Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu ambavyo vimewapoteza watu wengi ni kuchanganya kipato na utajiri. Wengi wamekuwa wanadhani wakishakuwa na kipato kikubwa, basi tayari wana utajiri.

Hiyo ni kwa sababu wakati watu hao wanaingiza kipato hicho kikubwa, wanakuwa wanaweza kuendesha maisha yao kwa namna wanavyotaka. Hilo linawafanya wajisahau na kubweteka.

Mambo hubadilika pale kipato kikubwa kinapofika ukingoni, jambo ambalo hutokea kwa uhakika. Hapo sasa ndiyo watu wanagundua kwamba hawakuwa na utajiri. Wanashindwa kuyaendesha maisha yao, ambayo tayari yalikuwa ni ya gharama kubwa.

Tumekuwa tunaona hilo kwa wasanii, wachezaji na watu wengine ambao wanalipwa kiasi kikubwa. Kwa kulipwa kiasi kikubwa, wanakuwa na matumizi makubwa na hivyo kushindwa kujenga utajiri.

Kitu ambacho wengi hawajui ni kwamba utajiri huwa hautokei tu kwa sababu mtu una kipato. Bali utajiri huwa unajengwa, kwa juhudi kubwa.

Utajiri ni kazi kabisa iliyokamilika, ambayo mtu anapaswa kuweka juhudi kwenye kuifanya ili afanikiwe.

Na ili kujenga utajiri, mtu anapaswa kuwekeza muda, nguvu na fedha. Hakuna aliyeweza kujenga utajiri mkubwa na wa kudumu kwa kubahatisha tu. Uwekezaji ni lazima ufanyike kwa uhakika ndiyo utajiri uweze kutengenezwa.

SOMA; Kama unataka Kujenga Utajiri Mkubwa, Kuwa Bahili.

Waandishi wa kitabu cha THE MILLIONAIRE NEXT DOOR, katika kufanya utafiti kwa matajiri, waliona wazi jinsi ambavyo wote waliopata utajiri waliufanyia kazi.

Katika kuwauliza kuhusu malengo yao ya kifedha, matajiri walikuwa na vipaumbele vifuatavyo;

1. Kuwa wamefikia utajiri wakati wanastaafu, ili waweze kuyaendesha maisha yao bila tatizo.

2. Kuendelea kuongeza utajiri wao kupitia fursa mbalimbali wanazokutana nazo.

3. Kujenga utajiri kupitia ukuaji wa mtaji kwenye biashara na uwekezaji ambao wanafanya.

4. Kujenga utajiri wao wakati wanatunza thamani ya mali wanazokuwa wanamiliki.

Waliendelea kuona jinsi matajiri wanavyotenga muda na kuweka juhudi kwenye kupangilia fedha zao na kufuatilia utajiri wao. Wanakuwa na mipango kwa kila kipato, kuweka akiba na kuchagua uwekezaji sahihi kwao.

Siyo watu wa kufuata mkumbo kwenye matumizi au uwekezaji, bali ni watu wa kujifunza na kuchukua hatua sahihi kwao.

Uwekezaji mwingine ambao matajiri wamekuwa wanafanya na unawanufaisha ni kulipa gharama za kupata mafunzo na ushauri sahihi. Matajiri wanathamini sana elimu, kwa sababu wanajua mchango wake kwenye kujenga utajiri.

Lakini zaidi wanaamini kwenye wataalamu waliobobea kwenye eneo la fedha na uwekezaji na kuwa tayari kulipa gharama ili kupata ushauri na mwongozo wao. Matajiri huwa wanakuwa na wahasibu bora pamoja na wanasheria ambao wanawashauri na kuwaongoza vyema kwenye mambo yao ya kifedha na uwekezaji.

Masikini hawahangaiki na yote hayo, wao wakipata fedha wanatumia mpaka ziishe, kipato kikiongezeka, matumizi pia yanaongezeka. Na kuwekeza ni mpaka waone wengine wanafanya hivyo, lakini pia hawadumu kwenye uwekezaji kwa muda mrefu, huuza uwekezaji wao na kufanya matumizi.

Masikini huwa ni wajuaji sana, hawathamini utaalamu wa washauri sahihi kwenye eneo la fedha. Hukazana kufanya kila kitu peke yao na hivyo kufanya makosa mengi ambayo yanawagharimu sana. Matokeo yake ni kubaki kwenye umasikini licha ya kuwa na kipato ambacho kingeweza kuwafikisha kwenye utajiri.

Kwa kuwa kipato peke yake hakitoshi kuzalisha utajiri, ni mpaka mtu awekeze muda, nguvu na fedha ndiyo aweze kuzalisha utajiri. Wewe kuwa tayari kuufanyia kazi utajiri wako. Usisubiri mambo yatokee, bali yafanye yatokee. Weka juhudi za kutosha kuhakikisha unajenga utajiri mkubwa unaotaka kuwa nao kwenye maisha yako.

Somo hili ni mwendelezo wa mfululizo wa masomo kutoka kitabu The Millionaire Next Door: The Surprising Secrets of America’s Wealthy kilichoandikwa na Thomas J. Stanley na William D. Danko. Masomo yote kutoka kwenye kitabu hicho yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mpana juu ya somo hili la kufanya uwekezaji wa MUDA, NGUVU na FEDHA kujenga utajiri mkubwa. Fungua hapo chini kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.