3406; Juhudi, muda na nyenzo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa unayoyataka, yanahitaji juhudi kubwa ambazo zinawekwa kwa muda mrefu.
Lakini hayo pekee hayatoshi, lazima pia kuwe na nyenzo, ambayo inasaidia juhudi hizo kuzalisha matokeo makubwa zaidi.

Nyenzo ni rasilimali za wengine, ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuyakuza matokeo zaidi.
Juhudi zinapoambatana na nyenzo na kupewa muda wa kutosha, hakuna kinachoweza kushindikana.

Matokeo yatakayopatikana yatakuwa ni makubwa sana kuliko ambavyo juhudi hizo hizo zingeweza kuyazalisha bila ya nyenzo.

Kwa mabadiliko yoyote unayotaka kupata kwenye maisha yako, jiulize ni juhudi zipi unazopaswa kuweka na nyenzo gani unazoweza kutumia na pia muda kiasi gani unaweza kutenga kwa ajili ya mabadiliko hayo.

Watu huwa wanataka kupata mabadiliko, lakini hawapo tayari kuwekeza juhudi, muda na nyenzo ya kutosha.

Chochote utakachoongeza zaidi kwenye hivyo vitatu, kutasababisha matokeo kuwa makubwa zaidi.
Ukiongeza juhudi, matokeo yanaongezeka pia.
Ukiongeza muda, matokeo yanaongezeka.
Kadhalika ukiongeza nyenzo, matokeo yanaongezeka.

Kukuza matokeo unayopata sasa, jiulize nini unapaswa kuongeza na ni rahisi zaidi kwako kwenye hali uliyonayo sasa.
Je ni juhudi, muda au nyenzo?
Kama umeshafanya sana na umetingwa kiasi kwamba huwezi tena kuongeza juhudi na muda, angalia upande wa nyenzo.

Upande wa nyenzo una nafasi kubwa ya kukuza kwa sababu hautegemei rasilimali zako binafsi.
Nyenzo ni rasilimali za wengine, ambazo zikiweza kutumika vizuri zinakuzalishia matokeo makubwa.

Wapo wenye mtazamo kwamba ili wayafurahie matokeo, lazima yawe yametokana na juhudi zao tu.
Yakitokana na nyezo wanaona kama hawayastahili vile.
Lakini unadhani kutumia nyenzo kwa manufaa ni rahisi kihivyo?
Ni rahisi zaidi kutumia rasilimali zako mwenyewe kuliko za wengine.

Hivyo usione kama ni udanganyifu kupata matokeo makubwa kwa kutumia rasilimali za wengine.
Uwezo tu wa kutumia rasilimali hizo kwa manufaa ni wa kipekee na siyo wote wanaoweza.

Mabadiliko au matokeo yoyote unayotaka kupata, anza kwa kupanga ni juhudi, muda na nyenzo kiasi gani vinahitajika.
Kisha wekeza vitu hivyo ili kuzalisha matokeo hayo unayoyataka.

Juhudi sahihi, ambazo zimeambatana na nyezo sahihi na kwa muda mrefu, vitakufikisha kwenye mafanikio makubwa zaidi ya pale ulipo sasa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe