Rafiki yangu mpendwa,
Bilionea Mwekezaji Warren Buffet amewahi kunukuliwa akisema; “Kama huwezi kuingiza fedha ukiwa umelala, utafanya kazi maisha yako yote.” Kauli hiyo ni nzito na muhimu sana kwa sababu utajiri ni pale fedha inapokufanyia wewe kazi na siyo wewe kuifanyia kazi fedha.
Kila mtu anajua nini anapaswa kufanya ili aweze kujenga utajiri, lakini ni watu wachache sana ambao wanafanya hayo yanayopaswa kufanyika. Na wengi siyo kwamba hawafanyi kabisa, wengi huwa wanaanza, lakini wanaishia njiani. Wakati utajiri unataka mtu ufanye mambo kwa msimamo bila kuacha kwa muda mrefu.

Mwandishi Ramit Sethi, kwenye kitabu chake cha I WILL TEACH YOU TO BE RICH, anatusaidia kuondokana na hali hiyo ya kuanza mipango ya utajiri na kuishia njiani. Kwenye kitabu chake anatushirikisha jinsi ya kuweka mipango ya moja kwa moja ambayo inafanya kazi bila ya kututegemea sisi kuingilia.
SURA YA 5; WEKA AKIBA UKIWA UMELALA.
Tunapopanga kufanya kitu, huwa tunakuwa na shauku kubwa ya kukifanya mwanzoni. Lakini kadiri muda unavyokwenda tunachoka kukifanya na hapo tunaacha. Hivyo ndivyo mipango mingi ya kifedha inavyoishia njiani. Kwa sababu ya kuchoka na usumbufu, wengi wanaishia njiani.
Kuondokana na hali hiyo, Ramit anatushirikisha mpango wa kufanya moja kwa moja (Automatic) ili kuhakikisha tunaendelea na mikakati yetu bila kuishia njiani.
Baada ya kuweka mpango wako sahihi wa matumizi, ambao unakigawa kipato chako kwenye mafungu, kinachofuata ni kuwa na mpango wa kugawa kipato chako kwenda kwenye makundi hayo moja kwa moja.
Unafanya hivyo kwa kuwa na akaunti mbalimbali benki na kisha kuipa benki maelekezo ya kuhamisha fedha kwenye akaunti yako ya kipato na kupeleka kwenye akaunti nyingine kulingana na mipango yako.
Kwa maelekezo hayo, benki itakuwa inatawanya fedha zako kama ulivyopanga. Hilo linakuhakikishia mkakati wako unaendelea bila kuathiriwa na hisia au tabia zako.
Faida za mfumo huu wa moja kwa moja wa kugawa kipato chako ni kama ifuatavyo;
1. Mfumo hauathiriwi na mapungufu yako kama binadamu.
2. Mfumo unakua kadiri kipato kinavyoongezeka.
3. Mfumo unaendelea kuwa na moto hata pale unapokuwa umepoa.
Ukitegemea hamasa yako binafsi kwenye kutekeleza mipango yako ya kifedha, utakwama. Weka mfumo wa moja kwa moja na uache ufanye kazi bila ya kuuingilia.
SOMA; Aina Za Uwekezaji Unaopaswa Kufanya Ili Kujenga Utajiri Mkubwa Kwenye Maisha Yako.
SURA YA 6; UONGO WA WATAALAMU WA FEDHA.
Eneo la fedha limekuwa na wataalamu wengi sana ambao wanashauri namna gani watu wapangilie fedha zao ili kujenga utajiri. Lakini sehemu kubwa ya yanayoshauriwa na wataalamu hao siyo tu hayafanyi kazi, bali pia yanakuwa hasara kwa wengi.
Changamoto za wataalamu wa fedha na ushauri wanaotoa ni nne;
Moja; ushauri wanaokupa unawanufaisha wao binafsi. Pale wataalamu wa fedha wanapokuambia wekeza eneo fulani, wanakuwa wanalipwa kamisheni kama utawekeza. Je unadhani watakushauri kwa usahihi au watakushauri kwa manufaa yao?
Mbili; gharama za ushauri au usimamizi ni kubwa na zinaathiri faida unayopata. Kwa wataalamu ambao wanatoza gharama za ushauri au usimamizi wa uwekezaji, huwa gharama zao ni kubwa na hivyo kuathiri faida inayoweza kupatikana.
Tatu; wanatabiri vitu ambavyo huwa havitokei. Kwenye fedha, utabiri huwa ni mwingi kila siku, kuhusu kupanda na kushuka kwa uchumi, lakini kwa sehemu kubwa utabiri huo huwa hautimii na hivyo kuzidi kuwa wanapotosha.
Nne; kuahidi kwamba wanaweza kulivizia na kulizidi soko. Ni wachache sana ambao wanaweza kulizidi soko kwa muda mrefu. Wengi wakipata faida kubwa mwaka mmoja, miaka mingine wanapata hasara.
Unapokuwa unaanza uwekezaji, achana na ushauri mwingi wa kitaalamu. Wewe chagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja yenye gharama ndogo, kisha endelea na maisha yako. Huko utapata ukuaji wa uhakika kwa muda mrefu.
SURA YA 7; UWEKEZAJI SIYO KWA MATAJIRI PEKEE.
Watu wengi wakisikia kuhusu uwekezaji, huwa wanadhani ni kitu kinachopaswa kufanywa na matajiri pekee. Wengi huona kwa kipato kidogo wanachokuwa nacho, hawawezi kuanza kuwekeza.
Lakini hayo siyo kweli, wakati mzuri wa kuanza kuwekeza ni wakati kipato ni kidogo. Kwani kwa njia hiyo mtu anajenga tabia sahihi huku pia uwekezaji wake ukikua na kumzalishia faida.
Na kwa kuwa tumeshaona hisia na tabia zetu ni kikwazo kwenye mipango yetu ya kifedha, tunapaswa kuwa na mpango wa moja kwa moja wa uwekezaji. Mpango ambao unahamisha fedha moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zetu na kupeleka kwenye akaunti za uwekezaji. Kwa njia hiyo utaweza kuwekeza kwa msimamo bila kuacha.
Ngazi tatu za uwekezaji.
Kwenye kufanya uwekezaji, kuna ngazi kubwa tatu;
Ngazi ya kwanza ni HISA, HATIFUNGANI NA FEDHA TASLIMU.
Hii ni ngazi ya uwekezaji ambao ni mgumu kwa mtu kufanya, udhibiti wake ni mkubwa na marejesho yake ni madogo.
Ngazi ya pili ni MIFUKO YA PAMOJA.
Hii ni ngazi ambayo uwekezaji ni rahisi kwa mtu kufanya, udhibiti ni wa wastani na faida pia ni ya wastani.
Ngazi ya tatu ni MIFUKO MAALUMU.
Hii ni ngazi ambayo uwekezaji ni rahisi zaidi kwa mtu kufanya, udhibiti wake ni mdogo na faida ni kubwa.
Kupangilia wapi uwekeze inategemea na umri ambao mtu anao. Katika umri mdogo, mtu anaweza kuwekeza ngazi ya kwanza, umri unapokwenda anahitaji ngazi za juu zaidi.
Ili kufikia uhuru wa kifedha kwa haraka, mtu anapaswa;
1. Kupunguza sana gharama zako za maisha ili sehemu kubwa uweke akiba na kuwekeza.
2. Kuongeza sana kipato chako kwa ukubwa na ongezeko lote kupeleka kwenye kuwekeza.
3. Kufanya vyote kwa pamoja, yaani kupunguza gharama na kuongeza kipato na hapo kupata manufaa ya pande zote.
Kumbuka kupunguza gharama kuna ukomo, ila kuongeza kipato hakuna ukomo. Unapofanya vyote kwa pamoja, manufaa yanakuwa makubwa.
Masomo yote ya kujenga utajiri kutoka kitabu kinachoitwa I WILL TEACH YOU TO BE RICH kilichoandikwa na Ramit Seth yanapatikana kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.
Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu somo hili. Fungua ujifunze kwa kina na kupata shuhuda za wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.