Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Tunajua jinsi ambavyo wanaotaka utajiri ni wengi, lakini wanaoupata utajiri huo ni wachache sana.

Kinachowatofautisha wachache wanaopata utajiri na wengi wanaoukosa siyo kwamba wanaopata utajiri wana uwezo zaidi. Bali ni kwa sababu wanaopata utajiri wana ujasiri kuliko wale wasiokuwa na utajiri.

Karibu kila mtu anayetaka kupata utajiri anajua kabisa nini anapaswa kufanya ili kupata utajiri huo. Lakini kufanya hayo anayopaswa kufanya ili kuupata utajiri ndiyo imekuwa vigumu kwa wengi.

Ili wewe uweze kujenga utajiri wa uhakika na utakaokufikisha kwenye uhuru wa kifedha unaoutaka, unapaswa kujijengea ujasiri kwenye maeneo muhimu tunayokwenda kujifunza hapa.

KUISHI MAISHA YAKO.

Watu wanaokuzunguka kuna aina ya maisha ambayo wamekupangia wewe unapaswa kuyaishi. Ukienda kinyume na maisha hayo waliyokupangia, wanakuona kama haupo sawa. Kuna hadhi fulani ambayo watu wanakutaka uwe nayo, kulingana na kipato unachoingiza.

Huo ni mtego ambao umewanasa watu kwenye matumizi makubwa, siyo kwa sababu wanataka, bali kwa sababu ndivyo wanavyotegemewa kuwa.

Kujenga utajiri, kuwa na ujasiri wa kuyaishi maisha yako kwa namna ambayo ni sahihi kwako na kupuuza viwango wanavyokuwekea wengine. Na hata wakuseme au kukudharau kiasi gani, wapuuze, ukishajenga utajiri kila mtu atakuheshimu.

KUJINYIMA MWENYEWE.

Mazoea ambayo wengi tumeshayajenga kwenye maisha yetu ni kitu kikiwepo kitumie, maana kesho kinaweza kisiwepo. Mazoea hayo ndiyo yamekuwa yanawakwamisha wengi wasiweke akiba wala kuwekeza, kwa sababu wanaona hawana uhakika na kesho, hivyo bora wajinufaishe leo.

Kutumia vitu kwa sababu vipo haijawahi kumjenga mtu kuwa imara wala kumnufaisha. Badala yake imewafanya wengi kuwa tegemezi kwenye starehe na raha za muda mfupi.

Kujenga utajiri, jijengee ujasiri wa kujinyima wewe mwenyewe. Jinyime kutumia kitu ambacho unacho bila hata sababu zozote za msingi. Ukifanikiwa kwenye hilo unakuwa unaweza kujidhibiti mwenyewe na kufanya makubwa. Hilo linahitaji ujasiri hasa, maana ni rahisi sana kujidanganya mwenyewe.

KUWAAMBIA WENGINE HAPANA.

Pale unapokuwa na nafasi fulani ambayo ni zaidi ya wengine, labda kuwa na ajira au biashara inayokuingizia kipato, wengine, hasa watu wa karibu huwa wanaona ni wajibu wako kuwakubalia kwenye mambo yao. Hivyo huwa wanakuja kwako na maombi na mapendekezo mbalimbali ambayo unajua kwako hayana tija au ni mzigo.

Kwa sababu ya mahusiano yaliyopo, unashindwa kuwakatalia. Hivyo unawakubalia, licha ya kujua kwamba kitu hakina tija kwako au kinakukwamisha. Unaona ukiwakatalia utaonekana una roho mbaya. Na wengine, hasa wale wa karibu na ambao waliwahi kuwa na mchango kwako huko nyuma, hutumia silaha ya hatia kupata wanachotaka kwako. Watakukumbusha jinsi walikusaidia huko nyuma na hivyo kuwa kama una deni kwao.

Ili kujenga utajiri, kuwa na ujasiri wa kuwaambia watu HAPANA kwenye mambo wanayokuomba au kukupendekezea na unaona hayana tija kwako au yanakuwa kikwazo. Haijalishi watu ni wa karibu kiasi gani au walikusaidia kiasi gani huko nyuma, bado unayo haki ya kuwakatalia kile ambacho hakijakaa sawa kwako. Utalaumiwa na kupewa hatia nyingi, na ndiyo maana inabidi uwe jasiri, kwa sababu ukiwa legelege, utatawaliwa na matakwa ya wengine.

SOMA; 3402; Ujasiri na Mafanikio.

KWENDA KINYUME NA KUNDI.

Kwenye uwekezaji, sehemu kubwa huwa wanapata hasara kwa sababu wanafuata mkumbo. Pale ambapo uwekezaji fulani unafanya vizuri, kila mtu anakimbilia kuununua na hapo bei inapanda na wengi zaidi wanafuata mkumbo wa kuwekeza. Hilo linapelekea watu wanunue uwekezaji kwa bei ya juu. Uwekezaji ukishapanda sana, huwa unaanza kushuka na hapo watu wanakimbilia kuuza, kitu kinachoshusha bei zaidi. Watu wanauza uwekezaji kwa bei ya chini kuliko walivyonunua. Na hivyo kuwa wamepata hasara.

Kujenga utajiri, kuwa na ujasiri wa kwenda kinyume na kundi. Pale watu wengi wanapokimbilia kununua uwekezaji, wewe uza. Na pale watu wengi wanapokimbilia kuuza uwekezaji, wewe nunua.

Hili ndiyo linalohitaji ujasiri wa hali ya juu kuliko mengine yote, maana ni sawa na kununua tiketi kwenye meli inayozama. Pale uwekezaji unaposhuka thamani, unahitaji roho ngumu sana kununua.

KUWA NA SUBIRA YA MUDA MREFU.

Tunajua faida kubwa ya uwekezaji ipo kwenye muda. Pale uwekezaji unapofanyika kwa muda mrefu ndiyo thamani yake inakua zaidi. Lakini watu wengi huwa hawana subira ya muda mrefu. Hadithi za mafanikio ya haraka huwa zinahadaa sana wengi na kuwapoteza.

Kujenga utajiri, kuwa jasiri wa kuachana na tamaa za muda mfupi na fanya uwekezaji wa muda mrefu. Hata kama unaona muda ni mrefu sana na unaweza usiwepo, wewe amini kwenye muda mrefu, utanufaika zaidi. Wengi wanaoona muda ni mrefu na hawatakuwepo, huwa wanaishia kuwepo, na kuwa chini sana.

NJIA YA KUJENGA UJASIRI.

Ujasiri siyo kitu ambacho unazaliwa nacho, wala siyo kitu cha kufundishwa. Pia huwezi kununua ujasiri hata kama una uwezo kiasi gani.

Ujasiri unajengwa kwa hatua ambazo mtu unachukua. Na njia pekee ya kujenga ujasiri ni kufanya yale unayohofia au kukwepa kufanya. Pale unapojua kitu ni sahihi kwako kufanya, unapaswa kukifanya licha ya hofu au mkwamo unaokuwa unakutana nao.

Ni kupitia kufanya ndiyo unagundua hofu na mikwamo unayokuwa nayo siyo uhalisia. Unagundua vitu hivyo vinakuwa na nguvu pale ambapo huchukui hatua. Ukichukua hatua unavinyima nguvu ya kukukwamisha.

Jijengee ujasiri kwa kufanya yale unayohofia au kukwama kuyafanya na utaona jinsi ulivyo na uwezo wa kufanya zaidi.

Ujasiri siyo kutokuwa na hofu, bali kufanya licha ya kuwa na hofu. Hivyo wewe ongozwa na hofu, pale unapohofia kufanya kitu, jiambie hicho ndiyo utafanya. Kwani upande wa pili wa hofu ndipo penye mafanikio makubwa kwako.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili kushirikisha yale uliyojifunza na unavyokwenda kuyafanyia kazi. Jibu maswali yafuatayo;

1. Ni ujasiri gani ambao umekuwa nao tangu muda mrefu na umekuwezesha kupiga hatua kwenye eneo la fedha na utajiri?

2. Ni ujasiri gani ambao umeukosa kwa muda mrefu na umekuwa kikwazo kwako kupiga hatua kubwa zaidi?

3. Ni hatua zipi unazokwenda kuchukua kuanzia sasa ili kujenga ujasiri mkubwa wa kukufikisha kwenye utajiri na uhuru wa kifedha?

4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Tuma majibu ya maswali haya kama sehemu ya kusoma somo, kuelewa na kwenda kufanyia kazi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.