3390; Kuna kitu hakipo sawa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Lengo la kuingia kwenye biashara ni mtu kupata uhuru wa maisha yake.
Kwa kuanza na uhuru wa kazi, kisha uhuru wa fedha na hatimaye uhuru wa muda.
Lakini kiuhalisia, wengi waliopo kwenye biashara wanakosa kabisa hizo aina za uhuru ambazo ndiyo lengo.
Na siyo tu mwanzoni ambapo ni kawaida, bali inakuwa ndiyo sehemu ya maisha ya kila siku.
Biashara zao zinakuwa zinawategemea kwa kila kitu na wasipokuwepo, biashara haiwezi kwenda.
Uzuri ni kwamba matatizo na changamoto zote ambazo biashara inapitia zinaweza kutatuliwa na kitu kimoja kwa uhakika.
Kitu hicho ni faida inayopatikana.
Matatizo mengi ya biashara yanaanzia kwenye faida ya biashara kuwa ndogo au kutokuwepo kabisa.
Faida ni matokeo ya mwisho ya biashara yenye mpango na kuendeshwa kwa usahihi.
Kama faida ni ndogo au haipo kabisa, kuna kitu hakipo sawa.
Inaweza kuwa ni mpango wa biashara haupo sawa au biashara haipaswi kuwepo kabisa.
Tatizo linakuwa mpango wa biashara kama mauzo yapo lakini faida ndiyo haipatikani.
Hapa matatizo yanaweza kuwa;
1. Hujaweka bei kubwa vya kutosha.
2. Gharama za uendeshaji ni kubwa.
Kwa kuanza na kuboresha mpango wa biashara, utaweza kuirudisha biashara yako kwenye njia sahihi.
Tatizo linakuwa biashara yenyewe kutokupaswa kuwepo kama mauzo siyo ya kutosha.
Kama mauzo ya biashara yamekwama, hayakui licha ya juhudi kubwa zinazowekwa, tatizo ni biashara yenyewe.
Na tatizo la biashara linaweza kuwa;
1. Watu hawana uhitaji mkubwa wa kile ambacho biashara inauza, siyo kipaumbele kwao.
2. Ushindani ni mkali sana hivyo wateja waliopo wamegawanyika kwenye biashara zinazoshindana.
Kwa kujua uhalali wa biashara kuwepo au kutokuwepo, utaweza kuchukua hatua sahihi.
Kila kitu huwa kina ukuaji ndani yake, kama ukuaji hauonekani, ni vyema kujua nini hakijakaa sawa na kurekebisha ili ukuaji sahihi uweze kuonekana.
Biashara ni rahisi kuendesha kama una namba za msingi ambazo inazifuatilia kwa karibu na kuchukua hatua sahihi kila mara ili kuboresha namba hizo na biashara kwa ujumla.
Kutoka kwa rafiki yako, Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe