Rafiki yangu mpendwa,
Furaha kwenye maisha imekuwa kitendawili ambacho watu wengi wameshindwa kukitegua.
Kila mtu anataka kuwa na furaha kwenye maisha yake.
Lakini kadiri mtu anavyokuwa anataka kuipata furaha, ndivyo anavyozidi kuikosa.
Furaha imekuwa kama kipepeo kizuri ambacho unakiona juu ya ua, lakini unapokisogelea, kinaruka. Na pale unapojaribu kukikimbiza ili ukikamate, ndiyo kinazidi kupotea.
Wengi kwa kushindwa kutatua kitendawili cha furaha, wamekuwa wanakubali kuishi maisha ambayo hayana furaha. Hilo limekuwa linachangia ubora wa maisha ya wengi kuwa wa chini sana.

Kinachofanya wengi wasipate furaha kwenye maisha ni kudhani kwamba furaha italetwa na matokeo wanayoyataka. Kwa mfano mtu anakazana apate kitu fulani, akidhani akishakipata basi atakuwa na furaha.
Anakazana sana kupata kitu hicho, na baada ya kukipata, anapata raha ya muda mfupi tu. Baada ya hapo maisha yanarudi kama kawaida na kujikuta wanataka kupata kingine kikubwa zaidi ili wapate furaha zaidi.
Tukitumia mfano rahisi, ni sawa na mtu ambaye anatembea kwa miguu anasema akipata baiskeli atakuwa na furaha. Anakazana ili apate baiskeli, kweli siku ya kwanza anaifurahia. Lakini kadiri siku zinavyokwenda ile raha inaisha na kuanza kujiambia akipata pikipiki atafurahia zaidi. Anakazana kupata pikipiki, akiipata anapata raha kidogo, lakini anagundua akiwa na gari ndiyo atapata furaha zaidi.
Mtu anakwenda na maisha hivyo, mpaka anaondoka hapa duniani hajawahi kuwa na furaha inayodumu. Furaha yake inakuwa ni ya vipindi vya muda mfupi tu.
Hivyo sivyo maisha yanavyopaswa kwenda. Furaha haitokani na matokeo ambayo mtu anayapata, bali inatokana na mchakato mzima ambao mtu anakuwa nao kwenye maisha.
Yaani unapaswa kuwa na furaha kwenye maisha yako ya kila siku na siyo kusubiri mpaka matokeo ya mwisho. Maana yake hapa unapaswa kuifurahia safari nzima na siyo mwisho wa safari.
Tunaweza kuliona hilo kwenye safari tunazokuwa nazo kwenye maisha. Ukiwa safarini, unatamani sana kufika mwisho wa safari. Lakini unapokuja kutafakari, unagundua kilichokuwa muhimu kwenye safari yako siyo huo mwisho, bali safari nzima.
Ukiwa shuleni unatamani sana siku ya kumaliza shule ukiona utafurahia. Lakini baada ya kumaliza shule, unachokumbuka siyo ile siku ya kuhitimu, bali zile siku ulizokuwa shuleni.
Hayo yote yanatuonyesha jinsi ambavyo chanzo cha furaha hakipaswi kuwa matokeo ya mwisho, bali kinapaswa kuwa mchakato mzima. Furaha yako kwenye maisha haipaswi kutegemea nini unapata, bali itegemee jinsi unavyoyaishi maisha yako ya kila siku.
Matokeo tunayotegemea kuyapata kwenye maisha yetu yapo nje kabisa ya uwezo wetu. Tunaweza kuweka juhudi kubwa, lakini bado matokeo yakaja tofauti na tulivyotegemea. Hivyo kama utaiweka furaha yako kwenye matokeo, itayumbishwa sana, kwa sababu huna uhakika nayo.
Lakini juhudi unazoweka kwenye yale unayofanya zipo ndani ya uwezo wako. Ni wewe ndiye unayepanga na kufanya. Kama utaiweka furaha yako kwenye kufanya, utakuwa nayo mara zote maana ni kitu unachoweza kukidhibiti.
SOMA; Jinsi Ya Kuboresha Furaha Na Mahusiano Yako
Furaha na mafanikio vimekuwa vinategemeana, lakini kwa mpangilio ambao ni tofauti na wengi wanavyodhani.
Wengi wanadhani wakishafanikiwa ndiyo watakuwa na furaha. Matokeo yake hawafanikiwi au hata wakifanikiwa furaha hawaipati, kwa sababu haidumu. Mpangilio sahihi ni unaanza na furaha ndiyo unafanikiwa. Yaani unatakiwa kuwa na furaha kwanza ndiyo uweze kupata mafanikio.
Falsafa ya Ustoa, moja ya falsafa za kale ambayo ina matumizi sana kwenye zama tunazoishi sasa inatupa mwongozo mzuri wa kuishi maisha yetu kwa furaha, bila ya kujali nini tunapitia au kupata.
Msingi wa Ustoa kwenye maisha ya furaha ni kwa mtu kuyaishi maisha yako kwa uhalisia wake. Kufanya kile ambacho mtu unapaswa kufanya na kukifanya kwa manufaa ya wengine.
Lakini pia furaha inachangiwa na mahusiano tunayokuwa nayo kwetu sisi wenyewe, imani yetu na watu wanaotuzunguka. Ukiangalia yote hayo, yanakuwa yanaanza na wewe mwenyewe.
Hivyo kwa Ustoa, ukitaka maisha ya furaha, lazima uweze kujidhibiti wewe mwenyewe, kuanzia fikra zako, hisia zako na matendo yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha mambo ya kuzingatia ili uweze kuwa na maisha ya furaha kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Huhitaji kitu chochote cha ziada kuyafurahia maisha, unahitaji kuwa na mtazamo wa tofauti tu.
Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini, uchukue hatua na kuwa na maisha ya furaha.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.