Rafiki yangu mpendwa,

Ukienda sehemu ambayo ni mgeni na wale unaokutana nao huwajui, ikitokea mtu ana viashiria vya kitu ambacho unahusika nacho, unaona ni kama unamjua mtu huyo. Kwa mfano kama mtu amevalia jezi ya timu ambayo hata wewe unaishabikia, utamwamini zaidi huyo kuliko wengine.

Mfano huo unaonyesha jinsi ambavyo binadamu tuna tabia ya upendeleo kwa wale watu ambao tunafanana au kuungana nao kwenye vitu fulani. Kitu chochote ambacho kinaleta umoja baina ya watu, huwa kina nguvu ya ushawishi kwa watu. Na hilo linafanya hali ya umoja kuwa nyenzo kubwa ya ushawishi.

Mwandishi Robert Cialdini kwenye kitabu chake cha INFLUENCE ametushirikisha nyenzo saba za ushawishi ambazo tukiweza kuzitumia tutaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Kwenye masomo ya nyuma tumejifunza nyenzo sita ambazo ni ; FADHILA, KUPENDA, MKUMBO, MAMLAKA, UHABA na MSIMAMO. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza nyenzo ya saba na ya mwisho ya ushawishi ambayo ni UMOJA. Tutaona jinsi nyenzo hii inavyoleta umoja na ushawishi na jinsi ya kuepuka isitumike vibaya kwetu.

Nyenzo ya saba ni UMOJA.

Kwa asili sisi binadamu tuna ukabila na upendeleo kwa watu ambao tunajiona kuwa pamoja nao kuliko wale ambao hatupo pamoja nao. Huwa tuna mpaka wa SISI na WAO, tukiwachukulia walio kwenye sisi kama sehemu yetu na walio kwenye wao kama sehemu tofauti na sisi.

Tunawakubali, kuwaamini na kushawishika zaidi na wale walio kwenye kundi la SISI kuliko walio nje ya kundi hilo. Tunawachukulia zaidi chanya wale ambao tupo nao pamoja kuliko ambao hatupo nao pamoja.

Umoja umekuwa na ushawishi mkubwa kwenye maeneo mbalimbali ya maisha.

Kwenye biashara, wateja huwa wanashawishika kununua kwa wauzaji ambao wanaona wako nao pamoja.

Kwenye siasa, watu huwa wanawaamini zaidi wale ambao wako nao kwenye chama kimoja au wana itikadi moja kuliko tofauti.

Kwenye michezo, watu huwa wanawaamini zaidi ale ambao wanashabikia nao timu moja kuliko wa timu tofauti.

Kwenye mahusiano binafsi, huwa tunawaamini wale ambao tupo nao pamoja, kama familia au ndugu kuliko ambao hatupo nao pamoja.

Umoja umegawanyika kwenye makundi mawili; kuwa pamoja na kufanya pamoja.

UMOJA WA I; KUWA PAMOJA.

Umoja wa kuwa pamoja ni ule unaowafanya watu kujiona ni wa aina moja, kwamba wapo pamoja.

Ngazi ya juu kabisa kwenye umoja huu ni ndugu wa damu, ambao wana uhusiano wa moja kwa moja. Hawa wanakuwa pamoja kwa sababu ya undugu wao. Lakini pia watu wanaoishi pamoja kwa muda mrefu huwa wanachukuliana kama ndugu wa damu.

Kutumia maneno kama ndugu, familia na mengine yanayoashiria kuwa pamoja pia huwa ina nguvu ya kuwafanya watu wajione wapo pamoja.

Watu wanaotokea eneo moja huwa pia wanajiona wakiwa pamoja hata kama hawana uhusiano wa karibu. Kitendo cha kutokea eneo moja kinawafanya watu kujiona wapo pamoja. Kadhalika wale waliotumia muda kwenye maeneo yanayofanana pia wanajiona wakiwa pamoja.

UMOJA WA II; KUFANYA PAMOJA.

Pale watu wanapofanya kitu kwa pamoja, huwa wanajiona wakiwa pamoja kuliko wasipofanya kwa pamoja. Mfano pale watu wanapoimba pamoja au kuruka pamoja au kufanya chochote kwa pamoja, wanajiona wakiwa wamoja zaidi kuliko kila mmoja akifanya kitu hicho hicho peke yake.

Muziki umekuwa na nguvu ya kuwaleta watu pamoja, hata kama watu hawaelewi yale yanayoimbwa. Jinsi muziki unavyokuwa, unaibua hisia ndani ya watu na wanapokuwa wanaimba au kucheza pamoja, wanajiona wakiwa kitu kimoja.

Watu wanaotengeneza kitu pamoja pia wanajiona wakiwa wamoja. Kwa mfano watu wanaoanzisha biashara pamoja au wanaofanya kazi ya aina moja, wanakuwa na umoja mkubwa kati yao.

Na pia watu ambao amepitia mateso pamoja, au magumu ya aina yoyote ile huwa wanajiona wakiwa kitu kimoja. Yale wanayokuwa wameyapitia kwa pamoja yanawafanya wajione ni kitu kimoja na hivyo kukubaliana zaidi.

Kumwomba mtu ushauri kunamfanya aone yuko pamoja na wewe kwenye kile ambacho amekushauri. Hilo litamfanya aende hatua ya ziada kuhakikisha unapata matokeo mazuri kwenye kile ambacho amekushauri.

Kulingana na haya tuliyojifunza kwenye umoja, ili uweze kuwashawishi watu, unapaswa kuwafanya waone mko pamoja. Na ili kuwafanya watu waone mko pamoja unapaswa kuwa nao pamoja kwa muda mrefu au kufanya nao kitu kwa pamoja. Hivyo ndivyo unavyoweza kutumia nyenzo hii kuwa na ushawishi mkubwa.

Hatari ya umoja ni watu kufichiana madhaifu yao kwa sababu ya kulindana kunakotokana na hali ya pamoja. Kuzuia hatari hii isilete madhara, inapaswa kuelezwa mapema mambo gani ambayo hayakubaliki ndani ya umoja uliotengenezwa na madhara yatakayowapata wale watakaokiuka. Kisha watu wanapokiuka, wayapate madhara hayo bila ya upendeleo. Hilo litafanya hali ya umoja inayotengenezwa kuwa na manufaa na siyo kutumiwa na baadhi ya watu vibaya.

HITIMISHO LA KITABU; NYENZO ZA USHAWISHI ZITAZIDI KUWA NA NGUVU.

Mwandishi Robert Cialdini anahitimisha kitabu chake cha INFLUENCE kwa kueleza kwamba nyenzo saba za ushawishi alizoshirikisha kwenye kitabu hiki zinazidi kupata nguvu kadiri muda unavyokwenda.

Hiyo ni kwa sababu ufanyaji wa maamuzi unazidi kuwa mgumu kadiri siku zinavyokwenda. Ugumu huo unatokana na taarifa nyingi sana zilizopo kwenye kila eneo la maisha yetu. Ili mtu uweze kufanya maamuzi sahihi, unapaswa kupitia taarifa nyingi sana zilizopo. Hakuna mtu mwenye muda wala utulivu wa kupitia taarifa zote zinazopatikana.

Kutokana na changamoto hiyo, sehemu kubwa ya maamuzi yetu tunayafanya kwa njia ya mkato. Njia hiyo ya mkato ni kutumia nyenzo za ushawishi tulizojifunza. Mifano ya haraka na kwa kila nyenzo ni kama ifuatavyo;

1. Pale watu wanapotupa kitu, tunawalipa fadhila, kwa sababu hicho ndiyo kinaonekana sahihi kufanya. (Nyenzo ya FADHILA)

2. Pale tunaposifiwa na watu tunawapenda na kuwakubali zaidi na hivyo kushawishika nao. (Nyenzo ya KUPENDA)

3. Pale tunapokuwa njia panda na hatujui nini cha kufanya, tunaangalia kinachofanywa na wengi na kuona ndiyo sahihi. (Nyenzo ya MKUMBO)

4. Pale mtu mwenye utaalamu kwenye eneo fulani anapotuambia nini cha kufanya, tunafuata hicho, kwa sababu tunajua wanajua zaidi yetu. (Nyenzo ya MAMLAKA).

5. Pale kitu kinapokuwa kinapatikana ka uchache, tunasukumwa kuchukua hatua kwa haraka ili tusikikose. (Nyenzo ya UHABA)

6. Pale tunapoahidi kufanya kitu, tunaendelea kukifanya ili tuaminike kwenye ahadi zetu. (Nyenzo ya MSIMAMO)

7. Tunawasikiliza zaidi wale ambao tupo nao pamoja kuliko ambao hatupo nao pamoja. (Nyenzo ya UMOJA).

Kwa sababu sisi sote tutaendelea kutegemea hizi nyenzo za ushawishi, mwandishi anatuasa tuzilinde. Tuzilinde kwa kuwazuia wale ambao wanazitumia nyenzo hiki kujinufaisha kama ambavyo tumeona kwenye kila nyenzo.

Kwa kuwa tutaendelea kutumia hizi njia za mkato kufanya sehemu kubwa ya maamuzi yetu, ni wajibu wetu kuzilinda zisitumike na wale wenye hila mbaya. Kwa njia hiyo tutaweza kufanya maamuzi bora bila ya kutumia muda mrefu na kuhitaji kufanya kazi kubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala kuhusu haya yaliyoshirikishwa hapa. Karibu ujifunze kwa kina kwenye kipindi ambacho kipo hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.