Rafiki yangu mpendwa,
Kuwa kwenye ajira ambayo kipato ni kidogo, huwa kunampa mtu hasira ya kuchukua hatua za kukuza kipato chake nje ya ajira hiyo.
Na hapo mtu anapata msukumo wa kuanzisha biashara akiwa bado yupo kwenye ajira. Kwa sababu ya nidhamu kali ambayo mtu anakuwa nayo, biashara inaonyesha mwelekezo mzuri wa mafanikio.
Hapo mtu anaona kama ameweza kuikuza biashara kwa kiasi fulani akiwa bado ameajiriwa, kama akitoka kwenye ajira na kuweka nguvu zake zote, ataweza kuikuza zaidi.
Na hilo ndiyo kosa kubwa sana ambalo waajiriwa wengi wanaoanzisha biashara wakiwa kwenye ajira huwa wanalifanya. Ni kosa ambalo huwa linawagharimu sana, wanaishia kuua biashara zao na kulazimika kurudi kwenye ajira.

Iko hivi rafiki, biashara kuonekana inafanya vizuri, siyo kigezo cha kuacha ajira na kwenda kuifanya kwa muda wako wote. Biashara inakuwa inafanya vizuri kwa sababu unakuwa huitegemei kama sehemu ya kipato. Kwa sababu tayari una mshahara, unautumia huo kuendesha maisha yako na hivyo kuipa biashara fursa ya kukua.
Unapoacha ajira na kuingia kwenye biashara yako muda wote, unaanza kuitegemea kupata kipato cha kuendesha maisha yako. Hapo sasa biashara inaanza kuwa na mizigo ambayo inaielemea na kupelekea kushindwa.
Kuondokana na hali hiyo ya kuua biashara ambayo ilikuwa na mwelekeo mzuri, kuna vigezo vikubwa viwili ambavyo unapaswa kuvitimiza kabla hujatoka kwenye ajira.
Kigezo cha kwanza ni MSHAHARA MBADALA.
Kabla hujaacha ajira na kwenda kusimamia biashara yako, hakikisha unajilipa kutoka kwenye biashara hiyo mshahara ambao unalingana au kuzidi ule unaopokea kwenye ajira. Kama biashara inaweza kukulipa hivyo kwa miezi sita, bila ya kuyumba, basi hiyo imeshakomaa. Kama utaacha ajira na kupeleka nguvu zako zote, utaweza kuikuza zaidi bila ya kuiongezea mizigo.
Hakikisha kila mwezi unajilipa kutoka kwenye biashara yako kwa namna ambayo biashara itamudu, kisha kuza kipato hicho unachojilipa mpaka kifikie au kuzidi mshahara unaolipwa kwenye ajira.
SOMA; BIASHARA NDANI YA AJIRA; Mwongozo Wa Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Kwenye Ajira.
Kigezo cha pili ni AKIBA YA KUENDESHA MAISHA.
Kabla hujaachana na ajira, unapaswa kuwa na akiba itakayotosha kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka 12 hata kama hutakuwa na kipato kabisa. Hii ni akiba ya dharura ambayo itakusaidia pale mambo yatakapokwenda tofauti na ulivyotegemea. Kwa sababu biashara inaweza kukulipa vizuri tu, lakini mabadiliko ya kiuchumi yakaiathiri sana biashara na mambo yakaenda tofauti.
Kwa sababu hujui mabadiliko yatatokea wakati gani, jipange kwa kuwa na akiba ya kukuwezesha kuendesha maisha hata kama hutakuwa na kipato. Kwa kuwa na akiba hiyo, utaweza kuendelea kupambana kuweka mambo sawa. Ukiwa huna akiba, unapokutana na magumu utajikuta unalazimika kurudi tena kuajiriwa.
Na ubaya ni kwamba ukiacha ajira na kwenda kujiajiri, kisha ukarudi tena kwenye ajira, huwa unakuwa na woga wa kuchukua tena hatua kama hiyo.
Kabla hujatoka kwenye ajira na kwenda kwenye biashara, hakikisha umeweka akiba hiyo ya kuwezesha maisha yako kwenda, kuanzia miezi sita mpaka mwaka. Hicho ni kipindi ambacho unaweza kujipanga upya na ukarudi vizuri, pale unapokuwa umekutana na ambayo hukuyategemea.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua vizuri vigezo hivyo viwili na jinsi unavyopaswa kuvijenga ili uweze kujenga biashara imara wakati unaendelea na ajira yako. biashara ikishasimama vizuri uweze kwenda kuiwekea juhudi kwa asilimia 100. Karibu ujifunze zaidi kutoka kwenye kipindi hicho ili uweze kununua uhuru wako wa kipato kutoka kwenye ajira.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.