3389; Ushindi ni mabadiliko.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Ushindi ni kitu ambacho kila mtu anakitaka kwenye maisha.
Lakini wachache sana ndiyo wanaoupata ushindi mkubwa wanaoutaka.
Wengi wanashindwa au kuishia kuwa kawaida.

Ukiwaangalia wale wanaoshindwa, siyo kwamba ni wazembe sana.
Wengi wana akili nyingi na wanaweka juhudi kubwa sana.
Pamoja na juhudi hizo kubwa wanazoweka, bado wanaishia kushindwa.

Sababu kubwa inayofanya wengi washindwe ni kutokuwa tayari kubadilika.
Kila mtu huwa anaanza na mpango fulani kwenye safari yake ya mafanikio.
Wanaoshindwa huwa wanabaki kwenye mpango huo bila ya kujali matokeo wanayopata.
Ndiyo maana licha ya kuweka juhudi kubwa, bado wanakuwa hawapati matokeo mazuri.

Wanaofanikiwa wana tabia moja, wanakuwa tayari kubadilika pale hali inapowataka wafanye hivyo.
Wanaanza na mipango, lakini wanakuwa wanajua kwamba mipango siyo matumizi.
Wanajua mambo huwa yanabadilika na hivyo nao wanapaswa kubadilika pia.

Bondia Mike Tyson amewahi kunukuliwa akisema; “Kila mtu huwa ana mpango, mpaka pale anapopigwa ngumi za uso.”
Mafanikio ya mtu yanategemea nini atafanya baada ya kukutana na mambo yanayovuruga mipango yake.
Kama ataendelea kung’ang’ana na mipango hiyo, hataweza kufanikiwa.
Lakini kama atakuwa tayari kubadili mipango yake ili iendane na mabadiliko yaliyotokea, ataweza kupata mafanikio makubwa.

Sababu inayofanya mabadiliko yawe na mchango mkubwa kwenye mafanikio ni watu wengi kutokuwa tayari kubadilika.
Mabadiliko ni kitu kinachoumiza na kuwachosha wengi na hivyo huwa hawakipendelei.
Mabadiliko ni magumu na watu huwa hawapendi vitu vigumu.
Mabadiliko hayana uhakika na watu wanapenda uhakika.
Wale wanaoweza kwenda na mabadiliko vizuri ndiyo wanaoweza kuvuna matokeo bora na kufanikiwa sana.

Rafiki, ni mambo gani makubwa uliyobadili kwenye safari yako ya mafanikio kutokana na mabadiliko yanayoendelea?
Na je upo tayari kiasi gani kukabiliana na mabadiliko licha ya kutokupenda kubadilika ambayo ndiyo tabia ya wengi?
Jipe majibu sahihi kwenye maswali hayo na uchukue hatua sahihi ili uweze kupata ushindi wa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako, Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe