Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anayetaka kuwa na afya bora anajua kwamba anapaswa kula kwa usahihi na kufanya mazoezi. Lakini wengi hawafanyi.
Kila anayetaka kujenga utajiri, anajua matumizi yanapaswa kuwa pungufu ya mapato, kisha kuweka akiba na kuwekeza. Lakini wengi hawafanyi.
Kila mwanafunzi anajua kufaulu mtihani anapaswa kujiandaa vyema kwenye masomo. Wengi hawafanyi.
Rafiki, kujua kile unachopaswa kufanya ili kupata matokeo unayotaka, bado haitoshi kukupa wewe mafanikio unayoyataka.
Na hili ndiyo limekuwa linawakwamisha wengi, tena wanasema kabisa, tayari najua yote hayo. Lakini cha kushangaza, hawafanyi.

Unachoweza kujiuliza kama mtu anajua na hafanyi, anajua kweli? Kama mti umeanguka porini na hakuna mtu aliyepo karibu, je unakua umetoa sauti?
Rafiki, kama unataka kupata mafanikio makubwa unayotaka kupata, wajibu wako ni mmoja, acha kujikwamisha wewe mwenyewe.
Na unaachaje kujikwamisha basi, ni kwa kujijengea nidhamu binafsi.
Nidhamu binafsi ni kufanya kile ambacho umepanga kufanya, iwe unajisikia kufanya au hujisikii.
Unakuwa na nidhamu binafsi pale unapopanga na kisha kufanya kama ulivyopanga, bila ya kujali nini kinaendelea.
Ukiweza hilo tu rafiki, mafanikio yoyote unayoyataka ni yako. Kwa sababu unakuwa na ushindani mdogo sana, maana wengi hawawezi kupanga na kufanya kwa muda mrefu bila kuacha.
Wengi sana hawaanzi hata kufanya. Na wapo wachache wanaoanza ambao hawafanyi kwa muda mrefu. Wachache mno, yaani kwa nadra sana ndiyo wanapanga na kufanya bila kuacha.
Kuwa mmoja wa hao wachache ili uweze kuvuna mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Najua unajiuliza mbona hasemi nafanyaje sasa ili niwe na nidhamu.
Rafiki, kama unasubiri jibu la miujiza, ambalo hujawahi kusikia, umeshapotea.
Unachopaswa kufanya ni KUPANGA NA KUFANYA.
Samahani, sina maneno mengine mazuri ya kuremba hilo kwako. Ni unapanga kufanya kitu, halafu unafanya kama ulivyopanga, bila ya kuacha.
Kama bado peke yako unashindwa kufanya bila kuacha, tafuta mtu atakayekuwajibisha. Mpate mtu ambaye utamwambia nini unafanya na adhabu ambayo utaipata kama hutafanya kile ulichopanga kufanya. Adhabu hiyo iwe kali sana kiasi cha kukuumiza kama hutafanya.
Kwa njia hiyo utalazimika kufanya kama ulivyopanga. Na ukisha weza hilo, hakuna chochote kitakachokushinda.
Rafiki, acha kujikwamisha mwenyewe kwa kupanga na kutokufanya. Anza kuwajibika kwenye kuhakikisha unafanya kila unachopanga ili uweze kujijengea mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa undani zaidi jinsi unavyoweza kujijengea nidhamu binafsi kali sana na itakayokupa mafanikio kwa uhakika. Karibu ujifunze ili uache kuwa kikwazo kwako mwenyewe.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.