuru wako ulioupoteza baada ya kuanzisha biashara.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.