Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli inayosema; Mipango siyo matumizi.

Hii ina maana kwamba, yale unayopanga na yanayokuja kutokea ni tofauti kabisa.

Huwa wanasema kupanga ni muhimu, lakini mipango haina maana.

Unahitaji kupanga ili ujue uko wapi, unataka kufika wapi na namna gani ya kufika.

Lakini ukishaweka mipango, mambo usiyotegemea huwa yanatokea na kuvuruga mipango yako.

Hatua gani ambazo mtu anachukua baada ya mipango yake kuvurugika ndiyo inaamua kama atafanikiwa au la.

Kwa walio wengi, ambao pia ndiyo wanaoshindwa, pale wanapokutana na vikwazo, huwa wanaona ndiyo mwisho wa safari.

Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wamepata maumivu makali sana na hawakuwa wameyategemea.

Kwa bahati mbaya sana, maumivu ya mara ya kwanza huwa ni makali sana. Kushindwa kwa mara ya kwanza huwa kunauma sana. Na changamoto za mara ya kwanza huwa zinakuwa ni ngumu sana.

Wengi wanaona ugumu huo wa mara ya kwanza ndiyo utakuwa hivyo milele, na hivyo kuishia kukata tamaa.

Ambacho wanashindwa kujua ni kwamba kama wakiendelea, mambo hayatakuwa magumu au kuumiza kama mwanzo. Maumivu na changamoto vitaendelea kuwepo, lakini havitaumiza kama mwanzoni.

Hivyo wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha unaendelea na safari yako ya mafanikio licha ya yoyote unayokuwa unakabiliana nayo.

Unachotaka wewe ni kuendelea kusonga mbele, ukijua kadiri unavyokwenda, mambo yatakuwa mepesi zaidi.

Hiyo ndiyo njia wanayochukua wale wanaojenga mafanikio makubwa na kudumu nayo. Siyo kwamba hawayapati maumivu, bali wameyazoea kiasi kwamba hayawaumizi tena kama mwanzo.

Uzuri wetu binadamu ni huwa tunaweza kuzoea kitu chochote.

Vitu vingi ambavyo huwa tunahofia vikitokea itakuwaje, huwa vinatokea na maisha yanaendelea.

Maisha hayajawahi kukwama kwa namna ambavyo tulikuwa tunahofia yatakwama.

Kwani mara zote huwa kuna mlango unaofunguka na kutuwezesha kutoka popote tunapokuwa tumekwama.

Ndiyo maana ni muhimu sana kuhakikisha tunaendelea na safari yetu ya mafanikio bila ya kujali tunakabiliana na nini.

Kwa sababu mengi tunayokabiliana nayo ni kwa muda tu, tusipoyakimbia, yatakimbia na kutuacha sisi tukiwa na mafanikio makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekufafanulia vizuri zaidi kwa nini hupaswi kukata tamaa pale unapokutana na maumivu ya mara ya kwanza. Karibu ujifunze.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.