Habari Matajiri Wawekezaji,

Kuwa na mipango ya uwekezaji ni kitu ambacho kila mtu anafanya. Lakini kufuata mipango hiyo kwa msimamo bila kuacha ni kitu ambacho wengi wamekuwa hawakifanyi. Matokeo yake ni kunakuwa na watu wengi wanaoanza uwekezaji, lakini wachache sana wanaoendelea na uwekezaji mpaka kupata manufaa.

Tamaa inavyopelekea kupoteza.

Tumekuwa tunaona watu wengi wakiingia kwenye uwekezaji usio sahihi kwa kusukumwa na tamaa. Michezo mingi ya upatu na utapeli, huwa inawaonyesha watu kwamba wakifanya uwekezaji, kunakuwa na ukuaji mkubwa, wa haraka na uhakika. Wanaahidiwa wakipanda kiasi fulani cha uwekezaji, wataweza kuvuna mpaka mara mbili. Wale wanaowahi kwenye hiyo michezo wanapata kweli, lakini lengo ni kuwavutia wengine wengi ambao huwa wanaishia kupoteza.

Pia wapo wengi ambao wakilinganisha marejesho wanayopata kwenye uwekezaji sahihi na ambayo wangeweza kuyapata kwa njia nyingine kama kufanya biashara, wanaona kwenye uwekezaji wanapoteza. Kwa mfano kama mtu kwenye uwekezaji anapata marejesho ya asilimia 10 kwa mwaka, wakati kwenye biashara anaweza kupata zaidi ya asilimia 30, anaweza kuona kuwekeza ni kupoteza na bora aweke fedha zake zote kwenye biashara. Kwa hesabu za nadharia inaweza kuonekana ni sawa, lakini inapokuja kwenye uhalisia mambo huwa ni tofauti. Biashara huwa zina hatari kubwa ya kupata hasara kuliko uwekezaji.

Utulivu ni kuwa na matarajio madogo.

Ili kuhakikisha tunapata utulivu kwenye uwekezaji na kuweza kwenda na mipango sahihi ya uwekezaji tunapaswa kupunguza matarajio tunayokuwa nayo.

Kuwa na matarajio makubwa ni kitu kizuri, kwa sababu yanatusukuma kuchukua hatua. Lakini kwa sababu hatuna udhibiti kwenye matokeo tunayoyapata, pale yanapokuwa chini sana kulinganisha na matarajio, inakuwa rahisi kukata tamaa. Kiwango cha furaha na utulivu wa mtu kinapimwa kwa kanuni ya UHALISIA/MATARAJIO, yaani uhalisia gawa kwa matarajio. Kama uhalisia ni mkubwa kuliko matarajio, unakuwa na utulivu na furaha, lakini kama matarajio yanakuwa makubwa sana kuliko uhalisia, unaishia kukosa utulivu na kukata tamaa.

Unachohitaji wewe ni kukaa kwenye mpango wako sahihi wa uwekezaji kwa muda mrefu zaidi. Kwa sababu faida kubwa ya uwekezaji inatokana na muda kuliko kitu kingine chochote. Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU, muda wa chini ni miaka 10 ya kuwekeza kwa msimamo bila kuacha. Ukianza na matarajio makubwa, halafu uhalisia ukawa tofauti na hayo matarajio, utakata tamaa haraka na kuacha.

Kuwa na matarajio madogo kunapunguza nafasi ya wewe kutapeliwa na michezo iliyojificha nyuma ya uwekezaji. Uwekezaji sahihi huwa hauna marejesho makubwa na ya kutisha. Mtu anapokuambia ukiwekeza mahali fulani unakuza mtaji wako mara mbili ndani ya muda mfupi, tambua hapo kuna utapeli. Wala hata usijiulize mara mbili kwamba labda inaweza kuwa sahihi. Kama ni nzuri sana kuwa kweli, basi jua siyo kweli. Unaweza kuvuka kikwazo hicho kama huna matarajio makubwa kwenye uwekezaji unaofanya. Ukishakuwa na matarajio makubwa unaingiwa na tamaa na hatimaye kuwekeza, matokeo yake ni kupoteza, siyo tu mtaji ulioweka, bali hata muda na sifa. Maana kwa kuwekeza maeneo yasiyo sahihi na ambayo yanakufanya uwashawishi wengine nao wawekeze inakuharibia sifa yako.

SOMA; Sheria 10 Za Kujenga Utajiri Mkubwa Kupitia Uwekezaji Mdogo Mdogo.  

Matarajio na mabadiliko ya uchumi.

Kuwa na matarajio madogo kunakuwezesha kuendelea na uwekezaji hata pale marejesho yanapopungua sana kulingana na mabadiliko ya kiuchumi. Katika kipindi cha muda mrefu, uchumi huwa unapitia vipindi tofauti. Kuna wakati uchumi unakuwa mzuri, ambapo marejesho ya uwekezaji yanakuwa makubwa, hapo ndipo wengi husukumwa kuwekeza. Na kuna wakati uchumi unakuwa mbaya, ambapo marejesho ya uwekezaji yanakuwa madogo na hapo wengi husukumwa kuuza. Wawekezaji wanaonufaika siyo wanaonunua kwa wingi wakati uchumi ni mzuri na kuuza kwa wingi wakati uchumi ni mbaya. Badala yake ni wale wanaoendelea kuwekeza kwa mpango wao katika nyakati zote.

Kitu pekee kitakachokupa ujasiri wa kuendelea kuwekeza wakati kila mtu anauza uwekezaji ni kuwa na matarajio madogo. Wengi wanaokimbilia kuuza ni kwa sababu walitarajia marejesho makubwa kwa haraka. Wewe huangalii marejesho ya muda mfupi, bali ya muda mrefu na huna matarajio makubwa bali madogo. Kwa njia hiyo unaweza kuendelea na uwekezaji wako bila ya kutetereka na mabadiliko ya kiuchumi.

Ili kuweza kuwa na matarajio madogo, unapaswa pia kuwa unafanya uwekezaji mdogo mdogo kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha. Ukichukua fedha nyingi na kuziwekeza kwa mara moja, hutaweza kutulia pale unapoona kuna hasara inaweza kutokea. Lakini kama umekuwa unawekeza kiasi kidogo kidogo, huumizwi na hasara, maana ni fedha ambazo huenda ungekuwa umezitumia na hunazo tena. Hapa ndipo programu yetu ya NGUVU YA BUKU inapopata nguvu, kwa sababu kiasi tunachowekeza ni ambacho kama tusingewekeza basi tungekuwa tumekitumia, hivyo hatari ya hasara haituumizi sana.

Kufurahia marejesho yoyote.

Moja ya ushauri ambao umekuwa unatolewa kwenye uwekezaji ni kuwekeza kiasi ambacho upo tayari kukipoteza bila ya kuumizwa sana. Hicho ni kiwango cha juu kabisa cha kuwa na matarajio madogo. Yaani hapa unakuwa huna matarajio yoyote yale, kitu kinachofanya furaha kwako iwe kubwa hata kama utapata matokeo madogo kiasi gani.

Pale unapokuwa tayari kupoteza, chochote unachopata unakifurahia, kwa sababu hukutarajia kabisa. Matokeo yoyote unayoyapata hukuwa unayatarajia hivyo unayafurahia. Na hata unapopitia vipindi vya kupoteza, hutaumizwa sana kwa sababu tayari ulishategemea kupoteza. Hilo linakuwezesha kudumu kwenye uwekezaji kwa muda mrefu na kunufaika kuliko ungekuwa na matarajio makubwa.

Mrejesho wa somo.

Karibu kwenye mrejesho wa somo, ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali haya;

1. Eleza kwa ufupi uhusiano wa UTULIVU, MATARAJIO na UHALISIA. Nini cha kufanya ili uweze kuwa na utulivu mkubwa zaidi kwenye uwekezaji?

2. Unawezaje kutumia matarajio madogo kuvuka vipindi tofauti vya uchumi huku ukiendelea kuwekeza kwa msimamo bila kuacha?

3. Kwa nini kuwekeza kidogo kidogo kwa muda mrefu kunakupa utulivu mkubwa kuliko kuwekeza kwa ukubwa mara chache? Unahakikishaje unaendelea na uwekezaji mdogo mdogo ili uwe na utulivu mkubwa?

4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili au programu ya NGUVU YA BUKU.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.