Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake,
Lakini ni wachache sana ambao wanayapata mafanikio hayo kwa uhakika.
Wengi wanabaki kuwa na maisha duni na ya chini, licha ya kutaka mafanikio makubwa.
Wengine pia wanaweka juhudi kubwa, lakini bado hawayapati mafanikio.
Swali ambalo limekuwa kitendawili kwa wengi ni nini kinapelekea hali hii?
Maisha ya Michael Jordan yanatupa funzo kubwa sana kuhusu kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Jina la Michael Jordan ni maarufu kwa wengi kutokana na mafanikio aliyoyapata kwenye mpira wa kikapu.
Ni mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea kwenye mpira wa kikapu.
Aliiwezesha timu yake ya Chicago Bulls kushinda mataji sita, yote kwa mchango wake mkubwa.
Alikuwa anajipa wajibu wa kuisukuma timu nzima mpaka kupata ushindi mkubwa.
Vitu viwili muhimu tunavyojifunza kwa Michael Jordan ambavyo tukivitumia, tutaweza kupata mafanikio makubwa.
MOJA; KUWA NA NJAA KALI YA USHINDI.
Michael Jordan anaelezwa kwa mtu ambaye ana njaa ya ushindi tangu akiwa mtoto mdogo.
Kwenye kila jambo alikuwa na msukumo wa kuwashinda wengine na kuwa namba moja.
Hata kwenye mambo ya kawaida kabisa, ambayo hayahitaji ushindi, yeye aliweka hali ya ushindi.
Hilo ndiyo lilimwezesha kupata mafanikio makubwa, kwani hakutaka apitwe na mtu mwingine yeyote kwenye mchezo wa mpira wa kikapu.
Kila mara alihakikisha anafanya zaidi ya wengine ili kuwashinda.
Unahitaji kuwa na njaa kali ya ushindi ndani yako, ambapo hukubali kabisa kushindwa kwenye maisha.
Pale unapoweka malengo na mipango yoyote ile, ona aibu kutokukamilisha kama ulivyopanga.
Kwa chochote kikubwa unachotaka kufikia, watangazie wengine wazi kabisa kwamba unakwenda kukipata kwa uhakika.
Kama watu watakubeza kwamba huwezi kukipata, pata hasira ya kutaka kuwaonyesha kwamba inawezekana kabisa.
Weka juhudi kubwa kwa msukumo wa kuwaonyesha wengine kwamba unaweza kupata kile unachotaka.
Kwa kuwa na msukumo mkubwa wa kupata ushindi, utaweza kuvuka vikwazo na changamoto mbalimbali kitu kitakachofanya mafanikio yawe ya uhakika kwako.
SOMA; Kinachofanya maisha yako yakose maana ni hiki.
MBILI; WEKA JUHUDI KUBWA HUKU UKIBORESHA.
Michael Jordan alikataliwa kwenye timu alipofanya maombi kwa mara ya kwanza, akionekana hataweza.
Kwenye maombi mengine alikubaliwa, lakini hakuwa anapangwa kwenye kikosi cha kwanza.
Badala yake alikuwa akifanya kazi ya kuwabebea wachezaji wengine maji.
Alichukuliaje hali hiyo?
Hapo ndipo patamu zaidi, kwani hakukubali hali hiyo imkatishe tamaa.
Badala yake aliweka juhudi kubwa zaidi kwenye kufanya mazoezi na kuwa bora zaidi.
Alikuwa wa kwanza kufika kwenye mazoezi na wa mwisho kuondoka.
Hivyo alikuwa akiweka juhudi kubwa kwenye mazoezi kuliko wachezaji wengine wote.
Na juhudi hizo zilianza kulipwa, hatimaye anaanza kupangwa kwenye kikosi cha kwanza na kuonyesha uwezo wake mkubwa.
Unaweza kuianza safari yako kwa malengo na mipango mikubwa sana.
Lakini kitu cha kwanza ni dunia itakukataa, itakukatalia mengi unayokuwa unayataka.
Utakabilianaje na hali ya kukataliwa ndiyo itaamua kama utafanikiwa au la.
Kwa wanaoshindwa, wanapokutana na vikwazo, huwa wanaona ndiyo mwisho wa safari yao.
Kwa wanaofanikiwa, huwa wanaweka juhudi zaidi, huku wakiboresha ili kupata matokeo wanayoyataka.
Wewe kuwa kwenye kundi la wanaofanikiwa, kwa kuendelea kuweka juhudi kubwa na kwa ubora wa hali ya juu pale unapokutana na magumu na changamoto.
Kama utaweza kuvuka kila aina ya ugumu unaokutana nao kwa kuweka juhudi kubwa zaidi, hakuna chochote kitakachokuzuia kufanikiwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu haya tunayojifunza kutoka kwa Michael Jordan na jinsi ya kuyaweka kwenye maisha yetu ili tuweze kufanya makubwa.
Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.