3393; Kukata tamaa mapema.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kinachofanya watu wengi washindwe siyo kwa sababu hawana uwezo wa kupata mafanikio makubwa.
Wala siyo kwa sababu mafanikio wanayotaka hayawezekani.
Bali ni kwa sababu watu wanakata tamaa mapema.
Wanakosa subira na uvumilivu wa kuendelea mpaka kupata matokeo makubwa wanayoyataka.

Sehemu kubwa ya matokeo ambayo watu wanayataka huwa inaletwa na muda.
Baada ya mtu kufanya yale anayopaswa kufanya, kinachofuata ni kuweka muda wa kutosha kusubiri matokeo yaweze kujijenga kwa ukubwa ambao mtu anataka.

Ili uweze kuwa na subira na uvumilivu wa kuendelea na kitu mpaka kupata matokeo makubwa, mambo mawili yanahitajika.

Jambo la kwanza ni kuwa na matarajio sahihi. Matarajio unayokuwa nayo yanaathiri sana mwenendo wako.
Unapokuwa na matarajio makubwa na ya haraka, unaishia kukatishwa tamaa na matokeo madogo na ya kuchelewa yanayokuja.
Unapaswa kuwa na matarajio sahihi, ukijua matokeo unayotaka yatachukua muda kutokea. Hilo litakuzuia usikate tamaa mapema.

Jambo la pili ni kuwa na imani thabiti na isiyoyumbishwa na chochote.
Pale mambo yanapokuwa magumu, na lazima utapitia hali hiyo kwenye safari yako ya mafanikio, kitu kitakachokuwezesha kuendelea ni imani uliyonayo.
Kama una amini, bila ya shaka yoyote ile kwamba utapata mafanikio makubwa unayoyataka, hilo litakupa nguvu ya kuendelea na hatimaye kupata ushindi.
Kama huna kiwango hicho cha imani juu yako mwenyewe na kwenye mafanikio unayoyataka, kama una mashaka yoyote kuhusu mafanikio unayoyataka, utaishia kukata tamaa haraka sana.

Mwongozo rahisi kwako kufuata ili kupata mafanikio unayoyataka kwa uhakika bila ya kukata tamaa.

1. Jua kwa hakika kile unachotaka, usibahatishe, eleza kabisa mafanikio unayotaka ni yapi na yanapimikaje.

2. Jua gharama unazopaswa kulipa ili kuyapata mafanikio hayo makubwa unayoyataka.

3. Lipa gharama hizo kupitia kuwa na mchakato wa utekelezaji kwenye kulipa gharama za mafanikio unayoyataka.

4. Jifunze kusubiri. Baada ya kufanya yale yaliyo sahihi, unapaswa kuwa na subira ili matokeo makubwa unayoyataka yajitengeneze. Wakati unasubiri unaendelea na mchakato bila kuacha.

5. Upende mchakato na siyo matokeo. Kama unasubiri matokeo ndiyo uyafurahie utakata tamaa mapema. Unapaswa kuupenda na kuufurahia mchakato wako. Huo ndiyo upo ndani ya uwezo wako wa kuathiri.
Kwa kuupenda mchakato utaweza kwenda nao kwa muda mrefu zaidi.

Kwa kufuata huo mwongozo, matokeo makubwa yatakuja kwa uhakika, kwa wakati wake yenyewe.
Umejifunza yote unayohitaji ili kupata mafanikio makubwa kwa uhakika, yaweke kwenye matendo ili kupata mafanikio hayo unayoyataka, hata kama mwanzo mambo yataonekana ni magumu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda, Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe