Rafiki yangu mpendwa,

Kufanikiwa kwenye maisha huwa kunahitaji kiasi kwenye kila jambo.

Kwa bahati mbaya sana, kipimo cha kiasi ni kitu ambacho huwa hakiwezi kufundishwa.

Kwenye kila jambo huwa kuna kingo mbili, ambapo kila ukingo siyo sahihi.

Sahihi ni mahali fulani katikati ya kingo hizo mbili. Na mahali hapo hapalingani kwa watu wote.

Wachache wanaoweza kujua mahali hapo sahihi huwa wanafanikiwa sana. Wakati wanaishindwa kujua na hivyo kubaki kwenye kingo, huwa wanashindwa.

Kwenye mambo ambayo watu tunafanya, huwa kuna kingo mbili za MSIMAMO na MABADILIKO.

Ukingo wa MSIMAMO ni kuendelea na kitu bila ya kubadilika kabisa. Hii huwa inakuwa rahisi kutekeleza,  lakini inamweka mtu kwenye hatari ya kuachwa nyuma na mabadiliko ya lazima ambayo yanatokea.

Ukingo wa MABADILIKO ni kubadili kile ambacho mtu anafanya. Hii siyo rahisi kutekeleza kwa sababu wengi hawapendi mabadiliko, lakini kwa wale wanaotekeleza kupitiliza, hushindwa kujua kinachowakwamisha ni nini. Maana wanaweza kubadilika kabla hata kitu hakijapata nafasi ya kufanya kazi.

Swali utakalokuwa unajiuliza ni wakati gani wa kubaki na MSIMAMO na wakati gani wa KUBADILIKA?

Na kama tulivyoona hapo, hilo ni swali ambalo hakuna mtu yeyote anayeweza kukujibu isipokuwa wewe mwenyewe. Ni wewe ndiye unayejua kama uendelee au ubadilike.

Kwa bahati nzuri sana, ipo njia rahisi kwako kujibu swali hilo. Na njia hiyo inaanza na swali muhimu ambalo unapaswa kujiuliza na kujipa jibu sahihi kwako.

Swali hilo ni; KWA KUJUA HIKI NINACHOJUA SASA, KAMA NINGEKUWA NAANZA UPYA LEO, NINGERUDIA NILICHOFANYA?

Kama majibu ni NDIYO, basi endelea kufanya kwa msimamo, maana ndiyo kitu sahihi kwako.

Kama majibu ni HAPANA, basi acha kufanya mara moja, badilika na nenda kwenye kitu kingine, maana hicho siyo sahihi kwako.

Msingi wa swali hilo ni kwamba pale unapokuwa unaanza kitu, kuna vitu vingi unakuwa hujui. Hivyo maamuzi yoyote unayoyafanya ni kwa taarifa ambazo hazijakamilika.

Unapoanza kufanya kitu ndiyo unajua taarifa nyingi za ndani ambazo awali hukuwa unajua. Sasa kama licha ya kujua taarifa hizo bado unafurahia kufanya, unapaswa kuendelea.

Lakini kama kwa kujua taarifa hizo za ndani unajiona hukufanya maamuzi sahihi, ni wakati wa kubadilika. Maana hata ukae kwenye maamuzi hayo kwa muda mrefu kiasi gani, hayatakuwa na manufaa kwako. Kadiri unavyobadilika mapema, ndivyo unavyoacha kupoteza muda na maisha yako.

Hakuna haja ya kwenda mbio wakati haupo kwenye njia iliyo sahihi. Hivyo kila mara jiulize hilo swali na kujipa majibu sahihi. Swali hilo litakusaidia kubaki kwenye njia sahihi kwako mara zote.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua zaidi kuhusu swali hili la mabadiliko unalopaswa kujiuliza na kujipa majibu sahihi ili ujue kama unapaswa kubadilika au kubaki na msimamo. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili kujenga maisha ya mafanikio.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.