Rafiki yangu mpendwa,

Ulipozaliwa, kiashiria cha kwanza ambacho wakunga walikitumia kujua kama uko sawa ni kulia.

Swali ambalo wakunga huwa wanajiuliza na kuulizana pale mtoto anapozaliwa ni je amelia?

Na hata uwezo wa kiakili, unapimwa na uharaka wa kulia. Mtoto anayelia haraka anakuwa na uwezo mkubwa kuliko mtoto anayechelewa kulia.

Rafiki, sijui kama unaona hilo fumbo kubwa sana ambalo lipo nyuma ya maumivu.

Kwa nini siku ambayo ni bora kabisa kwako, siku ya kumbukumbu kubwa kwenye maisha yako, ambayo utaisherekea siku zote za maisha yako, uianze kwa kulia?

Kuna matukio mengi ambayo watu wanapitia kwenye maisha na kuwa na kumbukumbu nayo. Lakini tukio la kuzaliwa ndiyo ambalo ni muhimu kwa kila mtu na huwa halisahauliki.

Sasa kwa nini tukio hili muhimu kuliko yote lilianza na kilio?

Jibu ni moja rafiki yangu, ulikaribishwa kwenye uhalisia wa maisha. Na uhalisia wa maisha ni maumivu, kwa kipindi chote cha maisha.

Wakati upo tumboni kwa mama yako, ulikuwa unapata kila kitu bila ya kusumbuka. Hakukuwa na maumivu yoyote. Lakini zoezi zima la kuzaliwa na kukutana na dunia kwa mara ya kwanza, lilikuletea maumivu na ndiyo maana ulilia.

Lakini baada ya yale maumivu ya wakati wa kuzaliwa, maisha yaliendelea, ukayazoea maisha na kuishi maisha ya kawaida haikuwa maumivu tena kwako. Kuanzia hapo, kila kitu kipya kwenye maisha yako kimekuwa ni maumivu. Ulipopata njaa kwa mara ya kwanza, ulilia, kwa sababu njaa ni maumivu. Ulipojisaidia, ulilia, kwa sababu ni maumivu.

SOMA; Kataa Hisia Za Maumivu Na Maumivu Yataondoka Yenyewe

Rafiki, ukiangalia maisha ya utoto, ambayo wote tumepitia, yanaeleza vizuri ni kwa namna gani maisha yetu yote yataenda. Hasa kwenye eneo la maumivu. Kila hatua ya maisha yetu ina maumivu, ambayo hatuwezi kuyakwepa.

Kutoka ngazi moja ya maisha kwenda ngazi nyingine kuna maumivu. Na kadiri hatua unazopiga zinavyokuwa kubwa, ndivyo maumivu yanavyokuwa makubwa pia.

Sasa swali ni je tunawezaje kuyafurahia maisha kama wakati wote ni maumivu?

Jibu ni rahisi, hakuna maumivu yanayodumu milele. Kila maumivu unayokuwa unayapitia ni ya muda tu. Ni labda maumivu hayo yatapita, utayazoea na kuweza kuishi nayo au yatakuua.

Sehemu kubwa ya maumivu unayokutana nayo kwenye maisha ni ya mpito. Inakuwa ni swala la muda tu, maumivu hayo yanapotea kabisa. Mengine yanakutaka wewe uchukue hatua fulani ili kubadili kile kinachosababisha maumivu hayo. Unapokuwa na maumivu ya aina hii, chukua hatua ambazo ni sahihi na jipe muda, yataondoka.

Sehemu ndogo ya maumivu unayokutana nayo kwenye maisha ni ambayo hayawezi kupita. Lakini unaweza kuyavumilia na maisha yakaendelea licha ya kuwa na maumivu hayo. Haya ni maumivu yanayotokana na mabadiliko ambayo ni ya kudumu. Mfano mtu anapopata ugonjwa sugu, ulemavu, kupoteza mtu wa karibu n.k. Matukio hayo huwezi kuyabadili, mwanzo yanakuwa na maumivu makali, lakini baadaye unayazoea na maisha yanaendelea. Pale unapokutana na maumivu ya aina hiyo, hakikisha unayakubali haraka ili maisha yaendelee. Usijiumize nayo sana kwa kujiuliza kwa nini yametokea, yameshatokea, ishi nayo.

Kwa nadra sana, unakutaka na maumivu ambayo hayana mwisho na hayazoeleki na hayo tunajua matokeo yake ni nini. Matokeo ya maumivu hayo huwa ni kifo. Hivyo nayo pia yanakuwa na mwisho, kwa sababu hutaendelea kuishi. Haya ni maumivu ambayo wale wanaofikia hatua za mwisho wa maisha yao huwa wanayapitia, hivyo utakapoyafikia ni kuyakubali na kushukuru kwa maisha ambayo uliweza kuwa nayo.

Rafiki, unaona wazi kabisa kwa nini hupaswi kukwamishwa na maumivu yoyote unayopitia kwenye maisha yako. Kwa sababu kwa vyovyote vile, kila maumivu yana mwisho wa kukusumbua. Yataisha yenyewe, utayazoea au utakufa.

Hilo linakupa wewe sababu ya kuhakikisha unayaishi maisha yako kwa ukamilifu wake na kutokuruhusu maumivu yoyote yale yakukwamishe. Hata kama unapitia maumivu kiasi gani, hakikisha unaendelea na safari yako, usikate tamaa wala kuishia njiani.

Kuacha kile unachofanya au unachotaka sana kwenye maisha kwa sababu ya maumivu, hakutasaidia chochote kwenye maumivu hayo. Badala yake kutazidisha maumivu, kwa sababu unakua hujapata hata kile ulichokuwa unataka na unajua kabisa umeacha.

Unakuwa na majuto kwamba kama ungefanya, huenda ungepata. Na majuto ndiyo yamekuwa yanaongeza maumivu kwa walio wengi. Ukiweza kupunguza majuto kwenye maisha yako, kwa kufanya yale unayojua unapaswa kufanya, utapunguza maumivu kwenye maisha yako.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ujifunze kwa kina dhana hii ya maumivu kuwa na mwisho ili uweze kuishi maisha yako kwa mafanikio makubwa bila ya kujali unapitia nini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.