3417; Kutamani na kutaka.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye haya maisha, kila mtu huwa anapata kile anachotaka.
Na hiyo inamaanisha kutaka kweli na siyo tu kutamani.
Kutaka kitu ni kudhamiria hasa kukipata na kuchukua hatua sahihi ili kukipata.
Hatua kubwa ya kuchukua ni kuwataka wengine wawape kile wanachotaka.
Wanaweka wazi nini wanachotaka na wapo tayari kutoa nini ili kupata wanachotaka.
Wanaokosa kile wanachotaka ni kwa sababu wanakuwa wamekitamani tu. Wanaishia kutoa tu mapendekezo ya yale wanayotamani yangetoea.
Wanakuwa hawajadhamiria kweli kupata, hivyo hawaweki msisitizo mkubwa kwa wengine ili wawape.
Ukweli wa maisha ni kwamba unaishia kupata kile unachowataka watu wengine wakupe.
Ni kile unachovumilia ndiyo unachoishia kukipata.
Kama utaweka viwango vyako kuwa juu na kukataa kupokea chochote chini ya viwango hivyo, utapata vitu vya viwango vya juu kama ulivyoomba.
Unaweza kuwa unajiuliza kama ni rahisi hivyo, kwa nini wengi hawapati yale wanayotaka kuwa nayo?
Jibu ni rahisi, kupata kile unachotaka kwa kuwataka wengine wakupe siyo rahisi kihivyo.
Kwanza kuna nafasi kubwa ya kukataliwa kuliko kukubaliwa.
Watu wengi huwa wanahofia kukataliwa kuliko kitu kingine chochote.
Ndiyo maana wengi wanakuwa tayari kutokupata kitu kuliko kukitaka na kulazimika kujiweka kwenye mazingira ya kukataliwa.
Kugeuza mtazamo wako kuhusu kukataliwa na kushindwa kuna nguvu ya kukuwezesha kupata unachotaka.
Kwenye kukataliwa kuwa na mtazamo kwamba kila hapana unayopata, unajisogeza karibu zaidi na ndiyo.
Na kwenye kushindwa, ni pale unapoacha kufanya, kama unaendelea kufanya, ushindi ni lazima.
Taka hasa kupata kitu.
Watake wengine wakupe unachotaka.
Na weka juhudi zako kuhakikisha kweli unapata kile unachotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe