3415; Haijawahi kuwa rahisi hivi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Tunaishi kwenye zama bora na za kipekee sana.
Hizi ni zama ambazo kupata mafanikio makubwa ni rahisi kuliko zama nyingine zozote.
Haijawahi kuwa rahisi kufanikiwa kama ilivyo sasa.
Maarifa kuhusu mafanikio ni mengi na yanapatikana kwa urahisi sana.
Kila unachopaswa kujua kuhusu mafanikio, tayari unaweza kujua bila ya kikwazo chochote kile.
Kwa vipindi vya nyuma, taarifa kuhusu mafanikio zilikuwa zinahodhiwa na watu wachache tu.
Fursa za kujenga mafanikio makubwa ni nyingi na zipo wazi kwa kila mtu.
Kitu chochote ambacho mtu anaweza kufanya, kina fursa ya kuweza kumpa mafanikio makubwa.
Mafanikio hayapo tena kwenye mambo fulani machache ambayo watu maalumu ndiyo wanaweza kuyafanya bali yapo kwenye yale yanayofanywa na kila mtu.
Ushindani ni mwepesi sana kwenye zama hizi kwa sababu ya wengi kufanya kwa mazoea.
Wengi wanafanya leo yale waliyofanya jana.
Kwa kutokujifunza na kufanya kwa mazoea kumepelekea wengi kupata matokeo madogo sana.
Hilo linawapunguzia sana nguvu ya ushindani.
Licha ya wengi kuwa wanafanya kitu, ushindani ni mdogo sana.
Hivyo ukiweza kwenda nje tu ya mazoea na kufanya vitu kwa utofauti, utazalisha matokeo makubwa na ya kipekee.
Kwa mazingira na hali zilizopo sasa, kutokufanikiwa ni kitu cha kujitakia.
Ni uzembe wa hali ya juu kabisa na ambao adhabu yake ni mtu kuishi maisha duni kwa muda mrefu.
Usikubali kutumikia hiyo adhabu wakati njia ni nyepesi kwako kuweza kufanya kwa ukubwa na tofauti ili kuzalisha matokeo makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe