3408; Kuomba na kutoa ushauri.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Eneo la ushauri ni eneo ambalo limekuwa na upotevu mkubwa wa muda na umakini wa watu.
Kwani ni eneo ambalo watu huwa wanalipenda sana, kwa sababu linawafanya wajisikie vizuri, hata kama hakuna matokeo ya tofauti yanayokuwa yamepatikana.
Tukianza na kuomba ushauri.
Watu wengi ambao huwa wanaomba ushauri, huwa hawaendi kuufanyia kazi pale wanapopewa ushauri huo.
Na siyo kwa sababu ushauri wanaokuwa wamepewa hauwafai, bali kwa sababu walichokuwa wanataka siyo ushauri.
Wengi wanapoomba ushauri wanakuwa wanataka kuhalalisha kile ambacho tayari wanakitaka wao.
Hivyo kama ushauri utaendana na walivyokuwa wanataka, watasema ni ushauri mzuri na kuendelea nacho.
Na kama ushauri utakuwa ni kinyume na walivyotaka, watasema ni ushauri mbaya na kuendelea na kile walichokuwa wamepanga.
Kwa ujumla, ushauri ambao mtu anaomba na kupewa, haubadili chochote.
Na hiyo inapelekea zoezi zima la kuomba na kupewa ushauri kuwa la kupotezeana muda.
Kwa upande wa pili wa kutoa ushauri, watu wanapenda kushauri hata pale ambapo hawajaombwa kufanya hivyo.
Yaani watu wakikutana na kitu au hali, tayari wanakuwa na ushauri ambao wanaweza kuutoa juu ya kitu au hali hiyo.
Watu hujipa umuhimu wa kushauri nini kinachopaswa kufanyika kwenye hali hiyo, wakiona ushauri wao ni muhimu na wenye mchango.
Lakini wale wanaoshauriwa huwa hawachukui ushauri huo, hata kama unakuwa mzuri kiasi gani.
Kwa sababu hawakuomba ushauri huo, hivyo hawana uhitaji nao.
Wataendelea kufanya kile ambacho walikuwa wanafanya au walipanga kufanya.
Hiyo inapelekea zoezi zima la kutoa ushauri ambao mtu hajaombwa kuwa la kupoteza muda.
Ili kuwa na tija kwenye zoezi la kuomba na kutoa ushauri;
Unapoomba ushauri, hakikisha hujafanya maamuzi bado. Kadhalika kwa wanaokuomba ushauri, hakikisha bado hawajafanya maamuzi.
Ni rahisi kujua hilo kwa kuuliza maswali na kusikiliza kwa umakini.
Unapotoa ushauri, kwanza usitoe kwa watu ambao hawajakuomba na usitoe kwa mambo ambayo wewe mwenyewe huna uzoefu nayo.
Tingwa na mambo muhimu kwako ili usipate muda wa kuhangaika na ya wengine na kujikuta unatoa ushauri ambao hujaombwa.
Zingatia haya tuliyokumbushana hapa ili kupunguza upotevu wa muda na hali za kukwazana kwenye kuomba na kutoa ushauri.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe