Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya tatu.
Na kwenye kanuni ya tatu tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni unapokuwa sahihi na wengine wamekosea, tumia njia ya makubaliano kuwasaidia wengine kuona kilicho sahihi.
Unapokuwa umekosea, na wengine wako sahihi kiri haraka makosa yako na kwa dhati.

SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Tatu

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya nne ambayo ni anza kwa njia ya urafiki

Mwandishi Dale anatuambia kwamba, pale tunapokuwa tumeshindwa kuelewana na watu na kupatwa hasira. Tunaweza kuwatolea maneno makali ambayo tunafikiri yatawafanya wabadilike.

Lakini hiyo, haijawahi kusaidia, hata kama mtu amekukosea kweli, unapomkabili kwa ukali, unamfanya azidi kusimamia kile alichofanya. 
Haijalishi utakua mkali kiasi gani kwa mtu, ukali wako hautasaidia kumfanya mtu huyo akubaliane na wewe au afanye kile unachotaka.

Aliyekuwa raisi wa Marekani Woodrow Wilson amewahi kunukuliwa akisema, ukija kwangu ukiwa umekuja ngumi, nakuhakikishia nitakunja ngumi haraka kama wewe.
Lakini ukija kwangu na kuniambia hebu tukae chini na tushauriane kwa pamoja na tuelewe kwa nini tunatofautiana, tutakaa chini na tutagundua tunakubaliana kwenye mambo mengi kuliko tunayotofautiana.

Hapa sisi kama wauzaji tunajifunza kwamba, unapokuwa unamwendea mteja kwa ukali ukifikiri kwamba utaweza kumshinda badala yake wewe ndiyo utashindwa. Hakuna uhakika wa ushindi pale ambapo pande mbili zinapokuwa zinatofautiana.
Ukimwendea mteja kwa hasira na yeye atajihami kwa namna ulivyokuja kwa hasira na hutaishia kukosa unachotaka kutoka kwake.

Somo liko wazi, hasira na ukali havitakusaidia kumfanya mtu akubaliane na wewe, hata kama uko juu yake. Hata kama wewe ni mzazi na unayetaka akubaliane na wewe mtoto, au ni bosi na unataka mfanyakazi wako akubaliane na wewe, kutumia nguvu, ukali na hasira havitakusaidia.
Hii ni kwa sababu watu huwa hawapendi kulazimishwa kubadilika, kwa sababu wanaamini wako upande sahihi. Wanakuwa tayari kubadilika pale wanapoamua kubadilika wenyewe.

Swali la kujiuliza, je kama ukali na hasira havisaidii, nini kinaweza kusaidia?

Lincoln amewahi kunukuliwa akisema kauli ya zamani kwamba tone la asali linavutia inzi wengi kuliko galoni la nyongo ni ya kweli na muhimu kuitumia.

Habari njema ni kwamba, kama unataka kuwashawishi watu wakubaliane na wewe, usimtumie galoni la nyongo (Hasira, ukali) bali tone la asali (urafiki).
Anza kwa njia ya urafiki, kwa kumwonesha mtu kwamba uko upande mmoja na yeye na unachomtakia ni kilicho chema. Kwa kuanza kwa njia hiyo, mtu atakuwa tayari kukusikiliza na hapo mnaweza kukubaliana kwenye jambo husika.

Hata kama mtu amekosea na wewe uko sahih, anza kwa njia ya urafiki, usimwoneshe kwamba uko sahihi zaidi yake, bali mwoneshe ungependa mjifunze pamoja. Hapo mtu atakosa cha kupingana na wewe na kuungana na wewe.

Tujifunze kupitia hadithi ya jua na upepo inaweza kutusaidia hapa.
Siku moja jua na upepo walikuwa wanabishana nani ambaye ana nguvu kuliko wenzake. Kila mmoja alitoa hoja zake lakini hawakuwa na njia nzuri ya kupima nguvu zao.
Upepo ukamwambia jua tuthibitishie nani mwenye nguvu ya kumvua mtu huyo koti.

Jua akakubali na upepo ukaanza kutumia nguvu zake. Ulianza kuvuma kwa kiasi na mtu hakuvua koti, ukaendelea kuongeza kasi zaidi na zaidi lakini mtu yule alizidi kushikilia koti lake. Baada ya kuvuma kwa muda na mtu huyo kuzidi kung’ang’ania koti lake, upepo ulikubali umeshindwa na kulipa jua nafasi.

Jua lilichukua nafasi na kuanza kutabasamu, likatoa mwanga wake huku likiendelea kuongeza mwanga huo kidogo kidogo kwa wakati.
Ghafla mtu yule alianza kujifuta jasho, na muda mchache baadaye akavua koti lake yeye mwenyewe bila hata kulazimishwa.
Jua alimwambia upepo, upole na urafiki una matokeo mazuri kuliko hasira na nguvu.

Hatua ya kuchukua leo;
Mara zote unapokabiliana na wengine, tumia upole na urafiki na siyo hasira na nguvu.

Hata pale mteja wako anapokuwa na hasira wewe tumia urafiki na upole kukabiliana naye, na utaweza kumshawishi na siyo kutumia ukali, hasira na nguvu.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz 📞0717101505