Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka CHUO CHA MAUZO.
Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.
Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.
Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.
Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 33 na 34.
Kwenye mbinu namba 33 tulijifunza ukamilishaji wa bajeti namba 5
Na kwenye ukamilishaji wa namba 34 tulijifunza ukamilishaji wa kusali.
Mteja akija na kukuambia yuko juu ya bajeti wewe unamwambia asilimia 90 ya wateja ninawauzia huwa wanakuwa juu ya bajeti wanapofika hapa, hivyo kamilisha malipo ili ukafurahie bidhaa au huduma yako.
Tumia imani ya mteja kukamilisha malipo kwa kusali kwa pamoja inakuwa ni njia nzuri ya kumkamata mteja kama anataka kukutoroka.
SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 33-34
Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 35 na 36
Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;

35. Ukamilishaji wa kufikiria zaidi – 1.
Mteja anakuja anakuambia nahitaji kitu fulani, unampatia inapofika kwenye bei, anakuambia ooh, bei kubwa, ngoja nikafikirie kwanza.
Baada ya mteja kukuambia hivyo, usiwe na wasiwasi, mshushie silaha ya ukamilishaji kwa kumwambia hivi;
“Kufikiria ni kitu cha mara moja. Fikiria kuhusu tembo. Umeona, mara moja umeweza kufikiria kuhusu tembo. Unachohitaji sasa ni kufanya maamuzi. Ndiyo au hapana. Unafanya au hufanyi. Nipo tayari kwa maamuzi yoyote, umeamua nini?”
Huu ni ukamilishaji wa nguvu pale mteja anaposema anataka akafikirie zaidi.
Kwa kutumia ukamilishaji huu, mteja anasukumwa kufanya maamuzi mara moja badala ya kutumia kufikiria kama kisingizio cha kutokuamua.
Mara zote tumia ukamilishaji huu pale mtu anapokuambia ngoja akafikirie zaidi.
36. Ukamilishaji wa kufikiria zaidi – 2.
Mteja anakuja na pingamizi lake, baada ya kushindwa kukamilisha malipo,akiwa anatafuta namna ya kukutoroka, anakuambia ngoja tu nikafikirie zaidi.
Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, hupaswa kukubali kirahisi, badala yake mgeuzie kibao kwa kumuuzia kwa kutumia mapingamizi anayokupa.
Mteja akikuambia, nahitaji kufikiria, mwambie hivi;
“Nakuelewa. Lakini wewe kufikiria zaidi haibadilishi ukweli kwamba bidhaa hii inakuokolea fedha, unaihitaji na inabidi uwe nayo muda siyo mrefu. Fanya maamuzi sasa ili uweze kuendelea kufikiria vitu vingine vinavyohitaji umakini wako. Weka sahihi yako hapa, tukamkabizi hili tafadhali, lipia uondoke na bidhaa yako, lipia ukafurahie huduma au bidhaa yako”
Kwa ukamilishaji huu unaonyesha kuelewa, kisha unatumia sababu yao kukamilisha mauzo. Unachopaswa kujua ni watu wanapokuwa wanakitaka kitu huwa hawafikirii, wanakinunua tu.
Kila wakati, usikubali Sababu za mteja kukuzuia wewe. Badala yake tumia sababu wanazokupa kuwashawishi kununua kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.
Hatua ya kuchukua leo;
Kwa kila pingamizi unalokutana nalo kuhusu mteja kukuambia ngoja nikafikirie kwanza, mkamate kwa mbinu hizi za ukamilishaji tulizojifunza leo ambao ni ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba moja na namba 2.
Mwisho, nenda kayafanyie kazi haya uliyojifunza leo. Kama mkamilishaji na muuzaji bora kuwahi kutokea unapaswa mwonyesha mteja matokeo mazuri anayokwenda kuyapata baada ya kuwa amenunua.
Elezea matokeo ambayo mteja atayapata baada ya kupata kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma na siyo kueleza sifa za biashara.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505 //0767101504