Rafiki yangu mpendwa,
Huwa wanasema mipango siyo matumizi.
Hiyo ni kwa sababu kile unachopanga ni tofauti kabisa na kile kinachokuja kutokea.
Hali hiyo ya mipango kutofautiana na uhalisia huwa inawafanya baadhi ya watu kuona hakuna haja ya kupanga.
Lakini hilo siyo sahihi, kupanga ni muhimu sana, hata kama mipango haitaendana na uhalisia.
Hiyo ni kwa sababu zoezi la kupanga linakufanya ukielewe kitu kwa undani zaidi. Hata kama mipango haitaenda kama ulivyoweka, lile zoezi la kupanga lilikuwa na manufaa kwako.

Kwa kuwa mipango haiendani na uhalisia, kuhakikisha hukwami kwenye mipango unayoweka, unapaswa kuwa na mpango mwingine.
Mpango huo mwingine unaopaswa kuwa nao unaitwa MPANGO WA MPANGO KUTOKWENDA SAWA NA MPANGO.
Yaani pale unapoweka mipango yako, weka pia mipango pale ambapo mambo yataenda tofauti na mipango uliyoweka.
Kwa njia hiyo utakuwa na hatua za kuendelea nazo hata pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyopanga.
Mpango kwenye mpango ni zoezi muhimu kufanya ili kuhakikisha hukwamishwi na kitu chochote kile.
Kwa kuwa hatuna uhakika wa yale yajayo, lakini bado unalazimika kupanga, kuwa na mpango juu ya mpango wako ni hitaji muhimu kwenye maisha yako.
Wanaofanikiwa huwa hawakubali kitu chochote kiwakwamishe, hivyo huwa na maandalizi ya kutosha na yanayoweka nafasi ya mengi kuwakwamisha.
Wanaoshindwa huwa wanajiandaa kushindwa kwa kutokuwa na maandalizi ya kutosha, hasa kwenye maeneo ambayo yanaweza kuwakwamisha.
Wewe chagua kuwa upande wa wanaofanikiwa kwa kuhakikisha unakuwa na maandalizi sahihi yanayozingatia mipango kutokwenda sawa na mipango ili usikwame.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekupa ufafanuzi zaidi kuhusu kuweka mpango juu ya mpango kutokwenda na mpango. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili usikwamishwe na chochote.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.