3399; Kuchukulia poa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Matokeo ambayo tunayapata kwenye kila eneo la maisha yetu, huwa yanategemea sana umakini na uzito ambao tunaweka kwenye eneo hilo.

Lakini kwa bahati mbaya sana, tumekuwa tunachukulia poa maeneo mengi ya maisha yetu na matokeo yake ni kukosa mafanikio makubwa tunayoyataka.

Hata pale unapokuja kushtuka kwamba eneo limechukuliwa poa, unakuwa huna hata cha kufanya ili kubadili hali husika.
Hivyo suluhisho ni kuhakikisha umakini na uzito unawekwa kwenye kitu tangu awali.

Pale kitu kinapofanya kazi, huwa tunakichukulia poa. Tunakimbilia kuhangaika na vitu vingine ambavyo hata havifanyi kazi.
Matokeo yake ni kushindwa kupata manufaa makubwa kwenye kile kinachofanya kazi.

Ili kunufaika kwa kiasi kikubwa na kile kinachofanya kazi, tunapaswa kuweka umakini na uzito wetu kwenye kitu kinachofanya kazi.
Kile kinachofanya kazi tunapaswa kukipa rasilimali nyingi zaidi ili kiweze kuzalisha matokeo makubwa zaidi.
Hakuna kitu ambacho kitakuwa na uzalishaji mkubwa kwa kujiendea chenyewe bila ya juhudi kubwa kuwekwa juu yake.

Pale ambapo kitu hakifanyi kazi, huwa tunachukulia poa vikwazo vinavyokuwa vimezuia.
Huwa ni rahisi kuona tukichukua hatua ndogo na chache tutaweza kutoka pale tulipokwama.

Ni mpaka pale tunapochukua hatua tulizodhani zingetosha kutatua jambo ndiyo tunashangazwa na jinsi ambavyo hazifui dafu.
Hapo ndipo tunapogundua kwamba juhudi kubwa zaidi zinapaswa kuwekwa ili kutoka kwenye hali ambayo imekwamisha.

Pale unapokuwa hupati matokeo uliyokuwa unategemea kupata, jua tatizo ni kubwa kuliko unavyodhani.
Hivyo likabili tatizo kwa uzito unaostahili ili kuhakikisha unapata matokeo unayoyataka.

Somo kubwa tunaloondoka nalo hapa ni tusichukulie chochote poa.
Umakini, uzingatiaji na uzito mkubwa unapaswa kuwekwa kwenye kila tunachofanya ili tuweze kupata matokeo makubwa tunayoyataka.
Matokeo yoyote makubwa, yanahitaji kazi isiyokuwa ya kawaida iwekwe.

Ni bora uweke juhudi kubwa mahali panapohitahi juhudi ndogo kuliko kuweka juhudi ndogo mahali panahitaji juhudi kubwa.
Mara zote kaa kwenye upande wa kukuwezesha kupata matokeo makubwa na bora hata kwa mambo madogo.
Hilo litakuwezesha kuweka juhudi kubwa mara zote na kuzalisha matokeo ya tofauti.

Usichukulie kitu chochote poa, undani wa vitu huwa ni tofauti sana na jinsi kinavyoonekana kwa nje.
Kipe kila kitu uzito ambao kinastahili na matokeo yako yatakuwa bora.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe