Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna aina mbili za utajiri, ambapo ni utajiri wa fedha (rich) na utajiri wa mali (wealth).

Utajiri wa fedha huwa unatokana na kipato cha moja kwa moja ambacho mtu anaingiza. Yule anayelipwa zaidi au kupata faida kubwa zaidi, ataonekana kuwa na utajiri huo.

Utajiri wa mali huwa unatokana na uwekezaji ambao mtu amefanya. Kupitia uwekezaji, mtu anakuwa na uwezo wa kuingiza kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja.

Tatizo kubwa kwenye kujenga utajiri ni watu wamekuwa hawajui hizi tofauti na hivyo kuishia kufanya maamuzi ambayo yanawakwamisha kupata utajiri.

Mwandishi Morgan Housel kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF MONEY anatufundisha utajiri ni kile kisichoonekana.

Kwenye kitabu hicho, Housel ametupa masomo 20 ya msingi kuhusu fedha, utajiri, tamaa na furaha. Kupitia masomo hayo tunapata nafasi ya kujifunza mambo ya kuzingatia ili kufanya maamuzi bora kifedha kwetu na kujenga utajiri na furaha.

Kwenye makala ziliyopita, tumepata masomo nane kati ya hayo 20. Kwenye makala hii tunakwenda kupata masomo mengine manne na hatua za kuchukua ili tujenge na kudumu kwenye utajiri.

9. Utajiri Ni Kile Kisichoonekana.

Huwa tunawahukumu watu kwa mwonekano wa nje. Hivyo inapokuja kwenye utajiri, imezoeleka matajiri ni wale wenye matumizi makubwa. Lakini hiyo siyo sahihi, unachoona kwa nje siyo utajiri, bali ni matumizi.

Utajiri halisi ni kile kisichoonekana. Kwa kumwangalia mtu huwezi kujua ana akiba kiasi gani au uwekezaji kiasi gani. Hivyo ndivyo vitu vinavyoamua utajiri wa watu, ambavyo huwa havionekani.

Hatua ya kuchukua;

Katika kujijengea utajiri, acha kuhangaika na vitu vinavyoonekana kwa nje na kazana na vile visivyoonekana. Weka akiba na wekeza ili kukuza thamani ya utajiri wako badala ya kuwa na matumizi makubwa yanayopunguza utajiri wako.

10. Weka Akiba.

Kila mtu anajua umuhimu wa kuweka akiba, lakini ni watu wachache sana ambao wanaweka akiba kwa uhakika. Watu wengi huwa hawaweki akiba, hivyo kuweka akiba ni kitu ambacho kinapaswa kuendelea kufundishwa na kusisitizwa mara zote.

Kwenye kuweka akiba huwa kuna makundi matatu ya watu; moja ni wanaoweka akiba, mbili ni wanaodhani hawawezi kuweka akiba na tatu ni wanaodhani hawahitaji kuweka akiba.

Kundi lililo sahihi kwenye kujenga utajiri ni la wale wanaoweka akiba. Haijalishi unaingiza kipato kiasi gani, utajiri wako utatokana na kiasi unachoweka akiba na kuwekeza.

Ili uweze kuweka akiba, ni lazima uweze kudhibiti matumizi yako. Kwa bahati mbaya sana, matumizi huwa yanaongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka. Hivyo kama mtu hutaweza kujidhibiti ili kufanya matumizi ya msingi pekee na kiasi kikubwa kwenda kwenye akiba, hutaweza kujenga utajiri mkubwa.

Hatua ya kuchukua;

Kwa kila kipato unachoingiza, sehemu kubwa weka akiba. Kwa kila kipato cha ziada unachopata, ambacho hukuwa na mpango nacho, chote peleka kwenye akiba. Kadiri unavyoweka akiba kiasi kikubwa ndivyo unavyokuwa na nguvu ya kuwekeza na pia kuwa huru kifedha.

11. Manufaa Ni Bora Kuliko Mantiki.

Mafunzo na ushauri wa fedha na uwekezaji huwa unahusisha ukokotoaji mkubwa na unaoleta mpango mzuri kimantiki. Lakini kwenye kutekeleza mpango huo inakuwa ni shida kubwa. Hiyo ni kwa sababu sisi binadamu siyo viumbe wa kimantiki, bali ni viumbe wa kihisia. Tunafanya maamuzi yetu kwa kusukumwa na hisia.

Ndiyo maana licha ya kuwepo kwa miongozo mingi na sahihi ya fedha na uwekezaji, bado maamuzi ambayo watu wanafanya kwenye fedha na uwekezaji huwa ni ya tofauti.

Hilo halipaswi kutuumiza, badala yake unapaswa kulitumia kama mwongozo sahihi kwako. Unapaswa kufanya maamuzi ambayo yana manufaa kwako na siyo yenye mantiki. Kwa sababu wewe ndiye utakayeishi na maamuzi hayo.

Vitu vikubwa viwili vya kukuongoza kwenye maamuzi yako ya manufaa ni kuhakikisha unakaa kwenye kitu kwa muda mrefu zaidi, kwa sababu mafanikio yanakuwa ya uhakika kwa muda mrefu. Na pia unapaswa kupunguza majuto ya baadaye, yaani ufanye yale ambayo hayatakupa majuto baadaye.

Hatua ya kuchukua;

Usiumie pale maamuzi yako yanapokuwa siyo ya mantiki, wewe ni binadamu mwenye hisia. Tumia hisia zako kufanya maamuzi yenye manufaa kwako, ambayo yatakuwezesha kudumu kwa muda mrefu na kukupunguzia majuto.

12. Mshangao.

Huwa tunapenda kutumia historia ya mambo ya nyuma kufanya maamuzi ya mambo yajayo. Lakini historia ya nyuma haileti uhakika wa mambo yajayo.

Mambo ambayo hayajawahi kutokea huwa yanatokea na pale yanapotokea yanawapa watu mshangao mkubwa. Kwa sababu watu huwa tunapenda uhakika na tunatumia mazoea ya nyuma kuamua yajayo, pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyozoea tunashangaa.

Kwenye fedha na uwekezaji mshangao huwa ni mkubwa kwa sababu hisia za watu zinaleta athari kubwa. Fedha na uwekezaji ndiyo eneo pekee ambalo kila mtu anakuwa tofauti na bado wote wanakuwa sahihi.

Hatua ya kuchukua;

Katika kuweka mipango yako ya fedha na uwekezaji, jua kwamba DUNIA ITAKUSHANGAZA. Mambo ambayo hayajawahi kutokea yana nafasi ya kutokea. Na kwa bahati mbaya sana, hujui nini kitatokea na wakati gani kitatokea. Muhimu ni kuhakikisha chochote kinachotokea, unanufaika nacho.

Hapa tumepata masomo mengine manne ya utajiri na furaha kutoka kitabu THE PSYCHOLOGY OF MONEY kilichoandikwa na Morgan Housel. Masomo yapo 20, kwenye makala inayofuata tutaendelea kuyapata masomo haya. Usikose.

Hapo chini kuna mjadala mzuri ambao tumekuwa nao juu ya masomo haya kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Fungua kipindi uweze kujifunza kutoka kwa mifano na shuhuda za wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.