Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanapenda kupata utajiri kwenye maisha yao. Lakini wanaoupata utajiri hasa wamekuwa ni wachache sana.

Wale wanaoutaka utajiri ila wanaukosa, siyo kwamba hawajui jinsi ya kuupata. Wengi wanajua kabisa nini wanapaswa kufanya ili kupata utajiri. Lakini inapofika wakati wa kufanya wanachopaswa kufanya, hawafanyi.

Mwandishi Ramit Seth, kwenye kitabu chake kinachoitwa I WILL TEACH YOU TO BE RICH, ameonyesha kwa nini watu wengi hawapati utajiri licha ya kuwa wanautaka sana.

Kupitia kitabu hicho, Ramit anatuonyesha jinsi ambavyo ikija kwenye fedha, tatizo siyo fedha, bali tatizo ni watu wenyewe. Hali yetu ya kifedha imekuwa inaathiriwa sana na saikolojia, hisia na tabia ambazo tunakuwa nazo.

Hivyo kama tunataka kujenga utajiri kwa uhakika, kazi yetu ya kwanza ni kujenga saikolojia, hisia na tabia sahihi kuhusu fedha.

Kwenye somo hili na mfululizo wa masomo mengine yaliyopo HAPA, tunakwenda kujifunza jinsi ya kujenga utajiri, kwa hatua sita za uhakika kabisa.

KILA MTU MJUAJI, ILA HAKUNA MFANYAJI.

Fedha na afya ndiyo vitu ambavyo vinawagusa watu wote kwa usawa kabisa. Lakini pia ni vitu vinavyofanana sana kwa sababu kila mtu huwa ana maoni yake binafsi ya nini sahihi na nini siyo sahihi.

Lakini pia kupata matokeo mazuri kwenye fedha na afya, kuna misingi inayojulikana, ila cha kushangaza wengi wamekuwa wanaipuuza.

Kwenye afya, ili kupunguza uzito, mtu anatakiwa KULA kwa usahihi na kufanya MAZOEZI. Mtu yeyote, akifanya hayo mawili, kwa nidhamu ya hali ya juu, atapata matokeo mazuri. Lakini sasa, njoo kwenye uhalisia na angalia ni vitu gani watu wanahangaika navyo ili kupunguza uzito. Wapo wanaohangaika na kunywa dawa za kupungua, wapo wanaofanya upasuaji na mengine mengi.

Kadhalika inapokuja kwenye fedha, ili kujenga utajiri, mtu anatakiwa kuwa na matumizi yaliyo chini ya kipato chake, kuweka akiba na kuwekeza kwenye kila kipato anachoingiza. Lakini sasa, njoo kwenye uhalisia na angalia vitu watu wanahangaika navyo kuhusu kujenga utajiri, njia za mkato, kuchuuza soko la hisa, fedha za kidijitali na mengine mengi.

Inapokuja kwenye fedha watu ni wajuaji sana, wanahangaika na mambo mengi, lakini hakuna matokeo mazuri wanayoyapata. Hiyo ni kwa sababu wanapuuza misingi muhimu ya kujenga utajiri.

SOMA; Jijengee Mtazamo Sahihi Wa Utajiri Kutoka Kitabu SECRETS OF MILLIONAIRE MIND.

UJUMBE MKUU WA KITABU; I WILL TEACH YOU TO BE RICH.

Mwandishi Ramit Seth anatuambia ujumbe mkuu wa kitabu chake ni kama ifuatavyo;

1. Suluhisho la asilimia 85; Ni bora kuanza kuliko kubobea, anza hata kama hauna taarifa kwa asilimia 100.

2. Ni sawa kufanya makosa, hasa unapokuwa unaanza.

3. Fanya matumizi makubwa kwenye vitu unavyopenda na punguza sana matumizi kwenye vitu usivyopenda.

4. Uwekezaji siyo maonyesho, bali kuingiza fedha.

5. Usiishi kwenye kikokotoo, chagua mfumo bora kwako kisha endelea na maisha yako.

6. Cheza mchezo wa utajiri kushambulia (kuchukua hatua) na siyo kulinda (kuhofia).

7. Unatumia fedha kutengeneza maisha ya kitajiri.

SHERIA 10 ZA MAISHA YA KITAJIRI.

Lengo la kujenga utajiri ni kuishi maisha ambayo mtu unayafurahia. Na maisha ya kitajiri yana sheria zifuatazo;

1. Matumizi kwenye vitu unavyopenda, ubahili kwenye vitu usivyopenda.

2. Weka umakini kwenye machache makubwa na muhimu, achana na mengi yasiyo na tija.

3. Fanya uwekezaji wa muda mrefu na wenye faida.

4. Kuna ukomo kwenye kupunguza matumizi, lakini hakuna ukomo kwenye kuongeza kipato.

5. Ndugu, jamaa na marafiki watakushauri sana kwenye fedha, lakini wewe nenda na mpango wako.

6. Chagua matumizi ambayo utafanya bila ya kufikiria.

7. Hangaika na yale ya msingi kwanza, hayo ndiyo yanajenga kila kitu.

8. Wewe ndiye unayewajibika na maisha yako, hakuna wa kukuokoa.

9. Kuwa tayari kuwa tofauti na wengine.

10. Ishi maisha nje ya kikokotoo, jenga na boresha mahusiano muhimu kwako.

HATUA SITA ZA KUJENGA UTAJIRI.

Kwenye kitabu cha I WILL TEACH YOU TO BE RICH, mwandishi anatufundisha hatua sita za kufuata ili kujenga utajiri kwa uhakika kwenye maisha yetu. Hatua hizo ni kama ifuatavyo;

Hatua ya kwanza; Kuondoka kwenye madeni na usimamizi wa mikopo.

Hatua ya pili; Kuwa na akaunti sahihi za benki.

Hatua ya tatu; Kufungua akaunti za uwekezaji.

Hatua ya nne; Kudhibiti matumizi.

Hatua ya tano; Kurahisisha mzunguko wa fedha.

Hatua ya sita; Kujifunza uwekezaji sahihi.

Hatua hizo sita zikifanyiwa kazi kwa uhakika, mtu anaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake.

Watu wamekuwa wanahangaika sana na siri za utajiri, lakini ukweli ni kwamba hakuna siri yoyote. Kanuni sahihi inajulikana; CHUKUA HATUA NDOGO NDOGO, KUWA NA NIDHAMU na KUWA NA SUBIRA. Ukiweza hayo, umeuweza utajiri.

Masomo yote ya kujenga utajiri kutoka kitabu kinachoitwa I WILL TEACH YOU TO BE RICH kilichoandikwa na Ramit Seth yanapatikana kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.

Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu somo hili. Fungua ujifunze kwa kina na kupata shuhuda za wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.